Habari

Lake Energies yazindua kampeni ya ‘Kumtua Mama Kuni Kichwani’

Makumi kwa maelfu ya akina mama na familia zao wa mikoa mitano ya Dodoma, Morogoro, Mwanza, Arusha na Geita, watanufaika na kampeni iliyozinduliwa jijini Dodoma na kampuni ya Lake Energies Group iliyopewa jina la ‘Tumtue Mama Kuni Kichwani’ kwa kuwagawia mitungi 13,500 ya gesi.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kampeni hiyo jijini Dodoma leo Septemba 1, 2023, Meneja Masoko na Mawasiliano wa Lake Energies Group, Matina Nkurlu, alisema kuwa uamuzi wao huo umelenga kuunga mkono jitihada za Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan za utunzaji mazingira kwa kupunguza kama si kutokomeza kabisa utumiaji wa nishati ya kuni na mkaa.

“Lake Energies tumeona ni vema kuunga mkono jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA), katika kampeni ya utunzaji mazingira kwa kupunguza kama si kutokomeza kabisa utumiaji wa nishati ya kuni na mkaa na tayari tumeshasambaza mitungi katika mikoa ya Arusha, Morogoro, Mwanza na Geita.

“Pia, kampeni hii inalenga kumwondolea mwanamke wa kitanzania adha ya kutumia muda mwingi kwenda kutafuta kuni au mkaa wa kupikia na hivyo kuepukana na hatari za huko maporini na badala yake kupata muda mwingi wa kutunza familia na ndoa zao,” alisema Nkurlu.

Akizungumza kwa niaba ya wabunge wenzake ambao majimbo yao yamehusishwa katika kampeni hiyo, Mwenyekiti wa Wabunge Mkoa wa Dodoma, Mheshimiwa Job Ndugai, aliishukuru Lake Energies kwa mpango wao huo, akiyataka na makampuni mengine kuiga mfano huo wa kumuunga mkono Rais Samia.

“Kwa niaba ya wabunge wenzangu wa Mkoa wa Dodoma, tunawashukuru sana Lake Energies kwa uamuzi wenu huu wa kuamua kugawa mitungi ya gesi kwa akina mama wa mkoa wetu kwa kushirikiana na serikali yetu.
“Kama ilivyo kwa mikoa mingine, akina mama wa Dodoma wamekuwa wakitumia muda mwingi kwenda kutafuta kuni za kupikia hali inayowachosha, lakini pia ikichangia kwa kiasi kikubwa uharibifu wa mazingira. Tunawashukuru sana,” alisema Ndugai ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Kongwa.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents