Bongo5 MakalaBurudani

Makala: Kwanini ni muhimu kwa wasanii wa Tanzania kuwa na maafisa habari wao

By Wynjones Kinye

Bila kuzungukazunguka niseme tu moja kwa moja kuwa ipo haja kubwa ya wasanii Tanzania kuajiri ma-afisa Habari (communication officers)… toeni ajira aisee kwa faida yenu wenyewe.

550791_483637455003610_580511176_n
Upo wakati wa kutumia lugha fulani kulingana na watu unaowakusudia katika ujumbe wako, communication officer mwenye vigezo atajua nini cha kufanya na kwa wakati gani (Photo by Gavin Gosbert)

Kila mtu anawasiliana ila si kila mtu anaweza kuwasiliana kiufasaha. Wazungu wanasema effective communication. Mawasiliano ni kitu sensitive sana katika dunia ya sasa. Umuhimu huu upo kwa kila anayewasiliana lakini kwa watu wengine umuhimu wa mawasiliano unazidi kutokana na kile wanachosema ama kuandika kuwa na uhusiano mkubwa na biashara zao.

Naupenda muziki, hivyo nijikite kwenye kuwasiliana katika mrengo huu hususani kwenye mawasiliano kati ya MSANII na HADHIRA. Hapa sizungumzii nyimbo mnazoimba ambazo pia kwa namna nyingine ni mawasiliano, ila nazungumzia maneno mnayosema na zaidi mnayoandika kwenye kurasa zenu mbalimbali za mitandao ya kijamii.

Inanichefua sana nikutanapo na maandishi yenye makosa ya kila aina ya msanii mwenye heshima zake, kachanganya herufi, kaandika broken English, kakosea spelling na mengine mengi kwenye kurasa zao ama kurasa za watu anaohusiana nao.

Utakuta msanii ana blog na anaimanage mwenyewe kwa kuandika habari zake, kuweka picha na hata kuweka ratiba ya shughuli zake. Ni kitu kizuri kufanya hivyo lakini kama nilivyosema mwanzo kabisa, si kila mtu anaweza kuwasiliana kiufasaha, kile unachokiandika kina nafasi kubwa sana ya kukutengeneza wewe kibiashara, masihara ambayo hukuyakusudia katika kuandika yanakupotezea mengi sana.

Ukiacha blog na website ambavyo bado ni vitu vikubwa kidogo kwa wasanii wetu walio wengi, kuna mitandao maarufu ya kijamii i.e Facebook, Twitter, Instagram na mingine teeeele ambapo moja kwa moja msanii hutengeneza habari, ama kupalilia biashara yake kwa kile anachokiandika.

Ngoja niseme nawe msanii. Sina tatizo na wewe kutengeneza Habari ama kupromote muziki wako au hata kuonyesha maisha yako ya kila siku. Tatizo langu na wewe ni namna unavyojiharibia kwa kuandika vibaya jambo ambalo lingeandikwa vizuri lingekuwa jema sana kwako.

Hivi unajua unakuwa kituko kwa watu? Wapo wanaokuchora na wapo wanaokuchana live kuwa unazingua aidha kwa kuandika kingereza/kiswahili kibovu ama kuwa na mtiririko mbovu tu katika yale unayoyaandika hivyo kutofanikisha mawasiliano.

Nazijua kurasa za wasanii wachache zisizoandikwa na wasanii husika and yeah mambo si haba kwani hata response ya watu katika kile kinachoandikwa huwa ni kubwa sana, zaidi ni namna wanavyowekwa juu kiheshima japo kile kilichoandikwa hakikuandikwa na wao bali tu kusemwa na wao, kitu ambacho si kibaya hata kidogo na hakikushushii heshima kwamba wewe ndio umesema lakini afisa ndio amekiandika.

Ni rahisi sana mimi kukuelewesha wewe, nichukulie mfano ambao unakugusa moja kwa moja wewe, maneno unayoyatumia kwenye nyimbo zako ni yale yale tusio wasanii tunayatumia, lakini wewe unayaweka katika vina, mizani, na kisha kutengeneza sauti kisha kuyaimba kwa sauti nzuri. Vivyo hivyo katika hili ninalolizungumzia leo, wapo watu maalum wa kuandika kiufasaha kile unachokizungumza kawaida.

Upo wakati wa kutumia lugha fulani kulingana na watu unaowakusudia katika ujumbe wako, communication officer mwenye vigezo atajua nini cha kufanya na kwa wakati gani, nasema vigezo ni muhimu sana, itashangaza ukiajiri mtu ambaye mwisho wa siku wewe ni bora zaidi yake mara kumi na tatu.

Kuajiri mtu wa nafasi hii hakumaanishi moja kwa moja kuwa wewe huwezi kuandika ama vipi, wewe kama msanii upo wakati ratiba yako imebana kwelikweli na unahitaji kuandika kitu ama unatakiwa kujibu tuhuma fulani kwa haraka, kwa mazingira hayo sitashangaa kusikia umemtukana mtu ama kumjibu vibaya kwasababu uko under pressure.

Yupo msanii mmoja rafiki yangu siku moja aliexperience nilichoandika hapo juu. Kwenye mitandao kuna habari zinasambazwa na kwa kiasi kikubwa habari zilikuwa zinahatarisha career yake. Nilipenda alivyorespond katika lile swala na moyoni nilimsifu kwa hekima zake, ila siku tunaongea akatoa mfano wa tukio lile na kusema kuwa alikuwa amekasirika sana kiasi kwamba alikuwa tayari kumfumukia mtu hivyo alimuomba msimamizi wake kuihandle issue na mambo yakaenda vizuri.

Usijiweke katika mazingira ya kujiharibia, hivi we unadhani zile msg tweets za Jay Z anaandika zote yeye? Au Obama? Au Kikwete? Unaweza useme wewe sio wa level zao lakini nikuambie kabisa yeye na wewe mko katika tasnia moja hivyo lazma wote muwe na namna moja ya kudeal na public.

Haya kwa kusema haya nadhani mtatangaza ajira! Watu wa soccer Tanzania walishafanya haya, tena wao ilikuwa ni lazima kila club iajiri afisa Habari. Fanyeni hivyo basi, kwa kuanzia chukua hata mmoja wa rafiki ama ndugu zako wa karibu mwenye kufahamu haya mambo.

Unaweza kumfollow Kinye kwenye Twitter kwa @Kinye42

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents