Siasa

Raza aponda kura ya maoni

Mfanyabiashara maarufu wa visiwani Zanzibar, Bw. Mohammed Raza, ameyaponda maamuzi ya Halmashauri Kuu ya CCM (NEC) ya kutaka kuitisha kura ya maoni juu ya serikali ya mseto

Na Mwinyi Sadallah, Zanzibar



 


Mfanyabiashara maarufu wa visiwani Zanzibar, Bw. Mohammed Raza, ameyaponda maamuzi ya Halmashauri Kuu ya CCM (NEC) ya kutaka kuitisha kura ya maoni juu ya serikali ya mseto kwa maelezo kwamba, hayana nguvu za kisheria.

Bw. Raza ambaye ni mmoja wa makada maarufu wa CCM, alitoa kauli hiyo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari nyumbani kwake Kibweni, mjini Zanzibar jana.

Alisema hadi sasa, hakuna sheria inayozungumzia uhalali wa kura hizo ya maoni juu ya serikali ya mseto.

Alisema ufumbuzi wa matatizo ya mpasuko wa kisiasa Zanzibar, utatatuliwa na Wazanzibari wenyewe na sio watu kutoka nje ya Zanzibar.

Alisema wakati umefika wa kuunda chombo kitakachowashirikisha Wazanzibari wenyewe kutatua matatizo yao ya kisiasa.

`Kama Wazanzibari tutaweka nia ya kweli, tukakaa pamoja, matatizo yanayotukabili tuna uwezo wa kuyatatua kwa saa tatu. `Kuitisha kura ya maoni, ni uvunjaji wa sheria kwa vile hakuna sheria Zanzibar inayozungumzia kuwepo kwa kura ya maoni, alisema.

Alisema mpasuko wa kisiasa Zanzibar, unaweza kutatuliwa na wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kwa vile ndiyo wawakilishi wa Wazanzibari kutoka vyama vya CCM na CUF.

Kwa mujibu wa Bw. Raza, Watanzania lazima wasome miafaka miwili ilivyokwama ukiwemo ule wa mwaka 1999 uliosimamiwa na aliyekuwa Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola, Chifu Ameka Anyauko.

Mwingine ni wa sasa baina ya Makatibu Wakuu wa vyama hivyo.

Aliitaka CCM na CUF kuaandaa mazingira mazuri yatakayowezesha kufanyika uchaguzi huru na wa haki kwa vile Rais Amani Abeid Karume amebakiza muda mfupi kumaliza kipindi chake.

Kada huyo wa CCM alisema muda uliobakia kuwezesha wananchi kupewa elimu juu ya kura ya maoni ni mdogo, kwa vile wengi hawafahamu suala hilo.

Alisema juhudi zinazochukuliwa na Rais Jakaya Kikwete katika kuleta maelewano visiwani humo ni changamoto kwa Wazanzibari kuwa tayari kukaa pamoja kutatua matatizo yao.

Sisi wananchi tumuombee dua Rais Kikwete, ikiwa misikitini na makanisani apate nguvu ya kutatua matatizo ya Zanzibar.

Jambo la msingi awe mkweli kwa vile wapo viongozi wengine Afrika huanza vizuri, lakini baadaye hubadilika, alisema Bw. Raza.

Mfanyabiashara huyo alisema Wazanzibar lazima wajifunze kutokana na yale yaliyotokea Kenya na kuhakikisha maslahi ya Taifa yanawekwa mbele na kujenga mshikamano.

Kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM kilichofanyika mwishoni mwa mwezi uliopita huko Butiama, kiliamua Wazanzibar waulizwe juu ya ridhaa yao ya serikali ya umoja wa kitaifa kupitia kura ya maoni.

Kauli hiyo ya Bw. Raza inafanana na ile iliyotolewa hivi karibuni na Katibu Mkuu wa CUF, Bw.Seif Sharif Hamad, aliyemtaka Rais Kikwete, amkutanishe na Rais wa Zanzibar kujadili mpasuko wa kisiasa Zanzibar na ufumbuzi wake.


 


Source: Nipashe

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents