Siasa

Serikali yakanusha kumuua Ballali

Bernard MemberSERIKALI imesema haihusiki na kifo cha aliyekuwa Gavana wa Benki Kuu (BoT), Dk. Daudi Ballali kama uvumi unaoendelea kuvumishwa na watu mbalimbali kuhusu kifo hicho

 

 

Veronica Mheta

 
SERIKALI imesema haihusiki na kifo cha aliyekuwa Gavana wa Benki Kuu (BoT), Dk. Daudi Ballali kama uvumi unaoendelea kuvumishwa na watu mbalimbali kuhusu kifo hicho.

Aidha serikali imesema kama kuna mtu yeyote ana uthibitisho wa kitabibu kutoka Marekani ambako Ballali alikuwa amelazwa kuwa Serikali imehusika na kifo hicho ajitokeze hadharani na aonyeshe ushahidi huo.

“Madai kama haya ni vyema yakatolewa na ambaye ameongea na daktari aliyekuwa akimtibu Dk. Ballali nchini Marekani na awe ameona cheti cha kifo chake na kuiletea serikali huyo ana haki ya kuituhumu Serikali,” alisema Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Benard Membe.

Membe alikanusha tuhuma hizo wakati akijibu maswali ya waandishi wa habari katika mkutano aliouitisha kuzungumzia Mapendekezo yaliyojitokeza katika mkutano wa Kamati ya Marais 12 wa Umoja wa Afrika uliomalizika mkoani Arusha hivi karibuni.

Membe alisema anashangazwa na uvumi huo na namna watu wanavyohoji kuhusu kifo cha Ballali kuwa kina utata; lakini akasisitiza kuwa serikali haiwezi kumuua gavana bali kifo chake ni cha kawaida.

Membe alisema ikiwa kuna mwandishi wa habari au mtu yeyote ana uthibitisho wa daktari aliyekuwa anamtibu ugonjwa uliokuwa ukimsumbua Dk. Ballali hadi kufikia mauti autoe hadharani.

Alisema ni daktari tu aliyekuwa anamtibu gavana huyo wa zamani mwenye kujua aina ya ugonjwa uliomuua. “Nitakuwa mkali sana ikiwa serikali inavumishiwa uongo, hivi kwanini watu wanaituhumu serikali, si vizuri kuituhumu serikali bila ushahidi.”

Membe ambaye alionyesha kutofurahishwa na tuhuma kwa serikali kuhusika na kifo cha Ballali alihoji tena “ Hivi kwa nini watu wasiituhumu serikali tangu mwanzo wa ugonjwa wake badala yake waituhumu serikali baada ya kifo chake si vizuri.”

Kauli ya Membe inatokana na shutuma mbalimbali ambazo zimekuwa zinatolewa hasa na wanasiasa kuhusiana na kifo cha Ballali. Wa kwanza kuonyesha mashaka kuhusiana na kifo hicho alikuwa Mbunge wa Karatu, Dk. Wilbroad Slaa aliyetaka kuundwa kwa tume kuchunguza kifo chake.

Pia kiongozi wa upinzani bungeni, Hamad Rashid Mohamed naye alisema Ballali alikuwa shahidi muhimu katika kesi ya ufisadi wa Sh bilioni 133 zilizochotwa katika akaunti ya EPA, hivyo usiri juu ya kifo chake unazusha maswali mengi.

Hamad alisema usiri wa serikali juu ya ugonjwa hadi kifo cha gavana huyo kunazusha maswali mengi miongoni mwa wananchi na ili kuondoa minong’ono hiyo ni vyema tume ikaundwa kuchunguza kifo hicho.

Juzi Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alidai kifo cha Ballali kina mkono wa baadhi ya vigogo wa serikali kwa sababu alikuwa shahidi muhimu katika vita ya ufisadi.

Chama cha NCCR Mageuzi pia juzi kimetoa tamko kuwa ni vyema ikaundwa tume ya kimataifa kuchunguza chanzo cha kifo hicho kutokana na usiri uliofanywa na serikali.

Naye Mabere Marando ambaye ni mwanasheria aliyebobea, alisema usiri uliofanywa na serikali juu ya ugonjwa hadi kifo cha Ballali ni wazi kuwa kuna jambo linalofichwa licha ya kuwa ilikuwa inafahamu hospitali alikokuwa anatibiwa.

Lakini pia alihoji sababu ya Tume iliyoundwa na Rais Jakaya Kikwete kuchunguza tuhuma za ufisadi wa EPA kutomhoji Ballali kuwa ni ishara nyingine namna kifo cha gavana huyo wa zamani ilivyozungukwa na wingu jeusi.

Baadhi ya vyombo vya habari pia vimeripoti kuwa ndugu wa Ballali wanaamini kuwa ndugu yao ameuawa kama alivyofanyiwa Horace Kolimba na Waziri Mkuu wa zamani Edward Moringe Sokoine.

 

 

 

Source: HAbari Leo

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents