Burudani

Video: Jokate aamsha shangwe baada ya kusema ‘nampenda Simba!’

Mwanamitindo na mfanyabishara Jokate Mwegelo akiambatana na msanii mkongwe wa muziki Inspector Horoun Jumanne hii ‘waliliamsha dude’ katika banda la Hifadhi ya Ngogogoro la msanii wa muziki wa asili, Mrisho Mpoto lililopo katika viwanja vya Maonyesho ya Sabasaba jijini Dar es salaam.

Jokate akiwa wa wamasai kutoka Ngorongoro

Awali ya yote Jokate ambaye alitajwa na jarida maarufu la Forbes Africa kuwa ni miongoni mwa vijana walio na umri chini ya miaka 30 wenye mafanikio katika sekta mbalimbali kwa mwaka 2017, alitua katika viwanja hivyo majira ya saa tisa jioni na kupokewa na shangwe za watu ambazo ziliambatana na maandamano ndani ya viwanja hivyo kama ishara ya upendo.

Akiongeza na waandishi wa habari muda mchache baada ya kufika kwenye banda hilo la Ngorongoro, Jokate alisema amefurahishwa na jinsi mashabiki walivyompokea kwa shangwe huku akidai hakutegea kupewa shangwe hiyo.

“Mapokezi yamekuwa makubwa sana na hii ni picha nzuri na ina maanisha Ngorongoro mpo juu sana, kijasho kimenitoka, nawashukuru sana haya ni mapenzi mazuri kwangu, na nawashukuru sana Ngorongoro pamoja na balozi wake Mrisho Mpoto,” alisema Jokate.

Katika hatua nyingine wakati akiuzungumzia ufahari wa Hifadhi ya Ngorongoro, mwanamitindo huyo alisema yeye anapenda kumuona mnyama simba atembeleapo mbugani kauli ambayo iliibua shangwe kutokana muimbaji Diamond Platnumz kutumia jina hilo kama aka yake huku yeye akionekana kuwa karibu zaidi ya muimbaji Alikiba ambaye ni Balozi wa Wild Aid Tanzania akionyesha kupinga mauaji wa Tembo.

“Mimi napenda muonekano wa Ngorongoro, nawapenda wanyama Simba, nampenda sana Simba,” alisema Jokate huku akicheka na watu wakimshangilia. “Lakini kikubwa zaidi napenda kuangalia ule muonekano wake ni wakuvutia sana. Unajua watu wengi wanafikiria ukitaka upate sehemu ya kupumzikia lazima utoke nje ya Tanzania lakini sio kweli Tanzania tu kila kitu ambacho kinaweza kukufanya ufurahi na ujisikie tofauti kabisa,”

Aliongeza, “Wito wangu kwa Watanzania ni kuwataka watembelee hifadhi zetu, watembelee maeneo yetu ya utalii, watembelee sehemu kama hifadhi ya Ngorongoro ni hifadhi nzuri na bei ni kama na bure kabisa kila mtu anaweza kutembelea. Kwahiyo sioni sababu ya mtu kushindwa kutenga hata siku moja katika siku 365 za mwaka mzima kutembelea Ngorongoro,”

Kwa upande wa Inspector Horoun amewataka watanzania kutembelea hifadhi za taifa ili kukuza uchumi wa nchi pamoja na kuunga mkono juhudi za Rais John Pombe Magufuli katika kutunza rasilimali za nchi.

“Kama ambavyo Jokate ameongea, tujenge tamaduni za kutembelea mbuga zetu pamoja na hifadhi za wanyama kwa sababu vijana tumekuwa tukidharau sana rasilimali zetu. Kwahiyo kwa pamoja wote tunamuunga mkono Rais Magufuli katika kusupport na kutetea rasilimali za nchi yetu,” alisema Inspector Horoun.

Mrisho Mpoto akiwa na bosi wa Ngorongoro

Naye balozi wa hifadhi ya Ngorongoro, Mrisho Mpoto amewataka wazazi kuwajenga watoto wao kwa kuwafundisha kutembelea hifadhi mbalimbali za taifa hali ambayo amedai itawajenga kuwa wazalendo.

“Mimi kama balozi mengi yamezungumzwa na wenzangu lakini wito wangu kwa wazazi tuwapeleke watoto wetu hifadhi ya Ngorongoro wakajifunze mambo mbalimbali. Hapa kwenye banda letu tumekuwa tukitoa elimu kwa watoto kuhusu Ngorongoro na wengi wao wanaonekana kuwa na shauku kubwa kutaka kwenda Ngorongoto. Kwahiyo mimi wito wangu tuwapeleke watoto ili tuanze kujenga kizazi ambacho kitasijikia ufahari na kujivunia vitu ambavyo wameviona kwa macho yao,” alisema Mpoto.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents