Siasa

Siri ya CCM Butiama

CCMMUASISI wa hoja ya kuurejesha muafaka wa kisiasa visiwani kwa wananchi, kwa njia ya kupigwa kura ya maoni, ni Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), Amani Abeid Karume, imefahamika

na Mwandishi Wa Tanzania Daima


 


MUASISI wa hoja ya kuurejesha muafaka wa kisiasa visiwani kwa wananchi, kwa njia ya kupigwa kura ya maoni, ni Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), Amani Abeid Karume, imefahamika.


Nyaraka ambazo gazeti hili limeziona, zinaonyesha kuwa, kamati ya mazungumzo ya muafaka ya CCM ilipewa pendekezo hilo na Rais Karume, nayo ikakubali kuliongeza katika rasimu ya makubaliano ambayo iliwasilishwa katika vikao vya juu vya chama hicho vilivyofanyika Butiama, mkoani Mara wiki iliyopita.


Mapendekezo hayo ya Karume, ndiyo yaliyoleta mustakabali tofauti wa mazungumzo hayo, kwani yanaonekana kuwa yaliingiza suala jipya, ambalo halikuwamo katika makubaliano ya awali ya kamati ya mazungumzo.


Taarifa ambazo gazeti hili linazo zineleza kuwa, mapendekezo hayo ya Karume yaliwasilishwa kama yalivyo na Katibu Mkuu wa CCM, Yusufu Makamba, kwanza ndani ya Kamati Kuu na baadaye katika kikao cha Halmashauri Kuu ya chama hicho.


“Liko wazo ambalo ujumbe wetu umelipata kutoka kwa Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar, Rais Amani Abeid Karume, linalohusu uzito wa makubaliano juu ya kuanzisha mustakabali mpya wa kisiasa kwa msingi wa serikali shirikishi katika Zanzibar. Yeye alikuwa na fikra kwamba jambo kubwa na la kutia matumaini kama hili, isingefaa maamuzi yake yakahitimishwa na viongozi katika Kamati Kuu na NEC tu.


“Kwa vile wadau wakuu katika hili ni wananchi wenyewe wa Zanzibar, ingekuwa bora kama suala hili likafikishwa kwao. Sisi (inataja wajumbe wa kamati ya muafaka ya CCM) tulivutiwa sana na pendekezo hili na tuliliunga mkono,” inasema taarifa hiyo ya kamati ya muafaka katika ukurasa wa 14 wa taarifa yake iliyosomwa Butiama mwishoni mwa wiki iliyopita.


Taarifa zaidi zinaeleza kwamba hitimisho la hoja hiyo ya Karume katika taarifa hiyo ya muafaka ya CCM iliyo ukurasa huo huo wa 14 yenye maneno yasemayo; “ …kwa kukubali wazo hili (la Karume kuhusu kura ya maoni) CCM itakuwa imeipiku CUF katika ubunifu wa kujenga” ndiyo iliyosababisha chama hicho cha upinzani kuhamaki na kuanza kuvutana na mahasimu wao hao wa chama tawala.


Habari za uhakika kutoka ndani ya CUF zinaeleza kuwa, pendekezo hili la Karume ambalo halijapata kujadiliwa katika vikao vyao vya pamoja na CCM ndilo ambalo kimsingi limesababisha hali ya wasiwasi na kutoaminiana iliyosababisha waamue kususa mazungumzo ya ziada.


Taarifa inaonyesha kuwa hoja hiyo ya Rais Karume, iliwavutia Makamba, Ali Ameir Mohamed na Kingunge Ngombale-Mwiru, ambao walikuwa ni wajumbe wa kamati hiyo kutoka CCM, na wakaamua kuiunga mkono wakitoa sababu tatu za kufanya hivyo.


Kwanza, wajumbe hao walisema kuwa suala hilo lina masilahi kwa CCM kwa sababu hiyo ni demokrasia na moja kwa moja, na pili, suala hilo litasaidia kufifisha madai madogo madogo kutoka kwa CUF ili watu wajielekeze zaidi katika masilahi makubwa ya watu na nchi.


Aidha, ilielezwa kuwa sababu ya tatu ya kuafiki hoja hiyo ni kuwa kura ya maoni ni njia ya uhakika ya kuwashirikisha wananchi wengi katika ujenzi wa mazingira ya kuaminiana kuelekea kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010.


Kubainika huku kwa taarifa za ndani ya CC na NEC ya CCM zinazidi kuthibitisha habari zilizopata kuandikwa na gazeti hili kwa mara ya kwanza zikimtaja Karume kuwa ndiye kikwazo cha kufikiwa kwa muafaka wa kisiasa visiwani.


Habari hiyo iliyoandikwa katika Tanzania Daima, haraka haraka ilitolewa kauli ya kukanushwa kwa nguvu kubwa na viongozi wa CCM, akiwamo Makamba mwenyewe, kabla ukweli haujathibitishwa Butiama.


Aidha, licha ya kuthibitisha kuwa hoja hiyo ya Karume haikuwamo katika makubaliano ya awali, vyanzo vyetu kutoka ndani ya CUF vimeeleza kuwa, haiwezekani hoja hiyo ikawemo katika taarifa hiyo iliyowasilishwa kwenye vikao vya CC na NEC, halafu baadaye ielezwe kuwa mabadiliko yaliyofanywa yalitokana na vikao hivyo.


“Kinachoonekana hapa ni kuwa hoja hii iliingizwa na kuwasilishwa CC na NEC. Si kweli kuwa CC na NEC ndiyo iliyopendekeza hoja hii, si kweli hata kidogo,” alisisitiza kiongozi mmoja wa CUF ambaye hakupenda kutajwa jina lake.


Kiongozi huyo anasema kuwa itifaki zinaonyesha kuwa ripoti hiyo ya CCM isingeweza kuwasilishwa kwenye vikao vya CC na NEC, bila ya Mwenyekiti wa chama hicho, Rais Jakaya Kikwete kuiona.


“Hivyo tunaamini kuwa (Rais Kikwete) aliliona suala hili na akabariki lipelekwe mbele… haiwezekani kuwa na yeye taarifa hii aliisikia kwa mara ya kwanza alipokuwa anaongoza kikao cha CC,” aliongeza kiongozi huyo wa CUF.


Kiongozi mwingine wa juu wa CUF aliieleza Tanzania Daima kuwa, lengo la siri la CCM katika pendekezo hilo la Karume ni kutaka kuona chama chao kikinyimwa fursa ya kufanya lolote la maana kabla ya mwaka 2010.


“Tumesikia kwamba hawa jamaa wa CCM wanaogopa kwamba tukiruhusiwa kuunda serikali ya mseto au ya umoja wa kitaifa Zanzibar tutakuwa tumewapiku kisiasa na kuchukua madaraka mwaka 2010. Hiyo ndiyo hofu ya CCM,” alisema kiongozi huyo.


Kauli hizo zinatolewa siku moja tu baada ya Rais Kikwete mwenyewe, juzi kuhutubia taifa na kusema kwamba, CCM bado ilikuwa na dhamira ile ile ya kuendeleza muafaka na kutafuta suluhu ya kudumu Zanzibar.


Aidha, katika taarifa yake hiyo, kamati hiyo ya muafaka ya CCM ilivieleza vikao vya CC na NEC kuwa katika kamati yao ya pamoja iliyokuwa na wajumbe 12, sita kutoka katika kila chama, ilikubaliana kimsingi juu ya muundo wa serikali hiyo, itakayokuwa na rais na makamu wa rais wawili.


Taarifa hiyo yenye kurasa 16, inadokeza kuwa chini ya muundo huo, rais atatokana na chama ambacho kitashinda uchaguzi, makamu wa kwanza atatoka katika chama kitakachoshika nafasi ya pili na makamu wa rais wa pili atatoka katika chama cha rais, na ndiye atakayerithi nafasi ya rais iwapo litatokea lisilotarajiwa.


 


Source: Tanzania Daima

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents