Siasa

Mwapachu awashitukiza polisi

WAZIRI wa Usalama wa Raia, Bw. Bakari Mwapachu, amefanya ziara ya kushitukiza katika kambi za askari Polisi walioko mjini hapa kwa ajili ya ulinzi wakati wa vikao vya Bunge.

Na John Daniel, Dodoma


WAZIRI wa Usalama wa Raia, Bw. Bakari Mwapachu, amefanya ziara ya kushitukiza katika kambi za askari Polisi walioko mjini hapa kwa ajili ya ulinzi wakati wa vikao vya Bunge.


Ziara hiyo ya Waziri Mwapachu ilitokana na malalamiko yaliyotolewa na askari hao kupitia safu ya barua ya wasomaji kwenye gazeti moja la kila siku, wakilalamikia huduma duni za chakula na posho na kutaka viongozi wakuu wa Serikali akiwamo yeye kuchukua hatua ili kuwanusuru.


Akizungumza na Askari hao muda mfupi baada ya kuwasili eneo hilo la Kituo Kikuu cha Polisi Wilaya ya Dodoma jana, Bw. Mwapachu alisema amesikitishwa na malalamiko hayo, kwani
Serikali inawathamini askari hao na kwa sababu hiyo, Rais Jakaya Kikwete, aliamua kuunda wizara hiyo ili kushughulikia matatizo na kero zao haraka.


“Kwanza nawaomba radhi kuja ghafla bila taarifa, hata RPC (Kamanda wa Polisi Mkoa) wenu hayupo hapa, niliposoma malalamiko yenu jana kwenye gazeti nilisikitika sana, sisi
sote, IGP na RPC wenu tunawathamini sana.


“Rais aliunda Wizara hii ili kushughulikia matatizo yenu kwa haraka na kuimarisha ulinzi kwa wananchi wetu, sasa nimekuja kuwasilikiza, muwe huru kuniambia matatizo yenu ili yapatiwe ufumbuzi,” alisema Bw. Mwapachu na kukaa kusubiri kuambiwa malalamiko.


Bw. Mwapachu ambaye alifanya ziara hiyo ya ghafla muda ambao askari hao wanakula ili ajionee chakula wanachopewa, alisema yeye na wenzake katika Wizara hiyo, hawako tayari kuona askari wanapata shida iliyo ndani ya uwezo wao.


Hata hivyo, askari hao zaidi ya 40 waliokuwa kwenye mkutano huo wa dharura, walionekana kusita kutoa dukuduku kwa kile kilichosadikiwa ni kuwapo kwa baadhi ya viongozi wao akiwamo Mpelelezi wa Makosa ya Jinai wa Mkoa (RCO) na Msaidizi wa RPC, Kamishna Msaidizi wa Polisi Michael Kamhanda.


Mmoja wa askari hao, Koplo Kululetera kutoka Kondoa alisema wanapewa chakula, lakini wakigawiwa matunda asubuhi jioni hawapati na kwamba mayai wakati wa chai pia hawapati kila siku.


Kwa upande wake, Koplo Joshua kutoka Chamwino, alisema hakuna tatizo lolote na kwamba wanashangaa aliyetoa malalamiko hayo kwani wanahudumiwa vizuri.


Awali, akizungumza na Majira muda mfupi kabla ya mkutano huo, msimamizi wa upishi kwa askari hao, Bw. Anangise Kalile, alisema kwa kawaida askari hao hupewa chai ya maziwa kila asubuhi, mkate na mayai, mchana wanakula ugali, nyama, mboga za majani na matunda, jioni wali, maharage,mboga za majani na matunda na kwamba Jumamosi hula wali au ugali na kuku.


Baadhi ya askari waliozungumza na waandishi wa habari huku wakichukua chakula, walisema wanaridhishwa na chakula wanachoandaliwa katika kambi hiyo.


Akitoa maelezo mbele ya Waziri, Bw. Kamhanda, alisema tayari askari hao wamelipwa posho zao ya sh. 30,000 mara mbili na kwamba wako mbioni kuwalipa tena awamu ya tatu na watalipwa nauli za kwenda na kurudi walikotoka na kama fedha zitapatikana, watalipwa posho awamu ya nne.


Alisema vyakula wanavyoandaliwa askari hao ni vizuri na kwamba hawajapokea malalamiko yoyote kuhusu hali hiyo.


Baada ya maelezo hayo na ukimya kutawala bila askari kujitokeza kutoa kero, Bw. Mwapachu aliomba apewe chakula ili akionje mwenyewe kwa kuwa jana pia ilikuwa siku yake ya kuzaliwa, jambo ambalo lilitekelezwa haraka huku akisisitiza kuwa iwapo kila siku wanapikiwa kama jana, ni vizuri.


Hata hivyo, Waziri huyo aliwaomba waandishi wa habari kuondoka ili abaki na vijana wake kuzungumzia masuala ya ndani zaidi.


Source: Majira

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents