Siasa

Tanzania yakataa kituo cha kijeshi cha Marekani

NCHI za Afrika ikiwamo Tanzania zimelikataa ombi la Marekani la kutaka kuanzisha kituo kikubwa cha kijeshi katika Bara la Afrika (Africom), imefahamika.

na Mwandishi Wa Tanzania Daima

 

 

 

NCHI za Afrika ikiwamo Tanzania zimelikataa ombi la Marekani la kutaka kuanzisha kituo kikubwa cha kijeshi katika Bara la Afrika (Africom), imefahamika.

 

 

 

Taarifa zilizopatikana jana kupitia Shirika la Habari za Uingereza (BBC) na baadaye kusambazwa na Ikulu, zilieleza kuwa, hakuna hata nchi moja barani humu iliyoonyesha nia au dhamira ya kuiruhusu Marekani kujenga kituo hicho katika ardhi yake.

 

 

 

Hapa nchini, kulikuwa na taarifa ambazo hazikuthibitishwa, lakini zikiibuliwa na wanazuoni na watu wengine wenye ushawishi katika masuala ya ulinzi na usalama kuwa Marekani ilikuwa imeiomba Tanzania kuipatia ruhusa kujenga kituo hicho katika ardhi yake.

 

 

 

Wasomi na wanazuoni hao waliibua taarifa hizo kwa misingi ya kuionya serikali isije ikakubaliana na ombi hilo, kwa sababu ingekuwa ni aina fulani ya kujiingiza katika utumwa wa nchi hiyo ambayo imefanikiwa kuonyesha ubabe wake sehemu kadhaa duniani.

 

 

 

Taarifa hiyo ya BBC ilieleza kuwa ni Liberia pekee, ndiyo iliyoonyesha nia ya kutaka kuwa ‘mwenyeji’ wa kituo hicho huku nchi nyingine zikisita kufanya hivyo.

 

 

 

Baada ya nchi za Afrika kutoonyesha nia ya kuruhusu kujengwa kwa kituo hicho, Jeshi la Marekani limeamua kuyaacha makao makuu ya kikosi hicho nchini Ujerumani yaliko hivi sasa.

 

 

 

Nchi nyingi za Afrika zimeonyesha wasi wasi wa kuruhusu kujengwa kwa kituo hicho kinachojulikana kwa Kiingereza kama Africom. Kamanda wa kituo hicho, Jenerali William Ward, alithibitisha kuwa mipango ya kujenga kituo kikubwa cha kijeshi barani Afrika imekufa.

 

 

 

Kituo hicho kilianzishwa mwaka jana kwa lengo la kuunganisha na kuratibu shughuli za vikosi vingine vitatu vya kijeshi vya Marekani. Jenerali Ward aliiambia BBC kuwa nchi nyingi za Afrika hazikuelewa maana halisi ya kituo hicho na ndiyo maana zimekuwa na wasiwasi.

 

 

 

Alisema kuwa lengo kubwa la Africom lilikuwa ni kujenga uwezo wa nchi za Afrika katika masuala ya ulinzi na kutunza amani.

 

 

 

Hata hivyo, Rais wa Nigeria, Umaru Yar’Adua, alitangaza mwezi Novemba mwaka jana kuwa asingeruhusu nchi yake iwe mwenyeji wa kituo hicho na kuwa anapinga kuwepo kwa kituo hicho katika nchi nyingine yoyote katika ukanda wa Afrika Magharibi. Msimamo huo ulionyeshwa pia na Afrika Kusini na Libya.

 

 

 

Kuna taarifa kuwa kuanzishwa kwa kituo hicho ni jitihada za Marekani kulinda masilahi yake katika masuala ya mafuta na madini barani Afrika kutokana na kukua kwa ushindani kutoka nchi za Asia.

 

 

 

Pia kulikuwa na wasiwasi kuwa, kuanzishwa kwa kituo hicho kunaweza kulifanya Bara la Afrika kuanza kujihusisha moja kwa moja katika vita dhidi ya ugaidi ambayo kwa upande mwingine imekuwa ikichukuliwa na makundi mbalimbali ya kidini kuwa ni vita yenye lengo la kuuangamiza Uislamu.

 

 

 

Hata hivyo, Jenerali Ward alisema kuwa Africom haihusiani na masuala ya kuitawala kijeshi Afrika, zaidi ya kuratibu shughuli mbalimbali za kijeshi katika kituo kimoja, huku Afrika ikisaidiwa katika mafunzo ya kijeshi, kulinda amani na shughuli za utoaji misaada.

 

 

 

Katika taarifa iliyotolewa na Ikulu, Mwandishi Msaidizi wa Rais Jakaya Kikwete, Premmy Kibanga, alifafanua kuwa: “Nimeona niwatumie hii article (habari) kuhusu Africom kama ilivyoandikwa na BBC, kwa vile kumekuwa na habari nyingi katika baadhi ya vyombo vya habari na pia kutoka kwa wasomi na wanazuoni mahiri hapa nchini kwetu ambao wamesimama kidete kuhusisha ziara ya Rais George Bush hapa Tanzania na kituo hicho cha kijeshi licha ya juhudi mbalimbali za Rais kuelezea wazi katika taarifa na hata hotuba yake kwa wananchi mwishoni mwa mwezi Januari.”

 

 

 
Source: Tanzania Daima

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents