Siasa

TUCTA yamuonya Kapuya

SHIRIKISHO la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA), limesema limeridhia mchakato wa mabadiliko ya mishahara unaofanywa na serikali, ili kupunguza matatizo yanayotokea hivi sasa katika sehemu za kazi, huku likiionya serikali kuwa makini na utekelezaji wa hatua hiyo.

na Salehe Mohamed

 

 

 

SHIRIKISHO la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA), limesema limeridhia mchakato wa mabadiliko ya mishahara unaofanywa na serikali, ili kupunguza matatizo yanayotokea hivi sasa katika sehemu za kazi, huku likiionya serikali kuwa makini na utekelezaji wa hatua hiyo.

 

Akizungumza na Tanzania Daima jijini Dar es Salaam jana, Naibu Katibu Mkuu wa TUCTA, Nicholous Mgaya, alisema kuwa hatua iliyochukuliwa na serikali itasaidia kupunguza au hata kumaliza kabisa matatizo yaliyojitokeza baada ya kutangazwa kwa viwango vipya vya mishahra mwishoni mwa mwaka jana.

 

Hata hivyo, Mgaya aliwalaumu wafanyabiashara wenye viwanda kuwa ndio chimbuko na sababu ya malalamiko na vurugu zilizotokea kutokana na kutangazwa kwa mishahara mipya.

 

Akifafanua alisema kuwa, wafanyabiashara hao walishindwa kuwasilisha vielelezo vya biashara zao wakati bodi za mishahara zilipopita kuratibu zoezi la mshahara, hivyo bodi hizo kutopata takwimu sahihi zilizohitajika.

 

Aidha, aliionya serikali kuhusu kusikiliza madai ya wafanyabiashara hao, kwani wanaweza kufanya mambo ili kulinda masilahi yao, badala ya wafanyakazi ambao hufanya shughuli zao katika mazingira magumu.

 

“Hawa wafanyabiashara wenye viwanda ndio walioleta mvurugano huu, kwani wao hawakuwa tayari kutoa ushirikiano walipofuatwa na bodi za ajira, hivyo ni vema safari hii serikali ikakaa chonjo,” alionya Mgaya.

 

Alisema iwapo serikali haitakuwa makini katika utendaji wake, kuna kila dalili vikaibuka vyama mbalimbali kupinga mishahara iliyotangazwa na serikali bila kuangalia masilahi ya wengi.

 

“Kama tusipokuwa makini, kamwe hatutaweza kufikia malengo yetu, kwani leo hii wataibuka wafanyabiashara hawa, kesho wale, ilimradi kila mtu anavutia upande wake, na mwisho wa siku itakuwa vurugu kama ilivyo hivi sasa,” alisema Mgaya.

 

Katika hatua nyingine, TUCTA imesema imeanza maandalizi kwa ajili ya sherehe za Sikukuu ya Wafanyakazi Duniani (Mei Mosi), itakayofanyika kitaifa mkoani Iringa, ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Rais Jakaya Kikwete.

 

Kauli hiyo ya TUCTA inakuja siku moja tu baada ya Waziri wa Kazi, Ajira na Maendeleo ya Vijana, Profesa Juma Kapuya, kutangaza kuhusu kuundwa kwa kamati mpya itakayopitia viwango hivyo vya mishahara na kutoa mapendekezo mapya.

 

Kapuya alisema hatua hiyo inatokana na msimamo uliowekwa na baadhi ya waajiri, ambao wamekataa katakata kulipa viwango vipya vya mishahara vilivyopangwa na kutangazwa na serikali mwishoni mwa mwaka jana.

 

Alisema utafiti huo mpya umepangwa kuchukua siku 60, kuanzia Machi 10 mwaka huu, na katika kipindi cha utafiti huo mpya, mishahara itakayolipwa ni ile iliyotangazwa na serikali Novemba mwaka jana.

 

 

 

 

 

Source: Tanzania Daima

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents