Habari

Vodacom, Polisi Kinondoni wazindua kampeni ya Usalama barabarani shuleni

Jeshi la Polisi Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni kwa kushirikiana na kampuni ya Vodacom Tanzania PLC wamezindua kampeni ya usalama barabarani shuleni.

Kampeni hiyo imezinduliwa leo kwenye shule ya Mwangaza, jijini Dar es Salaam ikilenga pia kutoa mafunzo kwa wanafunzi marafiki wa usalama barabarani ambao watawafundisha wengine na kuwaongoza kuvuka barabara katika maeneo yenye vibao vya usalama kwa wanafunzi

Kamishina wa Polisi Wilaya ya Kinondoni ACP, Ally Wendo, Mtaalamu wa afya na Usalama Kazini wa Vodacom Tanzania, Adamson Manya, wakimkabidhi vifaa vya usalama barabarani mwalimu wa taaluma wa shule ya msingi Kijitonyama Kisiwani, Peter Laizer (kulia) wakati wa uzinduzi wa kampeni kuhusu usalama wa jamii inayolenga shule zilizopo kandokando mwa barabara nchini, kulia ni Mkuu wa Usalama Barabarani SSP, Solomoni Mwangamilo.

Kampeni hiyo iliyoanzia kwenye shule ya Mwangaza na Kijitonyama itafanyika pia kwenye shule ya Salasala, Bunju A na Tandale shule ya msingi.

“Hii ni programu nzuri ambayo inakwenda kusaidia kupunguza ajali kwa wanafunzi wa hizi shule zilizo pembezoni mwa barabara,” alisema Mwalimu Makame Mpate wa shule ya Mwangaza na kuendelea.

“Ombi langu kwa Vodacom, programu hii ni nzuri kwa usalama wa wanafunzi, lakini pia wangefunga kamera za kutambua madereva watukutu katika hii kampeni,” alisema.

Mkuu wa kikosi cha Usalama Barabarani mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni, SSP Solomon Mwangamilo alisema wameshirikiana na Vodacom kutoa mafunzo kwa wanafunzi marafiki ambao kupitia hao watawafundisha wengine na kusaidia kuwavusha wenzao wakitumia vibao ambavyo vimetolewa na Vodacom katika kampeni hiyo.

Alisema shule nyingi ambazo ziko pembezoni ziko kwenye hatari kwa wanafunzi kugongwa wanapovuka barabara.

“Tumekuja na kampeni hii kuondoa hatari kwa watoto wetu, ili kuhakikisha ndoto zao zinatimia, tunaifanya kwenye shule tofauti za Kinondoni.

“Leo (jana) tumefanya uzinduzi na kuanzia kesho (leo), tunaendelea na mafunzo, vibao hivi maalumu kwa wanafunzi kuvukia kuanzia leo (jana) vitakuwa vikionekana huko mtaani.

“Hivi ni kama ambavyo dereva atafuata sheria za taa za barabani akikiona akitii kama ambavyo anatii kwenye taa, watakaokiuka na kubainika tutawachukulia hatua kama mtu aliekiuka taa za barabarani,” alisema Mwangamilo aliyekuwa ameambatana na ACP, Ally Wendo, Mkuu wa Ushirikishwaji wa Jamii mkoa wa Kipolisi Kinondoni.

ACP Wendo, aliyekuwa mgeni rasmi alisema Vodacom wamefanya jambo kubwa na jema kwa vijana hao ambao ni taifa la kesho na kubainisha kwamba kampeni inakwenda kupunguza hatari kwa wanafunzi wa shule hizo.

Meneja Afya na Usalama Kazini wa Vodacom, Adamson Manya aliyemwakilisha Mkurugenzi Mtendaji, Philip Besiimire alisema wamekabidhi vibao vya kuruhusu na kusimamisha magari kwa shule hizo, reflector vest na madaftari yenye michoro ya usalama barabani ambavyo vitatumiwa na wanafunzi hao katika kampeni hiyo.

Alisema kama kampuni wamekuwa wakizingatia usalama mahali pa kazi, hivyo wameamua kupanua wigo na kujikita pia kwa watoto ambao ni taifa la kesho.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents