Bongo5 Makala

Makala: OG Original ya G-Nako ni mfano halisi wa Hip Hop yenye ‘UTanzania’

Mawingu na manyunyu ya hapa na pale yalifanya nisipoteze muda mwingi Mlimani City nilipoenda Alhamis hii kwa shida binafsi kuogopa kuharibiwa siku yangu kwa kunyeshewa na mvua. Mbaya zaidi nilikuwa sijabeba mwamvuli.

Wakati nasubiri gari la kunisogeza mahala pangu pakazi, mara nasikia honi ikipiga nyuma yangu. Ilisimama gari ndogo na kioo cha mbele kikishuka. “Sky vipi bro!” ilisikika kutoka kwa dereva na mtu pekee aliyekuwa kwenye gari hilo. Alikuwa ni rapper, G-Nako aliyekuwa akitokea maskani akielekea kwenye ofisi za ITV.

Nilipanda gari lake ili anisogeze kidogo kule ninakoelekea na pia nilitaka nipate fursa ya kumpongeza kwa kazi yake mpya iitwayo OG Original. “Kaka kwanza hongera sana kwa kazi yako ya OG, tena naomba uiweke kwa sauti ya juu zaidi ili niweze kuisikia kwa uzuri zaidi,” nilimwambia G-Nako ambaye muda huo alikuwa akisikiliza muziki wa msanii wa Marekani.

Hakusita, alichukua CD ya wimbo huo na kuiweka. Wimbo unaanza kwa sauti kavu za G-Nako ‘Imma keep it real, Imma keep it OG.’ Sauti hizo zinapokelewa na trumpet zinazopigwa kwa ufundi na producer ambaye hachelewi kujitambulisha kwa sauti yake inayosikika kwenye kazi zake nyingi, ‘Nahreel on the beat.’

“Kaka lakini baadhi ya watu wanasema hawauelewi huu wimbo,” alisema G aliyekuwa busy kwenye usukani wa gari lake. Nilicheka kidogo baada ya kusikia kauli yake. “Kama kuna mtu anasema hauelewi huu wimbo basi hajui kabisa muziki,” nilimuambia. “Ukitaka kujua kuwa huu ni wimbo mkali, uchezwe kwenye sound kubwa,” niliongeza.

Nilimweleza kuwa OG ni wimbo tofauti, mkali na wenye ladha ya pekee ambao asiruhusu kabisa maneno ya watu wachache wasiojua muziki wanaodai kuwa haueleweki. “Nitakomaa mpaka waelewe lakini,” alisema G. “That’s the spirit,” nilidokeza.

Original ni wimbo ambao unajibu ile hamu ya Tanzania kufanya hip hop yenye ladha yake tofauti kabisa na ile ya Marekani. Huu ni wimbo ambao hata Kanye West akiusikia atatamani kuweka verse yake sababu si sound aliyozoea kuisikia.

Sababu kuna faida gani ya kutaka kwenda international kama tutataka kufanya muziki unaofanana na ule anaofanya Tyga au Lil Wayne?
Ukitaka kujua kuwa wimbo huu ni tofauti, sikiliza sauti za verse ya pili anasema, ‘atakuazimia chumvi akutangaze kitaa kizima, akikuazima mboga si kitanuka hii Dar nzima.’ Hizi ni sauti unazoweza kuzisikia kwenye nyimbo za mdundiko au muziki wa pwani na eenye asili ya Tanzania ambazo Warawara ameziweka kwenye mdundo huu wa kisasa.

Hata hivyo hiki si kitu kigeni kwa Weusi kwakuwa wanafahamika kwa namna ambavyo wamekuwa wakifanya muziki tofauti. Ukisikiliza Nusu Nusu na Don’t Bother za Joh Makini na Baba Swalehe ya Nick wa Pili utagundua jinsi wanavyobadilika. Huu ni wakati ambao wasanii wanatakiwa kukuna vichwa zaidi na kufanya muziki tofauti. Wasiogope kuthubutu na kutoa nyimbo zilizo nje ya ‘comfort zone’ yao ili kuepuka kuzoeleka.

Mfano wimbo ‘Asanteni Kwa Kuja’ wa Mwana FA ulivyo na mahadhi kama ya dancehall lakini rapper huyo akaidandia kwa style inayovutia au Nay wa Mitego alivyoamua kufanya mchiriku kwenye ‘Nyumbani Kwetu.’
Wasanii wasiendelee kufanya muziki kwa mazoea au kwa kuangalia muziki wa Nigeria unavyotrend.

Tunaweza kutumia muziki wa asili ya Tanzania na kuuboresha kwa utayarishaji wa kisasa na kuzipa video kali. Kwakuwa sasa tumeanza kupata nafasi kwenye TV za kimataifa, ni vyema tukaipa Afrika muziki mzuri na wa tofauti.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents