Habari

TRA yaweka wazi makusanyo ya kodi mwaka 2016/2017

Mamlaka ya Mapato Tanzania(TRA), imefanikiwa kukusanya kiasi cha shilingi Trilioni 14.4 kwa mwaka wa fedha 2016/17.

Makusanyo haya ni sawa na ukuaji wa asilimia 7.67 ikilinganishwa na makusanyo ya mwaka 2015/16 ambayo yalikuwa ni kiasi cha Shilingi Trilioni 13.3.

Sambamba na Makusanyo, Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipa kodi TRA Bw. Richard Kayombo alisema Mamlaka imeendelea kukusanya kodi mbalimbali ikiwemo kodi ya majengo na muitikio wake umekuwa ni wa kiwango cha kuridhisha.

Mamlaka hiyo inapenda kuwashukuru walipa kodi wote kwa muitikio huo na wengine wanaoendelea kujitokeza katika ofisi mbalimbali za Mamlaka nchi nzima ili kuweza kulipa kodi hiyo ambayo mwisho wa kulipa kodi hiyo ni tarehe 15 Julai, 2017.

Aidha, Mamlaka inatoa wito kwa wafanyabiashara wote kutoa risiti za EFD pindi wanapouza bidhaa au huduma na Wananchi wote kuhakikisha wanadai risiti pindi wanaponunua bidhaa au kupata huduma na kuwa, kinyume na hapo watakuwa wanatenda kosa kwa mujibu wa sheria ya usimamizi wa kodi.

Hivi sasa kuna zoezi la uhamasishaji na ukaguzi linaloendelea nchi nzima katika sehemu zote za biashara kukagua wafanyabiashara wasiotumia Mashine za Risiti za Kielektroniki za EFDs pamoja na wananchi wote wasiodai risiti baada ya kununua bidhaa au huduma.

“Napenda kuwakumbusha wananchi wote kuhakiki risiti zao ili kuona usahihi wa tarehe na kiasi walicholipa kabla ya kuondoka na risiti hiyo,” alisisitiza Kayombo.

Na Emmy Mwaipopo

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents