Habari

Corona: Waziri Mkuu wa Uingereza alazwa Hospitali

Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson amelazwa hospitalini ili kufanyiwa vipimo vya virusi vya corona, siku 10 baada ya kukutwa na virusi vya ugonjwa huo, ofisi yake ya Downing Street imesema.

Alikimbizwa katika hospitali moja ya mjini London siku ya Jumapili akionyesha dalili za virusi hivyo ikiwemo kiwango cha juu cha joto mwilini. Imedaiwa kuwa hatua hiyo ya tahadhari ilichukuliwa kutokana na ushauri wa daktari wake.

Waziri mkuu bado ndie msimamizi wa serikali, lakini waziri wa maswala ya kigeni nchini humo anatarajiwa kuongoza mkutano wa virusi vya corona siku ya Jumatatu.

Hatua hiyo inajiri baada ya malkia Elizabeth kulihutubia taifa akisema kwamba Uingereza itafanikiwa katika vita vyake dhidi ya mlipuko wa virusi hivyo.

Katika hotuba isio ya kawaida, malkia huyo aliwashukuru raia kwa kufuata maelezo ya serikali kusalia nyumbani huku akiwapongeza wale waliojitolea kuwasaidia wengine.

Pia aliwashukuru wafanyakazi muhimu akisema kuwa kila saa la kazi linazidi kuirejesha Uingereza katika hali yake ya kawaida.

Hotuba hiyo inajiri huku idadi ya watu waliofariki kutokana na virusi hivyo nchini Uingereza ikipanda na kufikia 4,934.

Akizungumza katika jumba la kifalme la Windsor, malkia huyo alisema kwamba tumekumbwa na changamoto nyingi katika siku za nyuma lakini hii ni tofauti.

Aliongezea kwamba wakati huu tutaungana na mataifa mengine duniani kwa kutumia hatua za kisayansi zilizopigwa ili kujiponya. tutafanikiwa na kwamba ufanisi huo utakuwa wa kila mtu.malkia Elizabeth

Malkia Elizabeth

Wakati huohuo waziri mkuu Boris Johnson anatarajiwa kulala hospitali na anaendelea kile kinachotajwa kuwa vipimo vya kawaida kulingana na muhariri wa BBC anayesimamia maswala ya kisiasa Laura Kuenssberg.

Katika taarifa , msemaji wa afisi ya waziri mkuu alisema: Waziri mkuu anaendelea kuwa na dalili za virusi vya corona siku chache baada ya kukutwa na virusi hivyo.

Aliongezea: Waziri mkuu ameishukuru sana idara ya afya NHS kwa kazi nzuri na kuwaomba raia kuendelea kufuata ushauri wa serikali wa kusalia nyumbani, kuwalinda wafanyakazi wa Afya na kuokoa maisha.

Rais wa Marekani Donald Trump alianza mkutano wake na vyombo vya habari kwa kutuma ujumbe wa kumtakia heri njema bwana Johnson katika vita vyake dhidi ya virusi vya corona. ”Wamarekani wote wanamuombea”.

”Ni rafiki yangu mkubwa , mtu muungwana na kiongozi mzuri”, alisema bwana Trump , akiongezea kwamba ana uhakika kwamba waziri huyo mkuu atapona kwa kuwa ni mtu mkakamavu.

Kiongozi wa chama cha Leba Keir Starmer pia alimtakia bwana Johnson heri njema akisema alitumai kwamba atapona haraka.

Dkt. Sarah Jarvis, ambaye ni mtangazaji ,aliambia BBC kwamba bwana Johnson atafanyiwa vipimo kifuani na mapafu yake hususan iwapo amekuwa akipata tatizo la kupumua.

Alisema pia huenda akafanyiwa vipimo vya moyo wake pamoja na vipimo vingine kuhusu kiwango cha oksijeni mwilini na kile cha seli nyeupe za damu , ini na figo kabla ya kutolewa hospitalini.

Bwana Johnson alikuwa akifanya kazi kutoka nyumbani tangu alipotangazwa kwamba amekutwa na virusi vya corona tarehe 27 mwezi Machi.

Alionekana hadharani mara ya mwisho akiwasifu wafanyakazi wa huduma ya Afya na wafanyakazi wengine muhimu katika nyumba yake huko Downing street siku ya Alhamisi jioni kabla ya kuongoza mkutano wa virusi vya corona akiwa karantini siku ya Ijumaa.

Pia siku ya Ijumaa waziri mkuu alichapisha kanda ya video katika mtandao wa twitter ambapo alisema alikuwa akipatwa na dalili chache.

“Bado nina joto mwilini . hivyobasi kulingana na ushauri wa serikali ninafaa kuendelea na karantini hadi pale dalili hizo zitakapopotea”, alisema.

”Hatahivyo tunafanya kazi muda wote ili kuvishinda virusi hivi”.

Siku ya Jumamosi mpenzi wake Carrie Symonds alichapisha ujumbe wa twitter akisema kwamba alikuwa kitandani kwa muda wa wiki moja akiugua dalili za virusi hivyo.

Alisema kwamba hajapimwa virusi hivyo.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents