Morogoro gizani

Wilaya tatu za Mkoa wa Morogoro, ziko gizani kwa siku mbili sasa kufuatia transfoma inayosambaza nishati hiyo kwa wilaya hizo kupata hitilafu na kuteketea kabisa.

Na Amina Saidi, PST Morogoro



Wilaya tatu za Mkoa wa Morogoro, ziko gizani kwa siku mbili sasa kufuatia transfoma inayosambaza nishati hiyo kwa wilaya hizo kupata hitilafu na kuteketea kabisa.


Wilaya zilizoathiriwa na hali hiyo ni Morogoro, Kilosa na Mvomero.


Tatizo hilo lilitokea juzi usiku, lilisababishwa na radi ambapo pia iliunguza jenereta tegemezi ya hospitali ya Mkoa wa Morogoro.


Kaimu Meneja wa Shirika la Umeme Nchini (Tanesco) mkoani Morogoro, Bw. Mhandisi Theodory Bayona aliiambia PST jana kuwa, hitilafu hiyo ilisababishwa na radi iliyopiga kituo hicho juzi saa 1:30 usiku.


Bw. Bayona alisema kazi ya kuirejesha huduma hiyo katika hali ya kawaida ni ngumu na hawajui itakamilika lini.


Hata hivyo, alisema jitihada za kuhakikisha kwamba kazi hiyo inakalimika mapema iwezekanavyo, zinaendelea.


Alisema transfoma iliyoungua ni ya kilovoti 33 na kwamba kilichokwamisha kuanza mapema kwa matengenezo hayo ni kukosekana kwa vifaa ambavyo vimeagizwa Tanesco makao makuu ya jijini Dar es Salaam na mkoani Dodoma pamoja na baadhi ya mafundi kwa ajili ya kuifanya kazi hiyo.


Aidha, taarifa kutoka Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka iliyothibitishwa na wataalam wa maji waliotembelea eneo la tukio jana, zinasema asilimia 70 ya wakazi wa Manispaa ya Morogoro wanaotegemea chanzo cha maji cha bwawa la Mindu, hawatapata huduma ya maji hadi tatizo hilo la umeme litakapopatiwa ufumbuzi.


Mjumbe wa Bodi ya Maji MORWASA ambaye pia ni Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro, Bw. Godfrey Ngaleya aliyetembelea eneo la tukio, alisema hali hiyo inatokana na mashine za maji zilizopo katika chanzo hicho kushindwa kusukuma maji bila nguvu ya umeme.


Kwa sasa, wanaopata maji ni wakazi wanaoishi maeneo ya milimani ambao hawategemei chanzo hicho.


Katika hatua nyingine, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dk. Meshack Massi alisema hitilafu hiyo ya umeme, pia ilijeruhi watu saba na kuunguza jenereta ya akiba na tegemezi kwa katika hospitali kuu ya Mkoa wa Morogoro sambamba na kukosekana kwa huduma ya maji.


Alisema kutorejea haraka kwa huduma ya umeme, kutawathiri wagonjwa hasa walio katika Chumba cha Uangalizi Maalum (ICU) na upasuaji.


Alisema majeruhi sita kati yao, walipatiwa matibabu na kuruhusiwa jana lakini mmoja bado hali yake siyo nzuri na alichukuliwa na wazazi wake na kuhamishiwa jijini Dar es Salaam kwa matibabu zaidi.


Alisema kwa sasa wanategemea jenereta ndogo mbili ambazo hazina nguvu ya kuweza kufanya kazi kwa zaidi ya saa tatu mfululizo.


Kutokana na hali hiyo, ameiomba Tanesco kufanya jitihada za kuhakikisha huduma hiyo inarudi haraka.


Alisema tatizo hilo limekuja katika kipindi kibaya cha siku kuu za mwisho wa mwaka ambapo ajali na matukio mengi ya majereha hutokea.


Kwa sasa hospitali pekee inayoweza kupokea wagonjwa na kuwahudumia kikamilifu ni ya Mtakatifu Francis iliyopo Ifakara wilayani Kilombero.


Source: Nipashe

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents