Habari

Soko la Kariakoo hasara tupu kwa miaka 15

Soko la Kariakoo Jijini Dar es Salaam, limekuwa likiendeshwa kwa hasara katika kipindi cha zaidi ya miaka 15.

Na Dunstan Bahai



Soko la Kariakoo Jijini Dar es Salaam, limekuwa likiendeshwa kwa hasara katika kipindi cha zaidi ya miaka 15.


Pamoja na matatizo mengine yanayolikabili soko hilo, imeelezwa kwamba yote husababishwa na kutofahamika mmiliki halali wa soko hilo, kati ya TAMISEMI na Jiji la Dar es Salaam.


Meneja Mkuu wa soko hilo, Kuboja Munu, aliitoa maelezo hayo kwa kamati ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala jana wakati ilipotembelea sokoni hapo.


Alisema soko hilo limekuwa likikabiliwa na matatizo mengi na wakati mwingine limekuwa na matumizi makubwa kuliko mapato na kwamba sasa lina hasara ya sh. milioni 532.


Kauli hiyo iliwashitusha wajumbe wa kamati hiyo na kuhoji ni vipi kuwepo na matumizi makubwa ikilinganishwa na mapato.


Alisema, katika kukabiliana na matatizo hayo, menejimenti imepanga mikakati mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuuza nyumba za shirika zilizoko Tabata na Mbezi na kufuatiwa na kupunguza wafanyakazi.


Meneja huyo alisema, shirika la Masoko Kariakoo lina jumla ya wafanyakazi 160, na wanaotarajiwa kupunguzwa ni nusu na linakusudia pia kupandisha viwango vya kodi kutoka sh. 1000 kwa mita ya mraba kwa mwezi hadi sh. 1,500, kiwango alichosema kuwa bado ni kidogo ikilinganishwa na pango la sh. kati ya 6000 na 8000 kwa maduka ya jirani.


Kwa mujibu wa meneja mkuu huyo, baada ya kupunguza wafanyakazi hao, shirika litakuwa limeokoa fedha zilizokuwa za malipo ya mishahara yao na sare kwa askari ikiwa ni pamoja na huduma ya matibabu.


Vyanzo vikuu vya mapato ya soko hilo ni pamoja na ushuru wa mazao, ada ya kutumia soko, kodi ya pango, marejesho ya maji na umeme, ada ya usaili na vitambulisho, michango ya wafanyakazi na michango mingine itokanayo na matangazo kwenye mabango, minada na maegesho ya magari.


Mbunge wa Ubungo, Charles Keenja alithibitisha kuwa soko hilo huendeshwa kihasara, kitu ambacho alisema hawakutegemea kwani kila siku mazao yanaingizwa kwa wingi kutoka karibu mikoa yote.


Bw. Keenja alishawahi kuwa Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam.
Alisema, mfumo mbaya wa uendeshaji wa soko hilo ikiwa ni pamoja na kutofahamika mmiliki halali, ndivyo vinavyochangia hasara hizo ikiwa ni pamoja na menejimenti kutokuwa na mikataba ya uwazi na wapangaji wao, hali inayosababisha mpangaji kukataa hata kulipa pango na hata akienda mahakamani kuwepo uwezekano wa kushinda.
Alishauri serikali ijiondoe kufanyabiashara moja kwa moja kwenye soko hilo na badala yake lipewe Jiji.


Kwa mujibu wa Keenja, lengo la kuwepo kwa soko hilo ilikuwa kujenga masoko mengine yatakayokuwa chini ya uangalizi wa menejimenti ya soko hilo, lakini imekuwa kinyume kwani hakuna hata soko moja lililojengwa chini ya mpango huo.


Baadhi ya wajumbe wa kamati hiyo walionyesha wasiwasi wa taarifa ya meneja huyo na kwamba imejaa ujanja mwingi na inayoonyesha mashaka makubwa.


Mwenyekiti wa kamati hiyo, George Lubeleje ambaye ni mbunge wa Mpwapwa, alisema wanatarajia mwezi ujao kukutana na waziri wa TAMISEMI na maofisa wake na kwamba suala la uendeshaji wa soko hilo litakuwa ni moja ya agenda kubwa muhimu.


Kwa ujumla kamati hiyo haikuridhishwa na uendeshwaji wa soko hilo na kwamba inahitajika nguvu ya ziada katika kuliboresha.


Source: Nipashe

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents