Habari

Serikali yajiandaa kuondokana na migogoro ya ardhi

Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba, Maendelo ya Makazi, Angelina Mabula amesema serikali inaandaa programu ya kupanga, kupima na kumilikisha kila kipande cha ardhi nchini. Mpango huo utaondoa muingiliano wa watumiaji wa ardhi nchini pamoja na kupunguza mgogoro wa ardhi.

Naibu waziri huyo ametoa kauli hiyo leo, akiwa bungeni wakati akijibu swali lililoulizwa na mbunge Amina Mwakilaji lililohoji,

Serikali ina mpango gani wa kupima ardhi yote ya Tanzania ikiwa ni njia mojawapo kubwa ya kutatua migogoro ya ardhi?

“Ni azma ya serikali kuondoa migogoro ya ardhi kote nchini, na ili kufikia azma hiyo, serikali imeandaa programu ya kupanga, kupima na kumilikisha kila kipande cha ardhi nchini, katika utekelezaji wa Programme hii , kila kipande cha ardhi nchini kitapangiwa matumizi na kupimwa hali ambayo itaondoa muingiliano baina ya watumiaji mbalimbali wa ardhi na hivyo kupunguza uwezekano wa kuibuka migogoro ya ardhi. Mpango huu utasaidia ardhi yote kutunzwa kwa watumiaji husika na kuhifadhi maliasili zilizopo katika ardhi kwa ujumla pia jamii inayozunguka maeneo hayo yaliyohifadhiwa itawezeshwa kutambua mipaka yao na kuwa na mipango ya matumizi ya ardhi na kuzibiri uvamizi wa maeneo ya hifadhi,” amesema Naibu Mabula.

“Aidha utekelezaji wa programu hii utaiwezesha jamii kufahamu umuhimu wa kulinda ardhi inayomilikiwa dhidi ya uvamizi wowote kuwezesha kukabiliana na mabadiliko yanayotokana na tabia ya nchi kuboresha makazi ya wananchi na kuleta usalama na ustawi wa maliasili za Taifa.”

“Mheshimiwa Spika programu ya kupima na kumilikisha kila kipande cha ardhi nchini, itahusisha Halmashauri zote 181 nchini na imepanga kufanyika katika miaka 10 kwa awamu ya miaka mitano kwa kila awamu ya mwaka wa fedha 2016/2017. Aidha programu hii itakuwa na miradi mikubwa miwili ambayo ni miradi ya upimaji ya kila kipande cha ardhi vijijini na mradi wa upimaji kila kipande cha ardhi mijini,”ameongeza

Na Emmy Mwaipopo

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents