Habari

Serikali yaingilia gogoro la msikiti Temeke

Serikali kupitia Wizara ya Katiba na Sheria, imesimamisha shughuli zote za Bodi ya Udhamini wa Msikiti wa Al-Qadri uliopo Temeke jijini Dar es Salaam, baada ya kubaini wajumbe wake siyo halali.

Na Abdul Mitumba, Temeke



Serikali kupitia Wizara ya Katiba na Sheria, imesimamisha shughuli zote za Bodi ya Udhamini wa Msikiti wa Al-Qadri uliopo Temeke jijini Dar es Salaam, baada ya kubaini wajumbe wake siyo halali.


Bodi hiyo inayoundwa na watu saba inadaiwa kuwasilisha vielelezo bandia katika ofisi ya Wakala wa Usajili na Udhamini, RITA, kisha kutwaa mamlaka ya msikiti huo, jambo ambalo lilisababisha vurugu.


Kwa mujibu wa barua iliyoandikwa na ofisi ya Kabidhi Wasii Mkuu kwenda kwa wajumbe wa Bodi hiyo ya Machi 27, mwaka huu, wajumbe hao waliingiza majina yao katika kumbukumbu za ofisi yake kijanja kwa maelezo kuwa walifanya uchaguzi Oktoba 3, 2005 wakati siyo kweli.


Barua hiyo iliyosainiwa na Bw.T.Z.M. Rugonzibwa kwa niaba ya Msimamizi Mkuu wa Wadhamini, imesema kwa kuwa suala la nani awe Mdhamini wa Msikiti huo lipo katika Makahama Kuu kanda ya Dar es Salaam, hali katika msikiti huo inapaswa kuachwa kama ilivyo.


Bw.Rugonzibwa amesema katika barua hiyo yenye Kumbukumbu Na.ADG/TI/857/50 kuwa suala hilo lilifikishwa Mahakama Kuu na kusajiliwa kwa Na.134/2006, hivyo akawataka wadhamini wapya kuiachia Bodi ya awali kuendelea na majukumu katika Msikiti huo hadi maamuzi yatakapotolewa.


Waliopigwa stopu kujishughulisha na kazi msikitini hapo ni pamoja na Bw. Ally Mkoyogore, Bw. Zailay Mkoyogore, Bw. Mintanga Moshi, Bw. Ahmed Mwami, Nurati Ludha, Bw. Shaaban Kiluka na Bw. Seif Juma Seif.


Agizo hilo la serikali limekuja wakati msikiti huo umekumbwa na mgogoro mkubwa wa uongozi, ambapo Bodi iliyosimamishwa imeipindua ya zamani wakati shauri hilo halijaamriwa na mahakama.


Katibu mkuu wa Bodi ya zamani, Bw.Farid Salah amethibitisha kufanyika kwa mapinduzi hayo na kuongeza kuwa ofisi za utawala wa shule inayomilikiwa na msikiti huo zote zimefungwa.


Bw.Salah, ambaye pia ni Meneja wa shule hiyo amesema mgogoro huo umesababisha masomo kusimama, ambapo walimu karibu wote 18 na wafanyakazi wengine watano kukimbia eneo la shule.


Mjumbe wa Bodi mpya iliyosimamishwa na serikali, Bw.Mintanga Samata amethibitisha kuwepo kwa hali hiyo na kusema Mwenyekiti wake, Bw. Ally Muhidini, atatoa taarifa rasmi kwa waandishi wa habari Jumamosi wiki hii


Source: Alasiri

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents