Siasa

Zitto ateuliwa kwenye kamati ya mikataba ya madini

Zitto KabweRAIS Jakaya Kikwete amemteua Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema), Zitto Kabwe kuwa mmoja wa wajumbe wa Kamati ya uangaliaji upya mikataba ya uchimbaji wa madini nchini.

Zitto Kabwe


RAIS Jakaya Kikwete amemteua Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema), Zitto Kabwe kuwa mmoja wa wajumbe wa Kamati ya uangaliaji upya mikataba ya uchimbaji wa madini nchini.


Kamati hiyo itakuwa na jumla ya wajumbe 11 na itakuwa chini ya uenyekiti wa aliyewahi kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Mark Bomani.


Wajumbe wengine watakaokuwa kwenye Kamati hiyo ni Mbunge wa Bariadi Mashariki (UDP), John Cheyo, Mwanasheria wa Wizara ya Nishati na Madini, Salome Makange, Kamishina wa Sera Wizara ya Fedha, Mugisha Kamugisha, Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Makazi Wizara ya Ardhi, Edward Kihundwa na Mbunge wa Kyela (CCM), Dk. Harrison Mwakyembe.


Wajumbe wengine ni Mbunge wa Msalala (CCM),Ezekiel Maige, Peter Machunde kutoka Soko la Hisa, Dar es Salaam (DSE), Mkaguzi wa Mahesabu kutoka Kampuni ya Kimataifa ya Ukaguzi wa Mahesabu, PriceWater Coopers, David Tarimo ambaye ni mtaalam wa masuala ya kodi na Mkurugenzi wa Madai na Sheria za Kimataifa, Wizara ya Katiba na Sheria, Maria Kejo.


Taarifa ya Ikulu iliyosainiwa na Katibu Mkuu Kiongozi, Philemon Luhanjo ilisema kuwa pamoja na mambo mengine, kamati hiyo pia itakuwa na kazi ya kuchambua mfumo wa kodi unaotumika katika sekta ya madini na kupitia mfumo wa usimamizi wa shughuli za uchimbaji mkubwa unaofanywa na serikali.


Kamati hiyo imepewa muda wa miezi mitatu kukamilisha kazi yake pia imepewa jukumu la kukutana na taasisi zinazosimamia madini na wadau wengine na kutakiwa kutoa taarifa yenye mapendekezo.


Kuundwa kwa Kamati hiyo kunafuatia hoja binafsi ya Zitto Kabwe aliyoitoa bungeni kutaka kuundwa kwa Kamati Teule yakuchunguza mazingira ya kusainiwa kwa mkataba wa mgodi wa dhahabu wa Buzwagi huko Uingereza na Waziri wa Nishati na Madini, Nazir Karamagi Februari mwaka huu.

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents