Makala

Azam FC na ‘Ukuta wa Berlin’ mechi 10 dakika 900 nyavu zake zimetikiswa mara mbili pekee

Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, ndio timu yenye safu kali ya ulinzi ‘Kuta za Berlin’ miongoni mwa timu 16 zinazoshiriki Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL).

Kikosi cha Azam FC msimu wa mwaka 217/18

Hadi sasa zikiwa zimechezwa mechi 10 za ligi hiyo (sawa na dakika 900), Azam FC imeruhusu nyavu zake kutikiswa mara mbili tu huku kipa wake Razak Abalora, akiiongoza timu hiyo kutoruhusu bao (cleansheets) katika mechi nane (sawa na dakika 720), rekodi inayomfanya kuwa kipa bora kwenye ligi mpaka sasa.

Ukimuondoa Abalora, ukuta huo mgumu wa Azam FC unaundwa pia na mabeki visiki Nahodha Msaidizi, Agrey Moris, Yakubu Mohammed, Bruce Kangwa, Daniel Amoah, waliounda kombinesheni bora ambayo imepelekea mafanikio hayo.

Mabeki wengine ambao nao wameshiriki mafanikio hayo ni David Mwantika, Swaleh Abdallah na Abdallah Kheri, ambao walishirikiana kuziba nafasi za Yakubu na Amoah, waliukosa mchezo wa jana dhidi ya Njombe baada ya kila mmoja kukusanya kadi tatu za njano.

Ubora wa safu ya ulinzi, pia umechagizwa na kikosi hicho kuwa na wachezaji bora kwenye kiungo cha ukabaji, ukianzia kwa Nahodha Himid Mao ‘Ninja’, Frank Domayo. Stephan Kingue, Braison Raphael, Salmin Hoza na kiungo wa juu, Salum Abubakar ‘Sure Boy’, ambao kwa pamoja nao wamekuwa wakiituliza vema safu ya ulinzi.

Licha ya kuwa na uwiano mdogo wa kufunga mabao, kikosi cha Azam FC ni miongoni mwa timu mbili za juu zinazokabana koo kileleni, ikiwa na pointi 22 katika nafasi ya pili sawa na Simba ambayo ipo juu kwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa.

Hadi inamaliza raundi ya 10, Azam FC imefanikiwa kushinda jumla ya mechi sita, sare nne huku ikiwa haijapoteza mchezo wowote na kufunga mabao nane, ambapo tayari kikosi hicho kimeshareja jijini Dar es Salaam leo jioni kikitoka kuichapa Njombe Mji bao 1-0 mkoani Njombe.

Kikosi hicho mara baada ya kurejea, kesho Jumanne jioni kitaanza rasmi maandalizi ya kujiandaa na mchezo ujao wa ligi dhidi ya Mtibwa Sugar unaotarajiwa kuwa mkali na wa aina yake utakaofanyika Uwanja wa Azam Complex Jumatatu ijayo saa 1.00 usiku.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents