Michezo

Sure Boy, Mbaraka Yusuph wavimbiana misuli tuzo za mwezi Azam FC

Wachezaji watatu wa Klabu Bingwa ya Afrika wamechaguliwa kuwania tuzo ya Mchezaji Bora wa timu hiyo (NMB Player Of The Month) mwezi Septemba.

Wachezaji walichaguliwa ni kipa namba moja wa Azam FC, Razak Abalora, kiungo Salum Abubakar ‘Sure Boy’ na mshambuliaji nyota Mbaraka Yusuph.

Tuzo hiyo iliyoanza kutolewa Agosti mwaka huu ikidhaminiwa na Mdhamini Mkuu wa Azam FC, Benki bora kabisa nchini ya NMB, ilishuhudiwa beki kisiki Yakubu Mohammed akiitwaa kwa mara ya kwanza.

Septemba mwaka huu, Azam FC ilicheza jumla ya mechi nne dhidi ya Simba, Kagera Sugar, Lipuli na Singida United na kufanikiwa kuvuna jumla ya pointi nane baada ya kushinda michezo miwili dhidi ya Kagera Sugar (1-0), Lipuli (1-0) na kutoa sare mbili ilipokutana na Simba (0-0) na Singida United (1-1).

Vigezo vya wachezaji hao

Razak Abalora – Kipa huyo ameingia kwenye kinyang’anyiro cha mwezi Septemba baada ya kuiongoza Azam FC kutopoteza mchezo wowote na akiruhuru wavu wake kuguswa mara moja tu ndani ya mechi nne sawa na dakika 360.

Huwezi kusifia ubora wake pekee bila kuwapa sifa mabeki walioshiriki kwenye mafanikio hayo, nahodha msaidizi Agrey Moris, Yakubu Mohammed, ambao wameunda safu nzuri ya kati wakishirikiana na Daniel Amoah na mabeki wengine wa pembeni Bruce Kangwa na Swaleh Abdallah.

Salum Abubakar – Kwa muda mrefu tokea timu hiyo ipande daraja, Sure Boy amekuwa ni nguzo muhimu kwenye eneo la kiungo wa ushambuliaji na hii ni kwa ubora wake mkubwa wa kuwapoteza viungo wa kati wa timu pinzani kutokana na staili yake ya umiliki wa mpira katika eneo hilo.

Mwezi Septemba alikuwa kwenye kiwango kizuri, akiwa ameongoza kwa upigaji pasi ndani ya eneo hilo kwa asilimia 55 kwenye kila mchezo na kuisaidia vilivyo safu ya ushambuliaji.

Mbaraka Yusuph – Akiwa ndio kwanza ameingia kwenye timu baada ya kusajiliwa msimu huu, tayari Mbaraka Yusuph, ameanza kutema cheche zake alizozianza msimu uliopita alipokuwa Kagera Sugar.

Mshambuliaji huyo amefanya makubwa sana mwezi Septemba, akiwa amefunga mabao mawili yaliyoiwezesha Azam FC kuzoa pointi sita huku akiwa ndiye mshambuliaji pekee anayeongoza kwa kutupia ndani ya timu hiyo msimu huu akiwa amefunga mara mbili.

Licha ya uchache wa mabao yake, kwa kiasi fulani kupungua kwa kasi yake kumetokana na kukosa sehemu kubwa ya maandalizi ya msimu (pre season) baada ya kufanyiwa upasuaji wa henia Juni mwaka huu na kuwa nje ya dimba kwa takribani miezi miwili akiuguza majeraha hayo.

Mbali na tuzo kwa timu kubwa, Azam FC pia inatoa tuzo kwa timu yake B (Azam B) inayojulikana kama Uhai Player Of The Month ikidhaminiwa na mdhamini namba mbili wa timu hiyo maji safi ya Uhai Drinking Water.

Aidha mwezi Agosti tuzo hiyo kwa upande wa Azam B, ilichukuliwa na kiungo wa timu hiyo Twaha Hashir Rajab.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents