Uncategorized

Mvua iliyokwama Tanzania yawasili Kenya ghafla, wakazi wa Nairobi washindwa kuamini

Hatimaye ‘mbingu zimefunguka’ nchini Kenya na jiji la Nairobi kwa mara ya kwanza lilipata hali ya unyevu mwaka 2019.

Mvua hiyo iliodaiwa kukwama nchini Tanzania ilinyesha kwa ghafla na kuwapata Wakenya wengi wakiwa hawajajiandaa.

Wachuuzi waliokuwa wakiuza mali yao katika barabara za jiji la Nairobi waliathiriwa na mvua hiyo.

Waendesha magari na raia pia walipatikana wakati ilipokuwa ikinyesha lakini hakuna aliyeonekana akijali.

Wakaazi walionekana wakitembea katika mvua bila kujali kwamba walikuwa wakinyeshewa.

Masaa mawili kabla ya mvua hiyo kunyesha, idara ya hali ya hewa nchini Kenya ilikuwa imetangaza kuwa mvua itanyesha jijini Nairobi, viungani mwake na maeneo mengine.

Raia wengi waliohojiwa walisema kwamba hawakutarajia mvua kunyesha.

”Sikutarajia kwamba itanyesha na nilipokuwa nikiendelea na biashara yangu , mvua ilinyesha na nikalazimika kutafuta hifadhi kwengineko” , alisema John Kimani ambaye ni mchuuzi.

Wiki iliopita idara ya hali ya hewa kupitia Naibu Mkurugenzi wake Bernad Chanzu ilikuwa imesema kuwa hakutakuwa na mvua msimu huu.

Bwana Chanzu pia aliwatahadharisha Wakenya kujiandaa kwa uhaba mkubwa wa maji ya kunywa, usafi na matumizi ya viwandani mbali na kuleta umeme.

Wiki mbili zilizopita idara hiyo ilikuwa imetangza kuwa kiangazi kitaendelea mwisho wa mwezi huu huku mawingu ya mvua yakisalia nchini Tanzania kutokana na kiwango cha chini cha upepo wa kusukuma mawingu hayo kuelekea kaskazini.

Kaimu mkurugenzi wa shirika la hali ya anga nchini Kenya Stella Aura alielezea hatahivyo kuwa mvua ndefu imechelewa lakini inatarajiwa kuanza kunyesha mwisho wa mwezi huu.

Mwezi Aprili ndio mwezi wa mvua ndefu nchini Kenya na onyo limetolewa katika maeneo kadhaa ya Kenya kuhusu kuchelewa kwake.

”Mvua ya msimu husababishwa na upepo wa mvua unaoelekea kaskazini lakini kufikia sasa upepo huo haujaelekea kaskazini”, aliambia vyombo vya habari.

”Mvua imekwama nchini Tanzania, mifumo ya upepo iliopo kusini haijashikamana kuweza kusukuma mawingu hivyobasi mvua itachelewa , lakini itaanza kunyesha mwisho wa mwezi huu”, alisema.

Mvua ndefu

Hatahivyo amesema kuwa mvua ndefu imeanza lakini kwa kiwango kidogo katika maeneo mbalimbali.

Mvua ndefu hunyesha miezi ya Machi, Aprili, na Mei hususan katika eneo la magharibi , bonde la Ufa na mkoa wa kati na ni muhimu sana katika sekta ya kilimo hatua inayosababisha kuwepo kwa chakula cha kutosha.

Idara hiyo imewashauri wakulima kupanda mimea inayokuwa kwa haraka na ile isiotegemea maji kwa kuwa mvua hiyo huenda isinyeshe kwa muda mrefu.

Wale wanaoishi katika maeneo ya nyanja za chini ikiwemo miji midogo isio na mitaro ya kusafirisha maji walionywa kwamba watarajie mafuriko.

Magharibi mwa Kenya, visa vya radi vinatarajiwa kuongezeka huku maporomoko yakitarajiwa kufanyika katika maeneo ya juu ikiwemo Murang’a na Meru miongoni mwa mengine.

Maporomoko pia yanatarajiwa kuathiri maeneo ya magharibi na mkoa wa Bonde la Ufa.

”Mikakati inafaa kuwekwa ili kuzuia maafo yoyote” ,ilishauri idara hiyo.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents