Habari

Je, hapa tutampata Rais ajaye?

Imeandikwa na Shabiru Chagulani (St Augustine University)

Imezoeleka kila unapokaribia muda wa uchaguzi kusikia watu wakitangaza nia ya kugombea urais hapa kwetu Tanzania.Nina imani sio kila mtu anaweza kuwa Rais, nafasi hii inahitaji mtu mwenye akili timamu ,busara, hekima,uwezo mzuri wa kufkiri na kufanya maamuzi pia.

URAIS

Katika maisha ya binadamu ndoto nazo ni sehemu ya maisha yake. Toka pale anapoanza kujitambua,binadamu huyu huwa na ndoto pale anapofikiri kuwa pindi atakapo kuwa mkubwa angependa kuwa mtu Fulani.Hivyo ndoto hiyo inaweza kufikiwa au isifikiwe kwa sababu mbalimbali.

Hapa nchini imeshuhudiwa viongozi mbalimbali wakiwemo wabunge na mawaziri wakionesha nia ya kutaka kugombea nafasi ya urais hapo mwakani 2015. Hawa wanaotangaza nia miongoni mwao ni wazee ,wenye umri wa kati na vijana pia.Ni jambo jema kama wanachokisema ni ndoto zao toka wakiwa watoto lakini hiyo haitoshi kwani urais ni zaidi ya ndoto kwa maana ya kuwa zipo sifa za mtu kuwa rais kama nilivyozitaja hapo juu katika utangulizi.

Kwa bahati nzuri viongozi hawa, wengi wao tumeona utendaji wao katika nafasi mbalimbali yaani uwaziri na ubunge,hivyo inaweza kuwa rahisi kwa mwananchi wa kawaida kujua na kuelewa mchango au mapungufu ya kiongozi huyo. Wapo wanafalsafa kama Hayati Mwalimu J.K.Nyerere waliwahi kuzungumzia nafasi ya urais ambapo aliwahi kusema: Kwa mtu makini urais ni mtihani.” Kauli hii inaweza kuonekana kuwa na maneno machache lakini maana yake ni kubwa hasa katika kipindi hiki ambacho kila mtu anaona sasa ni wakati sahihi kutangaza nia ya kugombea urais ifikapo 2015.

Waliotangaza nia ya kutaka kugombea nafasi ya urais hapo mwakani ni aliyewahi kuwa waziri mkuu, Edward Lowassa, waziri wa mambo ya nje na ushirikiano wa kimataifa Bernard Membe na Januari Makamba ambaye ni naibu waziri wa Mawasiliano Sayansi na Teknolojia pia ni mtoto aliyewahi kuwa katibu wa chama cha mapinduzi na mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Mzee Yusuf Makamba.

Harakati za kuutaka urais zimekuwa zikishuhudiwa wazi hasa Lowassa kupitia uchangiaji wa harambee makanisani na misikitini kwa kutoa kiasi kikubwa cha pesa pale ambapo amekuwa akikaribishwa. Pia Lowassa anakumbukwa kwa kuhusishwa na tuhuma za Richmond zilizopelekea yeye kujiuzulu.

Bernard Membe yeye anataka kuwa rais endapo akioteshwa. Na mwisho ni Makamba ambaye anajitambulisha kama kijana anayeona sasa umefika wakati wa kizazi cha wazee kuwaachia nafasi vijana wenye fikra mpya kugombea urais. Maneno haya aliyasema alipohojiwa kwenye kipindi cha Dira ya Dunia cha BBC Swahili.

Moja kati ya agenda zake ni ajira kwa vijana na kukuza uchumi. Hizi zinaweza kuwa ajenda nzuri kwa sasa hasa kwa vijana wengi waliomaliza vyuo vikuu lakini hawana ajira. Cha kujiuliza huyu ni kiongozi kutoka chama cha mapinduzi na tumeshuhudia mengi kutoka CCM baada ya Nyerere kustaafu. Chama kilipoteza mwelekeo na mwalimu pia aliwahi kukaririwa akisema ‘kama ningeona mbadala wa CCM ningeshauri wachukue dora’. Haya ni matokeo ya udhaifu wa chama hicho kuliua azimio la Arusha na mengi yakaanza kujitokeza ambayo ni pamoja na rushwa kushamiri ,matumizi mabaya ya ofisi za umma nk.

Hii inaweza kudhihirishwa na awamu ya nne ambayo mengi yameshuhudiwa kupitia serikali ya awamu ya nne mfano matumizi mabaya ya rasilimali kama madini. Tumeona wawekezaji ndio wamekuwa wakifaidika na rasilimali kwa kiasi kikubwa kuliko wazawa,rushwa kukithiri hasa mahakamani na polisi na rushwa sasa inaonekana kuwa sehemu ya utamaduni.

Tumeshuhudia pia ufisadi katika wizara mbalimbali mfano Tamisemi,wizara ya nishati na madini na wizara ya maliasili na utalii pia. Mwisho kabisa uvunjaji wa haki za binadamu wa watu kutekwa, kuuwawa na wengine kupoteza viungo vyao. Kwa udhaifu kama huu kupitia serikali ya awamu ya nne hawa wagommbea watawaeleza nini watanzania ambao ni wahanga wa mfumo mbovu kwa maana hakuna hatua zozote zinazochukuliwa na serikali kukomesha hali hii. Hawa wagombea nao ni sehemu ya mfumo huu na wengine ni vijana waliolelewa katika chama tawala.

Inaweza kuonekana ni rahisi kugombea urais lakini kwa hali kama hii ndugu Januari, Membe, Lowassa na wengine watawezaje kujenga uchumi wa taifa hili kwa jamii yenye matabaka kati ya walionacho na wasiokuwa nacho? Mbali na hiyo nini itakuwa hatima ya CCM hasa ukizingatia kila mtu anataka kuwa rais kwa hao waliotangaza nia?

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents