Habari

Balozi wa Marekani nchini aitwa na serikali kujieleza, Akiri ubalozi wake umefanya makosa kutoa tahadhari ya shambulio la kigaidi Dar

Serikali kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, imemwita Kaimu Balozi wa Marekani nchini, kutoa ufafanuzi kuhusu taarifa ambayo ubalozi huo, uliitoa juu ya angalizo la kiusalama la uwezekano wa kutokea kwa shambulio la kigaidi.

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Faraji Kasidi Mnyepe akimsikiliza Mwakilishi wa Kaimu Balozi wa Marekani hapa Nchini Bi Ann Marie Warmenhoven – Tilias.

Juzi, Ubalozi wa Marekani nchini ulitoa taarifa ya angalizo la kiusalama kuhusu shambulio la kigaidi katika baadhi ya maeneo ya Jiji la Dar es Salaam ikiwemo eneo la Masaki.

US Embassy Tanzania

@usembassytz

Security Alert – United States Embassy Dar es Salaam Tanzania (19 June, 2019)

View image on Twitter
502 people are talking about this

Kufuatia mwito huo, taarifa iliyotolewa jana na wizara ilisema ubalozi huo  ulimtuma mwakilishi wa Kaimu Balozi wa Marekani, Ann Marie Warmenhoven – Tilias, ambaye aliutambua na kukiri kuwa ujumbe huo umetumwa na ubalozi wa Marekani  nchini.

Katika ufafanuzi wake, kwa mujibu wa taarifa hiyo, mwakilishi huyo alikiri kuwa, “ubalozi wake umefanya makosa ya kutoa taarifa ambazo hazikuwalenga raia wa Marekani pekee bali raia wote wakitambua kuwa ubalozi hauna mamlaka ya kufanya hivyo, jambo lililosababisha taharuki kwa wananchi na wageni wanaotarajia kuitembelea Tanzania.”.

Kutokana na kukiri huko, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki imeukumbusha Ubalozi wa Marekani umuhimu wa kuzingatia sheria za nchi na taratibu za kidiplomasia zinazokubalika duniani kote katika utoaji wa taarifa za aina hii,” iliongeza taarifa hiyo.

Kwa upande mwingine, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk. Faraji Mnyepe, alikaririwa katika taarifa hiyo akiwataka wananchi na jumuiya za kimataifa pamoja na wageni walioko  nchini na wanaotarajia kuitembelea Tanzania, kuendelea na shughuli zao kama kawaida kwa kuwa mpaka sasa hakuna taarifa yoyote iliyothibitishwa ya kuwapo kwa tishio la aina hiyo.

SOMA ZAIDI TAARIFA ILIYOTOLEWA NA WIZARA YA MAMBO YA NJE.

WIZARA YA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA YA MASHARIKI WAMWITA KAIMU BALOZI WA MAREKANI WIZARANI

Tarehe 19 June 2019, Ubalozi wa Marekani Nchini Tanzania ulitoa taarifa katika mitandao ya kijamii “Twitter” kuhusu angalizo la kiusalama “security alert”. Angalizo hilo la kiusalama lilitokana na uvumi unaodaiwa na ubalozi huo kusambaa kuhusu uwezekano wa kutokea kwa shambulio katika baadhi ya maeneo ya jiji la Dar es Salaam.

Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ulimwita wizarani Kaimu Balozi wa Marekani ili kutoa ufafanuzi wa “twitter” yao. Ubalozi wa Marekani ulimtuma Mwakilishi wa Kaimu Balozi wa Marekani Bi Janine S. Young kuonana na uongozi wa Wizara.

Bi Janine S. Young ameutambua na kukiri kuwa ujumbe huo umetumwa na ubalozi wa Marekani hapa nchini. Katika ufafanuzi wake amekiri kuwa Ubalozi umefanya makosa ya kutoa tetesi ambazo hazikuwalenga raia wa Marekani pekee bali raia wote wakitambua kuwa Ubalozi hauna mamlaka ya kufanya hivyo jambo lililosababisha taharuki kwa wananchi na wageni wanaotarajia kuitembelea Tanzania.

Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki imeukumbusha Ubalozi wa Marekani umuhimu wa kuzingatia sheria za nchi na taratibu za kidiplomasia zinazokubalika duniani kote katika utoaji wa taarifa za aina hii.

Aidha, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dkt. Faraji Kasidi Mnyepe amewataka wananchi na Jumuiya za Kimataifa pamoja na wageni mbalimbali waliopo nchini na wanaotarajia kuitembelea Tanzania kuendelea na shughuli zao kama kawaida kwani mpaka sasa hakuna taarifa yeyote iliyothibitishwa ya kuwepo kwa tishio la aina hiyo hapa nchini na kwamba Vyombo vya Ulinzi na Usalama vimejizatiti kukabiliana na matishio yeyote.

Imetolewa na:

Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Dar Es Salaam.
20 Juni 2019

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents