Uncategorized

Shahidi aeleza sababu zilizomfanya ashindwe kuomba msaada wakati anatoa milioni 90 kwa kina Sabaya

Shahidi wa 10 Francis Mrosso, katika kesi ya Uhujumu Uchumi inayomkabili aliyekuwa Mkuu wa Wilaya, Lengai Ole Sabata amedai kuwa alishindwa kuomba msaada wakati pesa zake zinachukuliwa kwenye gari kwa kuwa alikuwa anahofu ya kupotezwa kama alivyokuwa ametahadharishwa awali.

Mrosso amesema hayo baada ya kuulizwa ni kwanini wakati anamshusha kwenye gari kijana aliyetoka naye benki akiwa amebeba boksi la milioni 90 hakupiga kelele ili asaidiwe na raia.

Mrosso amesema kwamba kilichomtia hofu ni kwamba kijana huyo awali alitambulishwa kuwa anatoka kitengo cha usalama wa Taifa na wakati huo alikuwa akifuatiliwa na gari nyingine kwa nyuma hivyo hakuwa akiamini kama maisha yake yapo salama.

Katika hatua nyingine Shahidi huyo ameieleza mahakama kiasi cha Milioni 90 hakumkabidhi Sabaya bali kijana aliyekuwa amekabidhiwa na Sabaya kutokea ofisini kwake.

“Tukiwa tunatoka benki yule kijana aliniambia simamisha gari nikasimama. Akashuka kutoka siti ya nyuma alipokuwa amekaa akafungua mlango wa mbele na kuchukua boksi lililokuwa na milioni 90 na kuondoka nalo. Nilibaki nimepigwa na butwaa” Shahidi Mrosso.

Mbali na hayo Shahidi huyo amekiri kitendo cha yeye kutoa milioni 90 ili asifunguliwe kesi ya uhujumu uchumi kitafsiriwe kama alitoa rushwa kwa kulazimishwa na kwamba yeye si mtoa rushwa kwani kazi zake zote anafanya kwa uwazi usio na makandokando.

Katika hatua nyingine Mrosso ameweka wazi kuwa ingawa muda wote aliachwa na simu yake lakini alikuwa akiitumia kwa kupewa maelekezo kitendo ambacho kilimfanya ashindwe kumuambia hata mke wake jambo lililomfika.

Kutokana na muda Mahakama imeahirishwa mpaka kesho Nov 30 ambapo upande wa utetezi utaendelea kumhoji Shahidi.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents