Siasa

Viongozi wa dini wapewa kazi

SIKU chache baada ya kikundi cha Wazanzibari kumi kutuma waraka kwa Chama cha Wananchi (CUF) kukitaka kujiondoa katika mazungumzo ya kusaka suluhisho la mpasuko Zanzibar, wametuma waraka mwingine kwa viongozi wa dini kuhusu suala hilo hilo la mapasuko wa kisiasa Zanzibar.

na Mwandishi Wa Tanzania Daima


SIKU chache baada ya kikundi cha Wazanzibari kumi kutuma waraka kwa Chama cha Wananchi (CUF) kukitaka kujiondoa katika mazungumzo ya kusaka suluhisho la mpasuko Zanzibar, wametuma waraka mwingine kwa viongozi wa dini kuhusu suala hilo hilo la mapasuko wa kisiasa Zanzibar.


Safari hii, watu hao, wanaojitaja kama wawakilishi wa wakazi wa mikoa mitano ya Zanzibar, wameuelekeza waraka wao kwa viongozi wa dini nchini.


Waraka huo umetumwa kwa Polycarp Kardinali Pengo wa Kanisa Katoliki, Mufti Mkuu wa Tanzania, Alhaj Shaaban bin Issa Simba na Mufti Mkuu wa Zanzibar, Alhaj Sheikh Haridhi bin Khelef.


Aidha, waraka umeelekezwa pia kwa Askofu Mkuu wa Kanisa Anglikana nchini, Donald Mtetemela, Askofu Msaidizi wa Jimbo Katoliki Dar es Salaam, Method Kilaini, Naibu Mufti wa Zanzibar, Alhaj Saleh Kabi, Askofu Augustino Shao na Kadhi Mkuu wa Zanzibar, Sheikh Ali Khatib Mranzi.


Katika waraka huo, waliouita kuwa ni wa wazi kwa viongozi wa dini Tanzania, juu ya kuumaliza mpasuko wa kisiasa wa Zanzibar, watu hao wamewataka viongozi wa dini kufanya hima kuonana na Rais Jakaya Kikwete na Amani Karume wa Zanzibar.


“Tunakuombeni mchukue juhudi za haraka za kukutana na Mhe Rais Kikwete, (na) Mhe Amani Karume, kuwaeleza yakuwa, jamii ya Wazanzibari wanahitaji, tena kwa haraka, kuona ufumbuzi wa mgogoro wa kisiasa Zanzibar unafikiwa na kumalizwa ili ufumbuzi uweze kupatikana,” inasomeka sehemu ya waraka huo ambao nakala yake imetumwa kwa vyombo vya habari.


Kwa mujibu wa watu hao, ufumbuzi huo ndio utaviepusha Visiwa vya Zanzibar kutumbukia au kutumbukizwa katika dimbwi la machafuzi kwa sababu tu kuna viongozi walio ndani ya madaraka, ambao wanaweka mbele maslahi yao binafsi kuliko kuweka mbele maslahi ya taifa.


Watu hao wanasema kuwa, ni wakati mwafaka sasa kwa viongozi wa kidini nchini kutumia busara zao na kuvunja ukimya.


Wanasema kuwa, watawala walio ndani ya madaraka ni sehemu ya waumini wao ambao wanatakiwa wafuate mafundisho yao kwa madhumuni hayo.


“Ni wakati mwafaka wa kuingilia kati mtafaruku huu wa kisiasa unaohatarisha amani nchini mwetu. Tunawahitaji na tunawategemea yakuwa mtakutana kwa haraka ili muweze kukutana na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kumuelezea matakwa yetu, ili ufumbuzi wa kudumu uweze kupatikana hapa Zanzibar,” inaongeza tarifa hiyo.


Wanadai uamuzi wao huo ni njia ya kuonyesha jinsi wanavyowaheshimu viongozi ambao wana jukumu la kuhakikisha amani inadumu nchini.


Waliwataka viongozi hao kuchukua hatua za kuhakikisha kuwa, mpasuko wa kisiasa Zanzibar unapata ufumbuzi wa haraka na wa kudumu.


“Kwa heshima, tunamalizia hapa tukiamini maombi yetu mutayafanyia kazi, tena kwa uwazi na kwa haraka, huku jamii ikifuatilia juhudi zenu, ambazo tunaamini zitakuwa za wazi kiasi ambacho kila mtu atasikia, ama kuona katika kipindi kifupi hiki kijacho,” inasomeka sehemu ya waraka huo.


Wanasema kuwa, wameamua kulipeleka suala hilo mikononi mwa viongozi wa kidini kwa dhamira njema kabisa na wanaamini Mungu, anayaelewa yaliyo ndani ya nyoyo na nafsi zao, atawasaidia kuyanusuru yale yaliyotokea na kufanywa katika nchi mbalimbali.


Waliwataka viongozi hao wa dini kulifanyia suala hilo uharaka ili katika muda mfupi, wananchi wapate taarifa kuhusu hatua za mwisho za kumalizwa kwa mgogoro huu wa kisiasa wa Zanzibar.


“Kinyume cha hayo, ikiwa ujumbe wetu huu utakapopokewa na kuwasilishwa kwa wanaohusika, nao wakadharau, watawala wawe tayari kubeba dhima kwa lolote lile litakaloanza kutokea, nasi tunaamini wengi watakuwa wameshaona juhudi mbalimbali tulizozichukua kuhakikisha mgogogro wa kisiasa unamalizika Zanzibar,” unasema waraka huo.


Watu hao wanasema wameamua kuwatumia viongozi wa dini kulikabili suala hilo baada ya kuona juhudi zao kwa kipindi kirefu, zikidhihirisha uwezo wao wa kuwafanya Watanzania wengi kushika ibada na kumuabudu Mungu.


“Haya yote mumekuwa mukiyafanya na mkiyaelekeza pasi na kuchoka na hata kufikia jamii ikatambua kwamba nyinyi ni viongozi wao, na ndio maana kwa utambuzi huo wa utukufu wenu sisi Wazanzibari, kwa niaba ya wenzetu tunaleta maombi haya mbele yenu,” unasema waraka huo.


Waliwaonya viongozi hao wa dini kutokukaa kimya ili kuzuia matukio kama yaliyotokea Rwanda na kufikia kupotezwa kwa roho za watu wasiopungua 800,000.


Walioandika waraka huo, wamejitaja kuwa ni Hassan Jaffar Bakar na Ubwa Kombo Mkangaa (Kusini Unguja), Fadhili Omar Kheri na Mtumwa Alli Makame (Kaskazini Unguja), Zubeir Mzee Juma na Yussuf Abdulrahman Himid (Mjini Magharibi).


Pia wamo Awesu Mgunya Bakar na Mwanakheri Sadifa Mtwana (Kusini Pemba) pamoja na Mussa Othumani Uledi na Masoud Khalid Hamad kutoka Kaskazini Pemba.


Nakala ya waraka huo, imepelekwa pia kwa Rais Kikwete, Makamu wa Rais, Dk. Ali Mohamed Shein, Waziri Mkuu, Edward Lowassa, Rais Karume, Spika wa Bunge, Samwel Sitta, Spika wa Baraza la Wawakilishi, ofisi za mabalozi Dar es Salaam na wahariri wa vyombo vya habari.


Source: Tanzania Daima

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents