Siasa

JK: Sina mpango kuvunja Baraza

RAIS Jakaya Kikwete amesema hana mpango wa kuvunja wala kubadili Baraza lake la mawaziri katika siku za karibuni. Aliyasema hayo juzi Ikulu, Dar es Salaam, alipozungumza na waandishi wa habari, kutathmini miaka miwili tangu Serikali yake ilipoingia madarakani, Desemba mwaka juzi.

Na John Mapinduzi


RAIS Jakaya Kikwete amesema hana mpango wa kuvunja wala kubadili Baraza lake la mawaziri katika siku za karibuni. Aliyasema hayo juzi Ikulu, Dar es Salaam, alipozungumza na waandishi wa habari, kutathmini miaka miwili tangu Serikali yake ilipoingia madarakani, Desemba mwaka juzi.


Akijibu swali kuhusu tetesi za kufanyika mabadiliko makubwa ya Baraza la Mawaziri karibuni, Rais Kikwete alisema taarifa hizo hazina ukweli na huenda zinatokana na mawazo ya watu binafsi wanaotaka kufanyika kwa jambo hilo.


“Ni uvumi kama tutakuwa na haja tutabadili au ni matakwa ya watu,” alisema.


Akizungumzia ukubwa wa Baraza hilo ambalo baadhi ya wananchi wanadai linafanya kazi chini ya matarajio ya wengi, Rais Kikwete, alisema liliundwa kutokana na mahitaji na kama ni kufanyiwa marekebisho, suala hilo ni la baadaye na si sasa. “Tuliliunda kulingana na mahitaji, tutaona mbeleni tufanye marekebisho,” alisema.


Ripoti ya REDET


Aliisifu ripoti iliyotolewa hivi karibuni na Taasisi ya Utafiti na Elimu ya Demokrasia (REDET) ambayo iliainisha masuala mbalimbali ya utendaji wa Serikali ya Awamu ya Nne na kubainisha kulegalega kwa utendaji wa Baraza la Mawaziri, huku likimwachia mzigo yeye.


Alisema ripoti hiyo ni nzuri, kwani imekusanya maoni ya wananchi mbalimbali na Serikali inayatumia kama kioo kujitazama na kuona wapi penye kasoro ili kufanya marekebisho.


“Ripoti ya REDET ni nzuri, imekusanya mawazo ya wananchi mbalimbali, watu walitoa mawazo yao barabarani, sokoni, n.k., sisi kama Serikali tunatumia kama kioo kujitazama kuona wapi kuna kasoro na kujirekebisha,” alisema


Rushwa kubwa


Akijibu swali kuhusu hatua zinazochukuliwa na Serikali kupambana na rushwa kubwa, Rais Kikwete alisema Serikali imepania kutokomeza tatizo hilo, lakini inakwamishwa na mikanganyiko iliyopo kwenye suala lenyewe.


Alisema mapambano dhidi ya rushwa kubwa yanahitaji mtandao mkubwa na pesa za kutosha kufuatilia na kubaini ukweli wa matatizo hayo, vinginevyo mambo hayo yataishia kuwashuku watuhumiwa bila kuwa na ukweli.


Kuhusu kashfa ya rushwa katika ununuzi wa rada, alisema uchunguzi wake unahitaji muda wa kutosha na jambo hilo linaendelea kushughulikiwa.


Ahadi ya maisha bora


Rais Kikwete alisema tofauti na mawazo ya baadhi ya watu kuwa ahadi hiyo imeshindwa kutekelezeka katika kipindi cha miaka miwili ya utawala wake, kilichofanyika ni kuweka misingi imara kwenye maeneo muhimu na kitakachofuata ni utekelezaji kuelekea mwaka 2010.


“Ahadi ni za miaka mitano, tumeweka misingi, sasa tunapoelekea mwaka 2010 tunaweka matofali. Kuna maeneo mengi yamefanyiwa kazi, huduma za afya, barabara, maji.


“Tutawaonesha Watanzania wapi tutafikia. Tunatayarisha Mpango wa Maendeleo ya Afya ya Msingi, kuanzisha zahanati zaidi na kuhakikisha huduma hiyo inapatikana chini ya umbali wa kilometa tano kwa wananchi na kuimarisha barabara za mikoa na wilaya kwa kiwango cha lami,” alisema.


Serikali kuhamia Dodoma


Akijibu swali lililohoji kasi ya Serikali yake kuhamia Dodoma katika kipindi cha miaka miwili, Rais Kikwete alisema jambo hilo lipo na ni sera inayoendelea kutekelezwa.


Kuhusu kupunguza msongamano katika Jiji la Dar es Salaam kwa kuanzisha miji mipya mbali na wa sasa, Rais Kikwete alisema Serikali yake imeona umuhimu wa jambo hilo na imechukua hatua mbalimbali ukiwamo mradi wa upimaji viwanja kwenye maeneo mbalimbali.


Hata hivyo, alisema pamoja na jitihada zilizofanywa na Serikali mkoani Dar es Salaam na miji mingine kugawa maeneo ya makazi katika maeneo mbalimbali, ilisahau kutenga maeneo ya ujenzi wa viwanda yanayoweza kusaidia ‘kusambaza miji’.


Reli ya Kati


Akizungumzia huduma duni kwa usafiri wa reli ya kati baada ya lililokuwa Shirika la Reli Tanzania (TRC) kukodishwa, Rais Kikwete aliwatetea wawekezaji hao na kusema kuwa ni mapema mno kufanyika marekebisho makubwa ndani ya shirika hilo, kwani ni kipindi kifupi tangu ukodishaji huo ufanyike.


“Tusiwasukumie lawama, hawawezi kufanya miujiza, tuwape muda ndio kwanza wameanza kwa mazingira ya sasa. Tunafuatilia kwa karibu utekelezaji chini ya programu ya menejimenti mpya.


Shirika la Ndege Tanzania


Akijibu swali kuhusu huduma duni zinazotolewa na Shirika la Ndege Tanzania (ATC) ambazo katika siku za karibuni, zilisababisha usumbufu mkubwa kwa mahujaji waliokuwa wakienda kuhudhuria Ibada ya Hija, Rais Kikwete alilitetea na kubainisha kwamba kwa sasa lina ndege moja tu, kilichotokea, lilikubali kuchukua dhamana ya kuwatafuatia usafiri mahujaji hao.


“Tunachofanya ni kuhakikisha tatizo walilopata wakati wa kwenda halitokei wakati wa kurudi. Awali tulianza na ndege tisa, tukabaki na ndege mbili. Sasa ndio tumeanza programu ya umiliki, tumeanza na mwanzo mzuri,” alisema.


Uuzaji nyumba, Mgogoro Z’bar


Akijibu swali lililotaka kujua hatua iliyofikiwa na Serikali katika kurudisha baadhi ya nyumba zilizouzwa kwa watumishi wake, Rais Kikwete alisema shughuli hiyo inakwenda vizuri na Serikali inaendelea kuainisha nyumba hizo.


Kuhusu hatua iliyofikiwa katika suala la muafaka kati ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Wananchi (CUF) Zanzibar, alisema suala hilo linaendelea vizuri na anaamini litamalizika salama.


Utendaji TANESCO


Akijibu swali kuhusu kusuasua kwa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na hoja ya kutaka libinafsishwe na kuruhusiwa wawekezaji wengine kwenye sekta hiyo, Rais Kikwete alisema:


“Fikra zetu zipo kwenye majibu mawili, kuwa na kampuni tatu tofauti, uzalishaji, usafirishaji na usambazaji. Ililetwa Net Group ili irekebishe mambo pale TANESCO. Kazi iliyopo ni kulijenga Shirika lenyewe… TANESCO ndiyo yenye ‘monopoly’ wazalishe.”


Mikataba ya madini


Kuhusu madini, alipoulizwa kwamba Serikali inaonekana kupuuza kauli na mwito wa wananchi kusitisha mikataba ya madini, Rais Kikwete, alisema baadhi ya watu wanaongea na kuonesha kana kwamba Serikali haijali maslahi ya nchi.


Alisema alipokuwa Afrika Kusini Machi mwaka huu, aliongelea suala la mikataba ya madini na lilizua maneno mengi.


“ Huku nchini tayari nilikuwa nimeunda tume ya kupitia mikataba ili tuone jinsi gani inaweza kutunufaisha. Sisi hatuna mitaji, teknologia na rasilimali watu lakini tuna maliasili. Kama tunataka kufaidika na madini yetu ni lazima tuangalie namna ya kuyachimba tena kwa manufaa,”alisema.


Rais aliendelea kusema kwamba kwa hali iliyopo sasa, mikataba inamlinda zaidi mwekezaji. Hata hivyo alisisitiza kwamba si kosa la wawekezaji bali ni tatizo la mikataba yetu.


Alipotakiwa kueleza hatua ya wachimbaji wadogo wadogo kunyang’anywa ardhi na kupewa kampuni kubwa, Rais alisema kwamba shughuli ya uchimbaji madini inatawaliwa na sheria na si kama kilimo.
Alisisitiza kuwa mchimbaji anayesema eneo fulani ni lake athibitishe kisheria na asidhulumiwe.


“Pale tunapowakaribisha wawekezaji basi tuwe tayari kuwapa na ardhi ya kufanyia shughuli zao. Hatuwezi kumruhusu mwekezaji aje na tusimpe ardhi ya kufanyia kazi. Sasa atakapokuja tunategemea nini kama hatujampa ardhi?” alihoji.


Kwa wawekezaji wanaojenga mahoteli sehemu za ufukweni, Rais Kikwete, alisema kisheria hakuna mtu anayemilikishwa fukwe badala yake anapewa kiwanja kilicho karibu na fukwe.


“Hakuna ramani inayochorwa kufikia ufukweni kabisa, fukwe si mali ya mtu,” alisisitiza.


Source: Majira

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents