Siasa

Tutaifanyia kazi ripoti ya REDET – JK

Rais Jakaya Kikwete, ameikubali ripoti ya Taasisi ya Mpango wa Utafiti na Elimu ya Demokrasia Tanzania (REDET), iliyoonyesha wananchi kutoridhishwa na utendaji kazi wa Mawaziri.

Na Flora Wingia



Rais Jakaya Kikwete, ameikubali ripoti ya Taasisi ya Mpango wa Utafiti na Elimu ya Demokrasia Tanzania (REDET), iliyoonyesha wananchi kutoridhishwa na utendaji kazi wa Mawaziri.


“Ripoti ya REDET ni nzuri. Hiyo ni njia bora inayotumika dunia nzima,“ alisema Rais Kikwete, alipozungumza na waandishi wa habari, Ikulu jijini Dar es Salaam juzi.


Aliongeza, “kitu cha muhimu ni kuwa, ripoti imetoa fikra za watu kuhusu utendaji wa Serikali katika sekta mbalimbali. Nimeisoma. Ripoti hiyo itaisaidia Serikali.“


Mkutano wa Rais Kikwete na waandishi wa habari, ulitoa fursa kwa Rais kujibu maswali mbalimbali yaliyohusiana na utendaji wa Serikali na ahadi alizozitoa wakati akiingia madarakani, miaka miwili iliyopita.


Katika ripoti ya REDET, pamoja na mambo mengine, ilionyesha kuwapo asilimia kubwa ya wananchi wasioridhishwa na utendaji kazi wa Mawaziri, lakini wakaridhishwa na utendaji wa Rais Kikwete.


Aidha, Rais Kikwete, alisema; “ahadi zetu zilikuwa kwa kipindi cha ndani ya miaka mitano. Hatuwezi kukamilisha kila kitu kwa miaka miwili.


Ninaamini kwamba ifikapo mwaka 2010, msingi tulioujenga katika elimu, afya, maji, kilimo na kadhalika, yapo mambo yatakayowadhihirishia Watanzania kwamba tumetimiza ahadi zetu.“


“Hata hivyo, kuna mambo mawili ya msingi katika dhana ya maisha bora. Kwanza kupata huduma bora za kijamii na kiuchumi, elimu bora, huduma za afya, barabara, reli na usafiri wa anga. Maeneo haya yakiboreshwa, hali ya maisha itabadilika. Kitu kingine ni pato la mtu mmoja mmoja.“


Alisema Serikali yake imefanya mambo mengi katika maeneo hayo, ikiwamo suala la watoto wanaojiunga kupata elimu ya msingi ambapo limefikia asilimia 97 kutoka asilimia 95.


Katika afya, alisema lengo kubwa ni kuandaa mpango wa maendeleo ya afya ya msingi, na kwamba utakapokuwa tayari, utekelezaji utaanza mwaka ujao.


“Tunataka kuwa na zahanati kila baada ya umbali wa kilometa tano kutoka maeneo wanapoishi watu, vituo vya afya katika kila kata, kuimarisha hospitali za wilaya na mikoa � Katika miaka hii miwili, tumeshajenga kilometa 1174 za barabara za lami.“


Kuhusu barabara, Rais Kikwete, alisema msukumo wa Serikali katika miaka mitano hii ni kuunganisha mikoa isiyounganishwa na mingine kwa barabara za lami.


Alizitaja barabara hizo zitakazojengwa kwa msaada kutoka Millenium Challenge Corporation (MCC) ya Marekani, Japan na Benki ya Maendeleo Afrika ni inayounganisha mkoa wa Rukwa na Tunduma, Ruvuma na Mtwara.


Nyingine ni sehemu ya kuanzia Masasi kwenda Mangaka, Mangaka kwenda Tunduru, Tunduru, Songea hadi Mbamba Bay na Tanga hadi Horohoro, itakayopandishwa kuwa kiwango cha lami.


“Bado tunakamilisha barabara ya kutoka Manyoni hadi Kigoma, inayofadhiliwa na Mfuko wa Abu Dhabi Fund na Korea Kusini. Bado tunaendelea kuzungumza na Mfuko wa Kuwait.


Tutakapokamilisha mazungumzo nao, tutaweza kupata fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara hizo.


“Tunatafuta pia fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya Geita hadi Usagara,“ aliongeza.


Kuhusu reli, alisema ipo haja ya kuipa muda kampuni ya India iliyowekeza katika Reli ya Kati, na kuwa Serikali inaifuatilia kwa karibu.


Source: Nipashe

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents