Bongo5 Makala

Wasanii wa Tanzania waanze kujipanga kufanya ziara zao binafsi za muziki sasa!

J. Cole ametangaza ziara yake ya Marekani iitwayo ‘Forest Hills Drive Tour’ yenye show 20 ambapo ataongozana na wasanii wengine wakiwemo Big Sean.

concert-11

Lakini pia Chris Brown na Trey Songz wana yao iitwayo ‘Between The Sheets Tour’ nchini humo. Ziara kama hizo ni za kawaida kwa Marekani na wasanii wote wanaofanya vizuri wamekuwa wakifanya zao. Ziara kwa wasanii wengi wa Marekani ni chanzo kikubwa cha mapato ukiachialia mbali mauzo ya kazi zao, biashara zao binafsi na mikataba ya matangazo. Kwa mfano ziara ya Beyonce na Jay Z, On The Run ya mwaka jana iliwaingizia zaidi ya dola milioni 100.

Kwa Tanzania hali bado ni tofauti. Show nyingi unazosikia wasanii wanazifanya ni zile ambazo promoter ameandaa na kuwalipa kwaajili ya kufanya show. Ziara kubwa zinazofanyika kila mwaka ni mbili tu, Fiesta na Kilimanjaro Music Tour. Ukitoa matamasha hayo, hakuna ziara nyingine inayofanyika nchini zaidi ya show za msanii mmoja mmoja ama wakiwa wengi basi wanne ambazo hufanyika katika mji mmoja tu.

Nafahamu kuwa si kazi rahisi hata kidogo na gharama kubwa huhitaji kufanikisha ziara kama hizo lakini kwanini wasanii wasijaribu wakati wengi wao wana mashabiki wengi?

Hata wasanii wakubwa tunaofahamu uwezo wao kifedha akiwemo Diamond Platnumz hawajawahi kufanya ziara zao wao wenyewe. Kuna haja sasa wasanii wakaanza kufikiria kutengeneza ziara ya labda katika miji 15 nchini kama wafanyavyo nchini za wenzetu.

Kwa proposal nzuri na mipango inayoonekana kuzaa matunda, makampuni mengi mno yanaweza kuwaunga mkono kwa kudhamini ziara hizo ambapo nayo yakatumia kutangaza bidhaa zao.

Nakubali kuwa kuna baadhi ya mambo ambayo hatuwezi kujifananisha na Wamarekani, lakini suala la msanii kuandaa tour yake linawezekana kabisa na ni muda sasa tukaanza kuelekea huko.

Nafahamu jinsi ziara za wanamuziki wa nje zilivyo na headache hasa kwakuwa msanii huongozana na timu kubwa sana kufanikisha hilo hivyo si lazima nasi tufanye hivyo lakini kwa level zetu msanii anaweza kufanikisha hilo iwapo ataamua. Wenzetu wanafanyaje kwenye ziara zao?

Hebu tujifunze na pengine tunaweza kutumia yale yaliyo ndani ya uwezo wetu kufanya ziara zetu.

Kwanza, tuangaalie ni mambo gani muhimu wasanii wa huko hutakiwa kujiuliza kabla ya kufikiria kufanya ziara zao wenyewe. Msanii akishirikiana na meneja wake ama timu yake maalum anayoweza kuitafuta kwaaajili ya shughuli anatakiwa kuzingatia maswali haya:

Ni katika mji gani na ukumbi gani au uwanja upi unataka kutumbuiza? Una vyombo gani vya kutumbuizia unavyohitaji kwa maana ya vyombo vya muziki kama unataka kufanya live performance?

Ni jukwaa gani, sound na taa ulizonazo?

Ni vifaa gani ambavyo bendi yako itasafiri navyo na vipi vitahitajika kuwepo kwenye ukumbi?

Ni idadi gani ya watu kwenye crew unayohitaji kuituma kwenye eneo la show na ujuzi gani au mafunzo wanayohitaji kuwa nayo?

Bajeti gani ya kuanzia uliyonayo kwaajili ya ziara yakiwemo malipo kwa wafanyakazi na gharama za vyombo?

Unapomaliza kufikiria masuala haya ya msingi, unahitaji kupata mtu ambaye atakuunganisha na audience yako. Kwa wenzetu wana utaratibu wa kuwa na ajenti anayesimamia masuala ya bookings. Lakini bila kujali unaye ama huna, wewe ama ajenti wako anahitaji kufanya kazi kupitia promoter au promoter wa ziara ambaye huandaa ziara hiyo.

Kufanya kazi na mapromota wa matamasha

Unaweza kujaribu kuandaa ziara yako lakini hauwezi kufika popote. Kwa wenzetu, kumbi au viwanja husimamiwa au vingine humilikiwa kabisa na mapromota wa matamasha. Wasanii hao hutakiwa kusaini mikataba na promota wa ziara kuandaa ziara hiyo.

Promota wa ziara huandaa ziara ya muziki wa live na huhakikisha kuwa inalipa. Hiyo ni pamoja na kutangaza au hata kulipia matamasha kwenye viwanja, kumbi, matamasha na matukio mengine. Kama ilivyo tu kwa mapromota wa Tanzania, nao hutafuta msanii, ukumbi, wafanyakazi, na kusimamia matangazo, marketing na pengine mauzo ya tiketi.

Kwa Marekani mapromota wakubwa wa ziara za kitaifa ni pamoja na Live Nation na AEG Live ambao hata hivyo hufanya kazi na wasanii wakubwa tu kama Madonna, Jay Z nk.

Timu ambayo msanii anatakiwa kuwa nayo kwenye ziara yake:

Tour manager au road manager: Huyu kazi yake ni kuhakikisha masuala ya usafiri, kulipa bili na kusimamia matatizo yanayotokea wakati msanii akiwa ziarani.

Production manager: Huyu kazi yake ni kusimamia timu ya ufundi na hufanya kazi na timu iliyopo kwenye ukumbi wanakofanyia show yenyewe. Husimamia pia kusafirisha vyombo kutoka ukumbi mmoja kwenda mwingine ikiwa ni pamoja na kuvifunga au kuvifungua.

Advance person: Huyu hufika mapema kwenye eneo la show kabla ya msanii na timu yake hajafika ili kumsaidia road manager na kuweka mipango ya mwanzo.

Stage manager: Huyu kazi yake ni kusimamia mizunguko ya watumbuizaji na crew juu na chini ya jukwaa.

Sound engineer: Husimamia mitambo yote kwenye show na sauti wanayosikia wahudhuriaji.

Monitor engineer: Huyu husimamia sauti ambayo msanii na bendi yake husikia wakati wa show.

Sound crew: Hii ni timu inayofunga, kufungua na kuendesha vyombo vya sauti kama wanavyoelekezwa na sound na monitor engineers.

Lighting operator: Huyu kazi yake ni kusimamia taa za kwenye ukumbi na husimamia timu inayoshughulikia masuala ya taa.

Lighting crew: Hufunga na hufungua na kusimamia taa.

Backline crew: Hawa hufunga na kusimamia vyombo vinavyotumika kutumbuizia.

Wakati msanii anapochukua watu hawa ni lazima atafute watu ambao:

Flexible na kuzoeleka. Kuna uwezekano wa kutokea mushkeli kwenye show na hivyo unahitaji kuwa na mtu ambaye anaweza kushughulikia masuala haraka na kwa utulivu.

Watu wanaoweza kufanya kazi kwenye timu watakaolewana na bendi na mameneja wengine kupunguza misuguano barabarani.

Wenye ujuzi kwenye kazi wanazozifanya na wana uzoefu kwenye vyombo ili waweze kuvitumia vyema kwenye kumbi ambazo hawajazizoea.

Wamejitolea vilivyo kwenye timu ya msanii huyo kiasi cha kuvumilia usumbufu unaoweza kutokea wakiwa barabarani na kuendelea kuwepo kwenye ziara hadi mwisho.

Na mwisho kama unataka kufanya show nzuri ya live, huu ni ushauri kutoka kwa wazoefu:

Usitumbuize kwenye ukumbi ule ule mara nyingi lasivyo mauzo ya tiketi yanaweza kupungua.

Tambua tofauti kati recording session na live performance na wape mashabiki show ya kukumbuka.

Jibadilishe na weka vitu vipya kwenye show zako ili kuwafanya mashabiki waje tena kila mwaka.

Chanzo: howstuffworks.com

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents