Burudani

Hizi njia 5 wasanii wa Bongo wanaweza kuuza albamu zao kwa faida

Kwa sasa muziki wa Bongo Flava umefanikiwa kuvuka mipaka ya kimataifa kwa kiwango kikubwa. Jambo la kusikitisha ni kuwa kukua kwa muziki wetu kumeshindwa kuimarisha soko la mauzo ya album za wasanii wetu.

Prof Jay - Machozi Jasho Na Damu

Kila msanii amekuwa akilalamikia ukiritimba uliokithiri katika usambazaji wa albamu zao suala linalopelekea wasanii wengi kutotoa albamu. Kiuhalisia ni kuwa albamu siku zote ni kipimo cha ubora wa msanii yeyote yule duniani.

Vuta pumzi kisha zirudishe nyuma kumbukumbu zako,HOMA YA DUNIA, ya Solo Thang, A.K.A MIMI ya Albert Mangwear, MACHOZI, JASHO NA DAMU ya Joseph Haule (MB).

Hizi ni baadhi ya albamu bora za muda wote kuwahi kutokea katika kiwanda cha Bongo Flava. Kwa kuutambua umuhimu wa albamu katika career ya msanii yeyote yule duniani.

Zifuatazo ni mbinu nilizozigundua mimi ambazo naamini endapo wasanii wetu watazitumia wataweza kutoa albamu zao huku wakiogelea kwenye tope la ukwasi mkubwa.

1. MITANDAO YA SIMU ZA MKONONI

Ukuaji wa kiwanda cha muziki wa bongo fleva ni dhamana tosha kwa wasanii kuitumia katika kuingia mikataba na makampuni hayo yenye mawakala kila pembe za nchi yetu.

Kupitia usambazaji wa kazi za wasanii,makampuni hayo pia yatakuwa yametanua wigo wa kujitangaza zaidi.Makampuni ya simu za mkononi yanaweza kuwatumia mawakala wao walio katika kila pembe ya Tanzania kusambaza albamu na kazi zingine za wasanii wetu. Utaacha vipi kununua albamu ya Afande Sele inayopatikana kwenye kibanda cha mpesa/tigopesa cha mango hapo kijijini kwenu Iselamagazi? Ni jambo linalowezekana kwani wasanii wetu wamekuwa wakitumiwa kufanya promosheni na kampuni hizo kila uchao.

2.MATUMIZI SAHIHI YA UKUAJI WA SAYANSI NA TEKNOLOJIA

Ukuaji wa sayansi ni moja kati ya mambo yakujivunia kwa wasanii wetu kwani umewaweka karibu sana na mashabiki zao, faukwa na hayo wasanii wetu wanapaswa kuitumia vyema teknolojia kuuza kazi zao za sanaa online.Wasanii wetu wanaweza kuuza albamu zao kwa kuwa na apps maalumu ya albamu husika ya msanii.

Alikiba ana followers laki saba na ushee kwa sasa kwenye page yake ya Instagram,endapo leo hii Alikiba akitoa apps ya albamu yake na ikawa inauzwa kwa tsh 5000,na ikitokea followers wake laki tatu na nusu wakainunua app hiyo, Kiba ataweza kujiingizia 1,750,000,000 na hao ni followers wake wa Instagram pekee.

Endapo followers laki saba na nusu wa Diamond Platnumz wakinunua app ya albamu yake kwa shilingi 5,000,atajiingizia kiasi cha shilingi 3,750,000,000.

Hapa ni kwa mauzo ya apps tu,na nimeangalia upande mmoja wa mashabiki walio Instagram tu,vipi mashabiki walio kwenye other social media na nyanja zingine za sayansi na teknolojia. Hatujaziangalia lakini ukweli ulio wazi ni kuwa wasanii wetu wana acha mabilioni yawapite mikononi mwao kwa uoga wao tu!!

3. MAWAKALA BINAFSI

Tanzania ina jumla ya mikoa 30,na wilaya zipatazo 169. Leo kama Vanessa Mdee,Jux,Fid Q, ROMA ama Q Chillah akiamua kusambaza albamu yake kwa kutumia mawakala wake binafsi kumi kila wilaya atakuwa na mawakala 1690 na endapo kila wakala akiuza copy mia za albamu watakuwa wameuza albamu 169,000 na ikiwa kila copy ya album inauzwa Tsh 5000,msanii atajiingizia tsh 845,000,000.

Kupitia mawakala hao wasanii wetu wataweza kujiongezea vipato na pia kutoa ajira kwa vijana wenzao wa kitanzania!!

4.KUTUMIA KAMPUNI ZA MAGAZETI

Kama yalivyo makampuni ya simu za mkononi hata kampuni za magazeti nazo zina mawakala kila kona ya Tanzania,hivyo basi wasanii wetu wanaweza kuingia ubia na kampuni hizo kuwasambazia kazi zao ili kuepuka ukiritimba.Wapo mashabiki lukuki wa Lady Jaydee, Weusi ama Jay Moe ambao kila siku wanawahi kwenye vibanda vya magazeti kujipatia habari zao, unadhani watashindwa kununua albamu zao watakapoikuta kwenye kibanda cha magazeti? Ni suala zuri na jema ambalo litaweza kuwasaidia wasanii wetu.

5.MUSIC/ALBUM TOUR

Katika mikoa 30 ya Tanzania endapo msanii akifanya show 3 kila mkoa kusambaza kazi zake atakuwa amefanya show 90. Katika kila show moja endapo akiuza copy mia tano kwa bei ya tsh 5000 ataweza kujipatia tsh 225,000,000. Wasanii wetu mnapoteza mabilioni lukuki kwa hofu ya kutegemea wadosi kusambaza kazi zenu lakini njia hii inaweza kuwafanya mabilionea kupitia jasho la kazi zenu.

Hizo ni baadhi ya mbinu ambazo zinaweza kutumiwa na wasanii wetu kuuza album zao ili waweze kujiongezea vipato na huku wakiacha Legacy katika career zao.

Makala imeandikwa Richards Limihagati (Instagram @ric_the_only) Mwanafunzi wa mwaka wa kwanza wa UDSM anayesoma LLB

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents