Habari

KENYA: Aliyesadikika kuruka kwenye ndege na kupoteza maisha London, akutwa yuko hai gerezani – Video

KENYA: Aliyesadikika kuruka kwenye ndege na kupoteza maisha London, akutwa yuko hai gerezani - Video

Kisa cha kukanganya kuhusu kutambuliwa kwa mtu mmoja aliyeanguka kutoka kwenye ndege ya shirika la Kenya Airways bado kinaendelea.

Mwanaume huyo ambaye picha yake ilionekana katika uchunguzi wa hivi karibuni, mtu huyo aliyejificha ndani ya ndege amebainika kuwa hai, akiwa kwenye gereza la Kenya.

Mamlaka za gereza zimesema kuwa mwanaume huyo ambaye alioneshwa kwenye picha ni Cedric Shivonje Isaac ambaye amekuwa akizuiliwa tangu mwezi Agosti, na si Paul Manyasi, ambaye alitambuliwa katika taarifa ya Sky News.

Uchunguzi wa shirika la habari Sky News wiki hii ulionekana kuthibitisha sura ya mtu huyo. Ripoti ilionesha sura ya mwanaume ambaye Sky News iliambiwa kuwa alifanya kazi kwenye kampuni ya usafi kwenye uwanja wa ndege, na ambaye anadaiwa kujificha kwenye eneo la chini ya gia ya ndege.

Lakini BBC sasa imebaini kuwa mwanaume aliyeonekana kwenye picha hizo yuko hai na amekuwa akishikiliwa na polisi kwa kipindi cha miezi mitatu iliyopita.

Mamlaka za gereza zimethibitisha kuwa jina la mwanaume huyo ambaye alionekana kwenye picha kwenye ripoti ya Sky News ni Cedric Shivonje Isaac. Baba wa mwanaume huyo amekana kauli yake alipozungumza na mtangazaji , na sasa anasisitiza mtoto wake bado yu hai.

Haijajulikana mkanganyiko huu umetokea vipi, wapelelezi wanajaribu kutafuta uwezekano kati ya bwana Isaac, mtu aliye kwenye picha na bwana Manyasi, mwanaume aliyetambuliwa kwenye ripoti.

Taarifa hii imezua maswali mapya kuhusu uwezo wa mamlaka za Kenya kumbaini mtu aliyeingia ndani ya ndege hiyo, ikiwa miezi minne tangu alipoanguka kutoka kwenye ndege ya Kenya Airways kuelekea kwenye uwanja wa ndege wa Heathrow jijini London.

 

Paul Manyasi ni nani?

Sky News wanasema walipata kidokezo cha kwanza kutoka kwa dereva wa teksi za Uber kwa jina Kamau aliyewajulisha kwamba yupo mfanyakazi wa kampuni ya kufanya usafi ya Colnet aliyetoweka kipindi hicho. Alisema baadhi ya wafanyakazi walizungumzia kutoweka kwa mfanyakazi huyo.

Baadaye walikutana na mwanamke mfanyakazi wa Colnet ambaye hakutaka kutambuliwa, ambaye aliwaambia kwamba mwenzake kwa jina Paul Manyasi alitoweka mwishoni mwa Juni.

“Mara ya mwisho kumuona, tulikuwa kazini, ghafla akatoweka, hakuna ajuaye alikoenda,” mwanamke huyo aliwaambia waandishi hao.

Anasema mkubwa wao kazini aliwaambia asubuhi iliyofuata kwamba yupo mtu aliyekuwa ametoweka lakini hawakuwa wanajua ni nani hasa na kwamba hilo lilifaa kuwekwa siri.

Mwanamke huyo alikuwa na picha za Paul na alisema walikuwa na uhusiano wa miaka miwili na walikuwa na mpango wa kuoana wakati mmoja.

Paul alikuwa anaishi mtaa wa Mukuru kwa Njenga pamoja na rafiki yake kwa jina Patrick ambaye ndiye aliyemsaidia Paul kupata kazi Colnet. Wawili hao wanatokea jimbo moja Kakamega.

Patrick anasema Paul alikuwa na ndoto ya kuondoka Kenya lakini hakuwahi kufichua alitaka kwenda wapi na ni kazi gani angeenda kuifanya.

By Ally Juma.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents