Diamond Platnumz

Diamond afya kwanza pesa baadaye, pumzika!

Jana kwenye mitandao ya kijamii, website na blogs kulienea picha ya Diamond akiwa kwenye kitanda cha hospitali akiwa na amewekewa vitu vingi kifuani kiasi cha kuifanya picha hiyo aonekane kama amezidiwa sana.
Wengine walihisi pengine msanii huyo alikuwa anaigiza filamu hasa ukizingatia kuwa kampuni ya Step Entertainment Ltd ilidai kuwa tayari imeshazungumza na msanii huyo kufanya filamu naye hivi karibunu.
Picha hiyo ilisababisha maswali mengi kiasi cha watu kumpiga simu kumuuliza kama picha hiyo ni ya kweli ama mchezo tu na kama ni kweli, tatizo ni nini?
“Dah nilikuwa nakohoa sana ikasababisha hadi homa, leo nikaamka nimezidiwa sana mwanangu ndo wakanilaza na ikabidi nifanyiwe vipimo vikubwa. Ndio wakanicheki moyo labda unatatizo, wakanicheki TB na damu pamoja na maradhi mengine wakaona niko poa. Wamesema nilifanya show kwa muda mrefu so nikawa na experience hali ya hewa ya sehemu tofauti tofauti mara kwa mara sometimes vijijini so hali ya hewa vumbi pia imezingua,” ni ujumbe aliomtumia Dj Choka.
Kutokana na maelezo yake, jibu sahihi la tatizo lake tayari ameliweka wazi kuwa ni kufanya show kwa mfululizo.
Hakuna anayebisha kuwa Diamond ndiye msanii wa Bongo Flava mwenye show nyingi zaidi kwa sasa.
Kwa wiki anaweza kufanya show zaidi ya tatu na zote zikimtaka kusafiri kwa muda mrefu, kucheza sana kwenye stage na hivyo kutumia nguvu nyingi.
Kwa wale walioshuhudia show zake, wanafahamu jinsi msanii huyo anavyojituma kwenye stage.
Huo ni uchapakazi wa aina yake ambao hata hivyo unaweza ukamletea matatizo makubwa ya kiafya.
Amefuliliza kufanya show nyingi katika mpishano wa siku chache mno ndani ya kipindi kirefu.
Tunakumbuka mara tu baada ya kufanya show ya Big Brother Africa, Diamond alitweet kwa kusema anahisi anahitaji kupumzika kwa muda sasa.
Tunahisi simu nyingi za mapromota zinazomtaka afanye show zililishinda nguvu hitaji lake la kutaka kupumzika ili kukusanya nguvu.
Na sasa baada ya kufululiza kwa show nyingi zinazotumia nguvu kwenye stage, matokeo yameanza kujitokeza na kama asipozingatia ushauri huu anaweza kupata shida zaidi.
Diamond anahitaji sasa kuipa kipaumbele zaidi afya yake kuliko pesa. Ameshajikusanyia fedha ya kutosha ambayo itamsaidia asiyumbe kwa namna yoyote ile kama akiamua kupumzika kwa kwa mwezi mmoja ama miwili.
Bahati nzuri ni kwamba kwa sasa yupo kwenye mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhan hivyo amejikuta akipumzika, lakini suala hilo anapaswa kulizingatia hata baada ya mfungo.
Bongo5 inamwombea apone kabisa tatizo hilo ili aendelee kuwapa burudani mashabiki wake.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents