Habari

Tisa mahakamani kwa tuhuma za kusafirisha dawa za kulevya aina ya Heroin, Methamphetamine Kilo 332

Tisa mahakamani kwa tuhuma za kusafirisha dawa za kulevya aina ya Heroin na Methamphetamine Kilo 332

Watuhumiwa tisa (9) wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashtaka ya kusafirisha dawa za kulevya aina ya heroin na methamphetamine zenye uzito wa kilogramu 332.

Akisoma mashtaka yao mbele ya mahakama hiyo, wakili wa serikali Batilda Mushi amewataja washtakiwa hao kuwa ni Ally Ally (28), Bilali Hafidhi (31), Mohamed Hamisi (47), Idrisa Mbona (33), Rashid Rashid (24), Shabenga Shabenga (24), Dunia Mkambilah (52), Mussa Hussein (35) na Hamis Omary (25).
Amesema, katika shtaka la kwanza, Aprili 16, 2024 karibu na hoteli ya White Sands wilayani Kinondoni jijini Dar es Salaam, washtakiwa walikutwa wakisafirisha dawa za kulevya aina ya Methamphetamine kiasi cha kilogramu 100.83.

Katika shtaka la pili wakili Mushi amedai mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Richard Kabate kuwa, tarehe hiyohiyo, karibu na eneo la hoteli hiyo ya White Sands wilayani Kinondoni jijini Dar es Salaam, washtakiwa walikutwa wakisafirisha dawa za kulevya aina ya Heroin hydrochloride kiasi cha kilogramu 232.69 kinyume na kifungu namba 15 (1|) (a) na(3) (i) cha sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Sura ya 95 kama ilivyorejewa mwaka 2019, ikisomwa pamoja na aya ya 23 jedwali la kwanza kifungu namba 57 (1|) na 60 (2) cha Sheria ya Udhibiti wa Makosa ya Uhujumu Uchumi na Uhalifu wa Kupangwa Sura ya 200 ya mwaka 2022.

Hata hivyo, washtakiwa wote hawakuruhusiwi kujibu chochote mahakamani hapo kwani mahakama hiyo haina mamlaka ya kisheria ya kusikiliza shauri hilo.

Aidha, upande wa mashtaka uliieleza mahakama hiyo kwamba upelelezi wa shauri bado unaendela na kuomba kupangiwa tarehe nyingine ya kutajwa ambapo Hakimu Kabate aliahirisha kesi hiyo hadi tarehe 6 Mei, 2024.

Washtakiwa wote wamerudishwa mahabusu kutokana na kesi inayowakabili kutokuwa na dhamana.

Watuhumiwa waliofikishwa Mahakamani ni kati ya watuhumiwa 21 waliotangazwa na kamishna jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za kulevya tarehe 22 April, alipozungumza na waandishi wa habari kufuatia ukamataji wa kilo 726.2 zilizokamatwa katika mikoa ya Dar es Salaam, Pwani na Tanga.

Written by Janeth Jovin

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents