Tragedy

Joni Woka: Rapper aliyerap kama mlevi lakini aliyekuwa hatumii kilevi chochote (Makala)

Miaka ya nyuma wakati muziki wa Bongo Flava umestawi zaidi na kuanza kukubalika kiasi cha kuanza kutawala playlist za redio za FM, ambapo kipindi hicho zilikuwa chache, uliibuka uiambaji wa lafudhi mbalimbali za makabila ya Tanzania.

Ni katika kipindi hicho, makundi kama Wagosi wa Kaya na Mr Ebbo walipata umaarufu mkubwa. Katika aina hiyo ya muziki pia, walitokea vijana wawili, Ras Lion aliyekuwa akirap kwa lafudhi ya Kijaluo na wakati mwingine kisukuma na pia Joni Woka aliyekuwa akirap kama mtu aliyeelewa chakali.

Kwa pamoja walikuwa wakiunda kundi liitwalo Watukutu. Nyimbo zao pamoja na kupendwa, zilikuwa na sifa ya uchekeshaji mwingi licha ya kuwasilisha ujumbe wa msingi.

https://www.youtube.com/watch?v=we2fmclIPeI

Kwa mfano kwenye wimbo wao ‘Umaskini Huu’, waliwasilisha ujumbe wa namna walivyokuwa wakiishi katika maisha ya dhiki, lakini wakiacha mbavu za watu zikiwauma kwa vituko walivyoviimba.

Kwa vyovyote vile ukimtaja Joni Woka, ulikuwa huachi kumtaja Ras Lion. Pengine kinachoshangaza zaidi na ambacho wengi wanaweza wakawa hawajui, ni kuwa pamoja na Woka kuimba kama mlevi, alikuwa si mnywaji kabisa wa pombe. Kwake hiyo ilikuwa ni sanaa tu.

“Woka ulikuwa ukimpa bia tatu chali kabisa,” amesema rafiki yake, John B.

Kifo cha Joni Woka

Kwa waliopata bahati ya kushuhudia hatua zote za kukua kwa muziki wa Bongo Flava na hatua zake kuanzia enzi za Saleh Jaber, zikaja enzi za Kwanza Unit, Diplomats, Wagumu Weusi, kisha Sugu, Profesa Jay na akina Lady Jaydee na rapper/waimbaji waliochipukia enzi zao hadi kizazi cha sasa cha akina Diamond na Alikiba, watakuwa walipata bahati ya kujua ni kwa kitu gani Joni Woka ameufanyia muziki huo.

https://www.youtube.com/watch?v=B-GXiHvxIQg

Kifo chake kimetokea ghafla na kwa kiasi kikubwa kimewagusa wasanii wengi. Michael Dennis Mhina kama ambavyo alikuwa akijulikana kwa jina lake halisi, alifariki February 16 baada ya kuwa amelazwa kwenye hospitali ya rufaa ya Muhimbili jijini Dar es Salaam.

https://www.youtube.com/watch?v=PxKi3VnveiI

Mauti yalimfika baada ya kuchomwa na kitu chenye ncha kali kilichochoka kufuatia mtungi wa gesi wa gari kulipuka walipokuwa wakitengeneza gari aina ya Volkswagen Polo kwenye gereji iliyopo Sinza.

Kitu hicho kilichomchoma kwenye paji lake la uso. Kwa mujibu wa madaktari chuma hicho kiliingia ndani zaidi kiasi cha kusababisha damu kumwagikia kwenye ubongo. Mungu alimpenda zaidi na hivyo alimchukua.

Alikuwa anafanya nini kabla ya mauti?

Pamoja na kwamba kimuziki alikuwa hasikiki sana licha ya kuendelea kurekodi kama kawaida, Joni Woka alikuwa amejiingiza kwenye shughuli za ujasiriamali zilizokuwa zikimuingizia kipato cha kutosha kuihudumia familia yake changa. Inauma zaidi kwakuwa amepoteza maisha, miezi sita tu baada ya kufunga ndoa.

20160218030144

Rafiki yake wa siku nyingi, John Blass ameiambia Bongo5 kuwa Joni alikuwa amefungua biashara zake Moshi na Dar es Salaam. Pia amesema alikuwa akifanya kazi Mererani.

Pamoja na muziki yeye na Ras Lion walikuwa wameanza kurekodi series za komedi ambazo pia walikuwa wamepanga kuzirusha kwenye TV.

“Katika vyote tulikuwa ndio tumemaliza kufanya dubbing ya DVD ya comedy series tulikuwa tumefanya huku Arusha,” amesema John B. “Na baada ya kilichomleta Dar,kuna movie tulikuwa tuanze kushughulikia ambayo yeye ndio alikuwa main character.”

https://www.youtube.com/watch?v=IKoXCVyzbfk

Hakika kifo kimeikatili mipango yake mingi na pia kimempa mke wake ujane katika umri mdogo. Joni Woka anazikwa Alhamis hii kwao mkoani Tanga. Tutamkumbuka daima.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents