Siasa

Serikali yabeza tishio la mgomo

SERIKALI imetupilia mbali shinikizo la Muungano wa vyama vya upinzani nchini la kumtaka Rais Jakaya Kikwete kuunda tume huru kwa ajili ya kuchunguza madai ya ufisadi wa baadhi ya viongozi la sivyo utaitishwa mgomo wa nchi nzima.

Maulid Ahmed


SERIKALI imetupilia mbali shinikizo la Muungano wa vyama vya upinzani nchini la kumtaka Rais Jakaya Kikwete kuunda tume huru kwa ajili ya kuchunguza madai ya ufisadi wa baadhi ya viongozi la sivyo utaitishwa mgomo wa nchi nzima.


Akizungumza na HabariLeo jana, Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, Muhammed Seif Khatib alisema kuwa rais hawezi kupewa shinikizo na upinzani wala kulazimishwa kufanya kitu kilicho ndani ya uwezo wake.


“Upinzani wao waendelee kuchukua hatua zao na serikali na rais wanaendelea na hatua zao …,”alisema juu ya shinikizo hilo.


Kauli ya serikali imekuja baada ya Muungano wa vyama vya siasa vya upinzani jana kutangaza kwamba unatoa mwezi mmoja kwa Rais Kikwete kuunda tume huru ya kuchunguza madai hayo ya ufisadi yaliyotolewa katika mkutano wa hadhara mwezi uliopita vinginevyo utashawishi wananchi nchi nzima kuandamana na kugoma hadi hapo ufumbuzi na ukweli juu ya tuhuma hizo utakapokuwa umepatikana.


Madai hayo ya ufisadi huo ni pamoja na mkataba wa uchimbaji dhahabu wa Buzwagi na madai mapya ya kuwapo kampuni hewa zinazodaiwa kuundwa na kupewa fedha na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ambapo zinadaiwa kutumika kufadhili uchaguzi mkuu uliopita.


Akizungumza kwa niaba ya Muungano huo wa vyama vya NCCR, Chadema, CUF na TLP, Mwenyekiti wake Augustino Mrema alisema kuwa Muungano huo unamtaka Rais Kikwete kuunda haraka tume vinginevyo ifikapo Novemba mwaka huu wataongoza maandamano na kuwashawishi nchi nzima kugoma.


Alisema bila kumtaja yeyote wala kuonyesha ushahidi, “Tunataka Tume iwe huru …tuhuma kama za BoT na mikataba ya madini haiwezi kuchunguzwa na serikali na vyombo vyake kwa sababu pesa nyingi za BoT zilipitia kwenye makampuni hewa ili kugharamia uchaguzi Mkuu wa 2005 kwa wagombea wote wa ngazi zote.”


Mrema alisema kambi ya upinzani bungeni ilitoa hoja na kuishauri serikali kuchukua hatua dhidi ya tuhuma za ufisadi lakini ilipuuzwa.


Mrema ambaye alisema kuna vithibitisho kuwa BoT ilitoa Sh bilioni 30 kwa ‘kigogo’ mmoja na kampuni hewa na kuidhinisha malipo ya zaidi ya bilioni 130 kwa watu wasiojulikana wanaodaiwa kuingiza fedha za kigeni nchini.


Source: Habari Leo

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents