Bongo5 Makala

Sanaa isiwe ngazi ya kutengeneza maskini wenye majina – Joe Makini

Umewahi kujiuliza kwanini wasanii wanaotajwa kupiga show sehemu ni kama wale wale tu? Ukisikia tangazo la show sehemu fulani siku hizi majina yanayotawala ni Diamond, AY, Roma, Ommy Dimpoz na wengine wanaohesabika!

Hawa wasanii wengine ambao nyimbo zao tunazisikia kila siku kwenye radio wanaishi vipi? Hawa akina nanihii hawa! mbona hatuwasikii kwenye matangazo kuwa watapiga show sehemu? Ama kama anavyosema Joe kuwa Sanaa ya Tanzania ni ngazi ya kutengeneza maskini wenye majina makubwa nchini!!

Ni kweli. Utamfikiriaje msanii mwenye ngoma kali redioni na mashabiki wanaiomba kila siku, akikusimamisha kukuomba ‘buku’ ya nauli? Usishangae ikikutokea hivyo kwakuwa jina na maisha halisi ya wasanii wengi ni kama maji na oil, havichanganyiki.

Ni wasanii wachache mno uwajuao Tanzania wana maisha mazuri. Wale wajanja waliligundua hili mapema mno wakaamuua kurudi shule. Wengine wameshapata kazi nzuri na muziki wanaufanya kama hobby tu. Ulipe usilipe poa tu, haina noma na maisha yanasonga!!

Wale wenzetu na sisi waliokimbia umande kwa kunogewa na umaarufu wa mwaka mmoja na kushobekewa na warembo, sasa hivi mambo magumu kichizi. Kwani hujasikia Dudu Baya juzi kampiga mtangazaji wa radio kisa kanyimwa show!,mambo hayaendi. Unaweza ukapita hata mwezi hajapigiwa hata simu ya kumpa show ya laki mbili! Wasanii wasiosikika kama yeye siku hizi inabidi watafute show hata kwa ubabe!

Sasa wale wapi wakati hawana issue zingine? Juzi tu hapa, Richie One alikamatwa na polisi baada ya kujifanya Alikiba. Yeye kama yeye pamoja na kuwa na jina kubwa hawezi kupata show. Ana familia inamtegemea, michongo hamna, kwanini asijifanye Alikiba? Ahhhhhh! Kwanini afe na njaa wakati akili anazo? Piga sana magumashi mjini! Ukiingia kwenye kumi na nane zake, anakupiga changa la macho, mjini hapa!!

Lakini seriously guys, huu muziki wa Bongo mbona uko hivi? Kwanini wakongwe wanaabika sana mjini wakati majina yao makubwa kuliko hata baadhi ya mawaziri. Kuna mtu asiyemjua Daz Baba? Hata kama wapo si wengi kama ambavyo ukimwambia mwananchi wa kawaida amtaje aliyekuwa waziri wa elimu miaka kumi iliyopita.

Tuliwahi kupata story kuwa O-Ten anakaanga chips mitaa ya Mwenge, Dar es salaam. Iwe ni kweli ama uzushi, hatushangai yeye kufanya hivyo kwakuwa game ni kama limeshamkataa tayari.

Pata picha mzee wa ‘Nichek’ anakukaangia ‘kiepe’ cha ukweli somewhere!! Duu! Sio fair kabisa. Muziki wa Bongo una pressure sana kwakweli. Huchelewi kuongea mwenyewe barabarani wakati wimbo wako upo kwenye Top Ten!

Tunakubaliana na Joe Makini, kuwa sanaa haitakiwi kuwa ngazi ya kutengeneza maskini wenye majina. Umaarufu bila maisha mazuri ni sawa na mboga isiyokuwa na chumvi.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents