Siasa

Sababu za rais wa Marekani Biden kuiondolea Tanzania vikwazo vya kuingia nchini humo

Rais mpya wa Marekani Joe Biden amewaondolea raia wa Tanzania vikwazo vya kushiriki bahati nasibu ya viza, mwaka mmoja baada ya kutangazwa kwa vikwazo hivyo.

Januari 30, 2020 serikali ya Donald Trump ilitangaza kuwawekea Watanzania vikwazo vya kushiriki bahati nasibu hiyo pamoja na raia wa nchi nyingine kadhaa.

Kwa mujibu wa afisa mmoja mwandamizi wa utawala uliopita wa Trump, nchi hizo ziliwekewa marufuku hiyo kwa kushindwa kufikia “kiwango stahiki cha ulinzi na kupashana taarifa”.

“Nchi hizi, kwa sehemu kubwa, zinataka kutoa msaada lakini kwa sababu mbali mbali zimefeli kufikia viwango vya chini tulivyoviweka,” aliyekuwa Naibu Waziri wa Usalama wa Ndani wa Marekani Chad Wolf aliwaambia wanahabari baada ya kutangazwa kwa vikwazo.

Hii leo, Ubalozi wa Marekani nchini Tanzania umetangaza kuwa marufuku hiyo imefutwa rasmi na rais mpya wa nchi hiyo Joe Biden aliyeingia madarakani juzi Jumatano.

“Mojawapo kati ya hatua zake za mwanzo kabisa akiwa Rais, Rais Biden ameondoa kikwazo kilichowekwa kwa Watanzania kuomba Viza ya Bahati Nasibu (Diversity VISA – DV),” ubalozi huo umeandika kupitia ukurasa wake wa Twitter.

Bahati nasibu hiyo ilipitishwa kisheria nchini Marekani mwaka 1990 na bahati nasibu ya kwanza ikafanyika mwaka 1995.

Toka wakati huo, takribani watu 50,000 kila mwaka kutoka nchi mbalimbali duniani hushinda bahati nasibu hiyo na kupata viza ya kuingia Marekani na kufanya kazi kama wakazi wa kudumu.

Washindi wa viza hiyo pia huweza kuhamia nchini humo na wenza wao pamoja na watoto walio chini ya umri wa miaka 21.

Kwa mujibu wa taarifa za Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani, katika kipindi cha miaka 10 kutoka 2008 mpaka 2018, jumla ya Watanzania 643 walishinda bahati nasibu hiyo.

Katika kipindi hicho, mwaka ambao Watanzania walishinda wengi zaidi ilikuwa 2009 watu 137 na mwaka ambao walishinda wachache ilikuwa mwaka 2014 watu 28.

Zaidi ya Watanzania 10,000 hutuma maombi ya kushiriki bahati nasibu hiyo.

Kwa mwaka 2017 pekee, Watanzania 13,733 walituma maombi, kati yao 6,919 waliingia kwenye kinyang’anyiro na mwishowe walioshinda bahati nasibu walikuwa 46.

Hata hivyo, ushiriki na ushindi wa Watanzania ni mdogo ukilinganisha na baadhi ya mataifa barani Afrika.

Sudan nayo ambayo imepigwa marufuku kama Tanzania katika kipindi hicho cha mwaka 2008-2017 raia wake 8,127 walishinda bahati nasibu hiyo.

Majirani wa Tanzania nchi ya Kenya katika miaka 10 hiyo imeshuhudia raia wake 15,172 wakishinda bahati nasibu hiyo.

Kwa mwaka 2017 pekee, Wakenya 360,023 walituma maombi, kati yao 249,397 waliingia kwenye kinyang’anyiro na mwishowe walioshinda bahati nasibu walikuwa 1,014.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents