Uncategorized

Rais wa Sudan Omar al-Bashir atangaza hali ya hatari, ateua wakuu wa vikosi vya usalama kuchukua nafasi za magavana

Rais wa Sudan Omar al-Bashir ametangaza hali ya hatari nchini humo na kufutilia mbali utawala wa majimbo na uongozi wake.

Kwa mujibu wa shirika la habari la BBC, Katika hotuba yake kwa taifa rais Bashir alisema kuwa maandamano yanayoshuhudiwa nchini yanalenga kuvuruga amani na kuhujumu utawala wake.

“Natangaza hali ya hatari kote nchini kwa mwaka mmoja.”

“Natangaza kuvunjiliwa mbali kwa utawala wa majimbo katika ngazi zote hadi za mikoa.”

Waandamanaji walimiminika katika mji wa Omdurman baada ya tangazo hilo, lakini waliyoshuhudia wanasema maandamano hayo yalizimwa na polisi kwa kutumia mabomu ya machozi.

Saa kadhaa baada ya tangazo hilo rais Bashir amewateua wakuu wa vikosi vya usalama kuchukua nafasi ya magavana waliyofutwa kazi.

Katika hotuba yake kwa taifa bwana Bashir ameliomba bunge kuahirisha mchakato wa marekebisho ya katiba ambao ungemruhusu kugombe muhula mwingine madarakani.

Bashir pia alisema kuwa maandamano yanayoshuhudiwa nchini yanalenga kuvuruga amani na kuhujumu utawala wake.

Ripoti za awali kutoka shirika la kitaifa la ujasusi (NISS) ziliashiria kuwa Bashir huenda akajiuzulu.

Lakini saa kadhaa baada ya tangazo hilo alitoa amri ya rais ya kuwateua maafisa wa kijeshi na wa vikosi vingine vya usalama kusimamia mikoa 18 ya nchi hiyo.

Pia alitangaza kuwa mawaziri watano ikiwa ni pamoja na wizara ya mambo ya nje, ulinzi na ile haki wataendelea kushikilia nyadhifa zao.

Maandamano ya kuipinga serikali kwa mara ya kwanza yalianza katikati ya mwezi Desemba mwaka jana kufuatia kupanda kwa gharama ya maisha.

Bei ya mkate ilipanda mara tatu katika baadhi ya maeneo na bei ya mafuta pia ikapanda.

Zaidi ya watu 1,000 wameripotiwa kukamatwa tangu maandamano hayo yalipoanza.

Makundi ya kutetea haki yanasema zaidi ya watu 40 wameuawa wakati wa makabiliano kati yao na vikosi vya usalama.

Kwa mujibu wa shirika la habari la AFP, waandalizi wa maandamano hayo wameapa kuendelea na juhudi hizo hadi pale bwana Bashir atakapoachia madaraka.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents