Habari

Mauaji ya watafiti: Washtakiwa 13 wafikishwa mahakamani

Mwenyekiti wa kijiji cha Iringa Mvumi wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma, Albert Chimanga na watu wengine 12 wamefikishwa katika mahakama ya wilaya ya Dodoma mjini, wakikabiliwa na mashtaka ya mauaji ya waliokuwa watafiti wa Kituo cha Utafiti wa kilimo cha Serian (SARI) jijini Arusha.

washitakiwamauaji

Washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni pamoja na ndugu watatu wa Chimanga ambao ni Cecilia Chimanga, Julius Chimanga na David Chimanga.

Wengine ni Dorca Mbehu, Edna Nuno, Grace Msaulwa, Juma Madehe, Sosthness Mseche, Lazaro Kwanga, Yoram Samamba, Edward Lungwa na Simon Samamba.

Washtakiwa hao walifikishwa kwa hakimu mfawidhi wa mahakama ya wilaya ya Dodoma mjini, Joseph Fovo na kusomewa shitaka lao na Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Beatrice Nsana. Ilidaiwa kuwa Oktoba 1, mwaka huu, katika kijiji cha Iringa Mvumi wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma, washitakiwa waliwaua watu watatu wakiwemo watafiti wawili wa Kituo cha Utafiti cha Kilimo (SARI) jijini Arusha.

Washitakiwa hawakutakiwa kujibu lolote kutokana na mahakama hiyo kutokuwa na mamlaka ya kusikiliza kesi za mauaji, hivyo walipelekwa rumande hadi kesi hiyo itakapotajwa tena Oktoba 31, mwaka huu.

Waliouawa walitajwa kuwa ni Nicas Magazine alikuwa dereva wa watafiti wawili, Teddy Lumanga na Jafari Mafuru, waliokuwa kwenye gari lenye namba za usajili STJ 9570 aina ya Toyota Hilux Double Cabin. Oktoba Mosi mwaka huu watafiti hao waliuawa kisha miili yao kuchomwa moto baada ya kuhisiwa ni wanyonya damu.

BY: EMMY MWAIPOPO

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents