Siasa

Balali kusakwa

Gavana BalaliSerikali imesema itamsaka Gavana wa zamani wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Dk. Daudi Balali mahali popote alipo muda utakapowadia


 



Na Mashaka Mgeta



 


Serikali imesema itamsaka Gavana wa zamani wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Dk. Daudi Balali mahali popote alipo muda utakapowadia.

Kwa mujibu wa ofisi ya Rais, mbali na Dk. Balali, aliyekuwa Waziri wa Miundombinu, Bw. Andrew Chenge, `amewekwa kiporo` ili kupisha uchunguzi dhidi ya tuhuma zinazomkabili kufanyika, na hatimaye kuchukuliwa hatua kulingana na matokeo yatakayopatikana.

Hayo yalisemwa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Bw. Salva Rweyemamu, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari, Ikulu, jijini Dar es Salaam jana.

Jana, gazeti hili lilimkariri Waziri wa Fedha na Mambo ya Uchumi, Bw. Mustafa Mkulo, akisema serikali haijui mahali alipo Dk. Balali, na kwamba timu iliyoundwa na Rais Jakaya Kikwete, inaendelea kushughulikia masuala yote yanayohusiana na Gavana huyo wa zamani wa BoT.

Hata hivyo, katika maelezo yake, Bw. Rweyemamu alisema hatua ya Rais Kikwete kumfukuza kazi Dk. Balali, ilimfanya (Balali) kuwa raia wa kawaida, mwenye uhuru wa kuishi mahali popote anapotaka, alimradi havunji sheria.

Taarifa zilizotolewa kwa mara ya mwisho na aliyekuwa Waziri wa Fedha, Bi. Zakhia Meghji, zilisema Dk. Balali alikuwa katika hospitali moja huko Boston nchini Uingereza, akipata matibabu ya ugonjwa ambao hata hivyo haukujulikana.

“Balali ni raia wa kawaida mwenye mambo binafsi, hivi sasa hatafutwi, lakini ukifika wakati wa kufanya hivyo, serikali itajua yupo wapi na tutampata tu,“ alisema.

Dk. Balali alifukuzwa kazi na Rais Kikwete, baada ya ripoti ya ukaguzi iliyofanywa na kampuni ya Ernst and Young kubaini vitendo vya ufisadi, vilivyosabaisha upotevu wa mabilioni ya fedha katika Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA).

Hatua ya kufukuzwa kazi ilitangazwa wakati Dk. Balali, akidaiwa kuwa Marekani kwa ajili ya matibabu.

Kwa upande mwingine, Bw. Rweyemamu, alisema uamuzi wa kumkamata na kumfungulia mashtaka Bw. Chenge, utafikiwa baada ya uchunguzi wa tuhuma zinazomkabili kukamilika.

Bw. Chenge ambaye pia ni Mbunge wa Bariadi Magharibi, anatuhumiwa kuhifadhi takribani Dola 1,000,000 za Marekani kwenye benki iliyoko katika visiwa vya Jersey, Uingereza, fedha zinazohisiwa zilipatikana kwa njia ya ufisadi katika ununuzi wa rada, wakati wa serikali ya awamu ya tatu, iliyoongozwa na Bw. Benjamin Mkapa.

“Tukisema tumkamate Chenge sasa hivi, kutakuwa na kelele kutoka kwa wanaharakati wa haki za binadamu na hata ninyi waandishi wa habari. Tusubiri uchunguzi ukamilike,“ alisema.

Aidha, alisema Rais Jakaya Kikwete, bado hajafikia uamuzi wa kumtangaza Waziri wa Miundombinu, kuziba nafasi iliyoachwa na Bw. Chenge.

“Suala la kumtangaza Waziri wa Miundombinu litafanywa kwa umma na si kificho, hivyo wananchi wasubiri tu, kwa sababu suala hili haliwezi kufanyika kinyemela,“ alisema.

Pia Bw. Rweyemamu, alisema suluhu ya mgogoro wa kisiasa visiwani Zanzibar baina ya Chama cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Wananchi (CUF), inastahili kufikiwa kwenye meza ya mazungumzo.

CUF ilitangaza kutoendelea na mazungumzo hayo baada ya Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, kuazimia kuwa makubaliano ya kuundwa serikali ya mseto visiwani humo, yanapaswa kupata ridhaa ya wananchi, kupitia kura za maoni.

Msimamo wa CUF ni kwamba suala la kura ya maoni halikuwepo katika ajenda za mazungumzo baina ya vyama hivyo.


 


Source: Nipashe

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents