Makala: Diamond jitafakari, umewakwaza mashabiki wako (+Audio)

Aliyekuwa nguli wa muziki wa Hip Hop nchini Marekani, Amaru Shakur, 2Pac aliyezaliwa Juni 16, 1971 na kufariki September 13, 1996, alipata kusema, inaweza kukuchukua miaka mingi kupata uaminifu lakini inakuchukua sekunde chache kuupoteza.

Ipo hivi; Watu wanaokuzunguka, kufanya nao kazi, biashara au jambo lolote lile linalowakutanisha, kitendo cha wao kukuamini kwa kile kinachowaunganisha au kuwakutanisha ni jambo lenye kuchukua muda mrefu, pengine miaka kadhaa.

Hata hivyo kuupoteza uaminifu huo mbele ya macho ya wale waliokuamini ni kitendo cha muda mfupi sana. Ni muda ambao upo kasi kama mwanga unaposafiri kwenye chumba chenye giza. Tuachane na hilo.

Kuhusu Diamond

Hapo jana April 15, 2018 msanii Diamond Platnumz aliweka video mtandaoni zikimuonyesha akiwa faragha na wanawake wawili, mmoja wapo hajafahamika na mwingine ni mwanamitindo Hamisa Mobetto aliyezaa nae mtoto mmoja.

Baada ya video hizo mashabiki wake wameonyesha kutopendezwa na kitendo hicho na kukichukulia kama udhalilishaji. Kivipi?, unawezaje kuweka video mbili ndani ya muda mfupi ukiwa na wanawake wawili tofauti.

Diamond hadi kufika hapo alipo kwa sasa amepigana kwa miaka mingi, amepigana usiku na mchana, kiangazi na masika. Kutoka Diamond yule wa Kamwambie hadi leo Diamond wa African Beaut, kuna nguvu ya watu nyuma yake.

Hapo ndipo mashabiki wake waliokuwa naye bega kwa bega kwa kipindi chote hicho wanakereka. Wanamchukulia kama mtu aliyeshiba umaarufu kwa sasa kutokana na kile alichokifanya.

Maoni ya mashabiki wengi katika mitandao wamekosoa vikali kitendo hicho na wengine kwenda mbali zaidi na kumtolea maneno makali yenye kuudhi, hata baadhi ya wasanii nao wameonyesha kutopendezwa na hilo ingawa hawajamlenga moja kwa moja.

Kosa la Diamond lipo Wapi?

Wiki iliyopita April 12, 2018 kulivuja mtandaoni video iliyowaonyesha Nandy na Bill Nass wakiwa faragha. Ni tukio ambalo liligonga vichwa vya habari kwa kiwango chake kutokana na uzito wa wasanii hao katika Bongo Flava.

Siku iliyofuata, April 13, 2018 Nandy aliitwa na Baraza la Sanaa Taifa (BASATA) kwa ajili ya mahojiano kwa kile kilichotokea.

Katibu Mtendaji wa Basata, Godfrey Mngereza alisema kilichotokea kwa Nandy haikuwa kazi ya sanaa ila aliitwa kutokana ni msanii ambaye ni wajibu wao kumlea. Weka Nukta hapo.

Hivyo basi, kitendo cha Diamond kuweka video hizo katika mitandao yake kijamii ni kosa kwani si kazi ya sanaa na hakuna kinachomuunganisha yeye na mashabiki wake.

Ukiweka video za matangazo ya bidhaa zake ni sawa, kwani mashabiki wake ndio wananunuzi wa bidhaa hizo. Video alizoweka ni maisha binafsi na kwa maudhui yake hazipaswi kuonekana hadharani.

Kwa vile alichokifanya hakina uhusiano wowote na sanaa yake ni vigumu kuchukuliwa hatua za kinidhamu na Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kupitia Basata, hata hivyo kuna hatari kubwa ya kudondokea katika sheria ya makosa ya kimtandao (The Cyber crimes Act, 2015) endapo tukio husika likiripotiwa.

Wiki mbili zilizopita, April 01, 2018 wakati Rais Rais Magufuli anapokea ndege ya Tanzania, Bombardier iliyokuwa ikishikiliwa nchini Canada, Diamond alikuwepo katika hafla hiyo na aliweza kuimba na Ras alimpongeza kwa uimbaji wake na sio mara ya kwanza kufanya hivyo.

Sasa leo Rais Magufuli akiona video hizo anamuweka Diamond katika nafasi ipi kimaadili?. Na uhakika hatopendezwa hata kidogo kwani kitambo alishaonya kuhusu hilo.

December 12, 2017 wakati Rais John Magufuli akihutubia katika mkutano wa Jumuiya ya Wazazi CCM alieleza kuwa anaupenda muziki na ni mfuatiliaji, hata hivyo anakerwa na baadhi ya wasanii ambao wanavaa nguo zisizo za maadili katika video za nyimbo zao.

Hivyo Diamond ajitakari kwa hilo alilofanya anaiweka wapi sura yake mbele ya kiongozi mkubwa kama Rais Magufuli ukiachilia mbali mashabiki wake.

Tunafahamu Diamond na wasanii wote waliochini ya label yake, WCB mlezi wao ni Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Paul Makonda, sidhani kama na yeye anafurahishwa na video hizo yeye kama mlezi.

Diamond Ajitafakari Zaidi

Diamond anarejea tena kwenye vichwa vya habari kwa tukio hili, utakumbuka wiki kadhaa zilizopita alikuwa katika mvutano na Naibu Waziri, Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Juliana Shonza mara baada ya nyimbo zake mbili, Waka na Hallelujah kufungiwa.

Katika mahojiano aliyofanya na Times FM, March 19, 2018 alitoa baadhi kauli ambazo si za kiungwana kwa kiongozi huyo kitu kilichopeleka hadi kituo hicho cha radio kuomba radhi hapo, March 28, 2018.

Msanii kuzungumzwa mara kwa mara ni faida katika sanaa yake ila kuzungumzwa katika mambo hasi ni jambo ambalo linatafuna pole pole sanaa ya msanii husika. Diamond ametoka katika mvutano na Wizara, mwezi unaofuata anatenda jambo lingine lisilo la kimaadili, jamii, mashabiki wake na viongozi wake wanamchukuliaje?.

Wakati Katibu Mtendaji wa Basata, Godfrey Mngereza anazungumzia suala la Nandy alieleza licha ya kuwa Nandy hawezi kuadhibiwa na Baraza hilo kutokana kilichotokea ni nje ya wasanaa yake, kuna kitu alionya.

Mngereza alisema kuwa Nandy muziki wake ulikuwa umekubalika hadi kufiki hatua ya kuitwa nyumbani kwa Makamu wa Rais, Mama Samia Hassan Suluu kuimba, pia ni balozi wa Kampeni ya Tulia Trust iliyopo chini ya Naibu Spika wa Bunge, Dkt. Tulia Ackson, hivyo video ile iliyovuja mtandaoni ingeweza kumuharibia kama si kumuweka mbali na viongozi hao.

Hivyo Diamond ajitafakari kwa kile alichokifanya kwani kuna mashabiki wake anawakaza na viongozi wakubwa walionyuma yake atawakosesha sababu ya kuufuatilia muziki wake na kumpigania katika lolote lile. Asante.

Related Articles

Bongo5

FREE
VIEW