Bongo5 Makala

Makala: Kiki, kipaji duni, kuikosoa WCB, shobo kwa Alikiba ndio kaburi la Harmorapa kimuziki (+Audio)

March 23, 2017 jina la msanii Harmorapa liliteka ghafla mitandao ya kijamii na vyombo vya habari. Ni baada ya kutokea katika mkutano wa aliyekuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye na waandishi wa habari.

Bila shaka unakumbuka katika mkutano huo kulitokea tukio la Mhe. Nape kutishiwa na bastola ambapo Harmorapa alitimua mbio kama Usain Bolt. Baada ya mbio zake hata wale ambao walikuwa hawamjui waliweza kumjua.

Kwanini Harmorapa

Licha ya Harmorapa kupata umaarufu mkubwa nje ya muziki lakini ni wazi ameshindwa kutumia umaarufu huo kwa upande wa muziki wake na hatimaye sasa hasikiki kabisa, hata matukio yake nje ya muziki hayana nguvu tena kama ilivyokuwa hapo awali.

Ni zaidi ya miezi saba Harmorapa hajatoa wimbo wowote, mara ya mwisho kutoa wimbo ilikuwa ni August 24, 2017 ambapo alitoa wimbo unaokwenda kwa jina la Ajitokeze.

Swali la kujiuliza ni kwanini kijana huyu aliyetokea kupendwa ghafla hasikiki tena?. Napenda kuangazia mambo kadhaa ambayo yanaweza kuwa sababu ya kupotea kwake.

1. Kiki, Kibaji Duni

Ukweli uliopo na ambao utaendelea kuishi miaka yote ni kwamba Harmorapa hajawahi kupendwa kutokana na muziki wake bali vituko vyake. Huyo ni mwanamuziki na sio mchekeshaji, hivyo utaona bidhaa aliyokuwa anauza inapishana na wateja wake.

March mwaka jana wakati anagonga vichwa vya habari kupitia tukio la Mhe. Nape alikuwa ameshatoa ngoma mbili ambazo ni Usigawe Pasi na Kiboko ya Mabishoo. Watu walitarajia baada ya tukio hilo ngoma ambazo zingefuata zingefanya vizuri lakini ikawa ndivyo sivyo.

Ngoma aliyofanya na C Pwaa ‘Nundu’ pamoja Ronia iliyotoka May 08, 2017 haikufanya vizuri kama ile aliyofanya na Juma Nature ‘Kiboko ya Mabishoo. Baada ya hapo hajaweza kutoa ngoma nyingine kubwa kwa upande wake hata hiyo ya mwisho kutoa hadi sasa zaidi ya miezi saba haina video kitu ambacho si kizuri kwa msanii anayechipukia.

Utakumbuka kabla ya tukio la Mhe. Nape, Harmorapa aligonga vichwa vya habari hasa mtandaoni mara baada ya kujitokeza hadharani na kudai ana mpango wa kumuoa Wema Sepetu.

Wema Sepetu huyu aliyekuwa Miss Tanzania mwaka 2006 aolewe na kijana aliyekuja mjini hivi karibu?, ilikuwa ni stori ya aina yake iliyomfaa kila mwandishi wa habari za burudani hasa wale wa udaku.

Kipindi anaweka wazi dhamira yake hiyo ndio kipindi ambacho alikuwa ametoa nyimbo mbili za mwanzo, hata hivyo dhamira yake ilikuwa na nguvu katika vyombo vya habari na mitandao kuliko muziki wake.

Katika matukio yake mawii aliyoyatengeneza kulikuwa nafasi ya yeye kutoa muziki mzuri na watu wakaupokea. Tukubaliane kuwa kuna baadhi ya wasanii hutengeneza matukio ‘kiki’ na siku chache mbeleni wanatoa nyimbo na zinafanya vizuri.

Hilo kwa Harmorapa linaonekana kutofanya kazi kabisa, naweza kusema ni kutokana na kipaji chake kutokuwa cha kiwango hicho, yaani ni butu.

Alijikita katika kutengeneza matukio kuliko muziki, utakumbuka kuna kipindi zilisambaa picha mtandaoni akiwa na Amber Lulu aliyedai kuwa ni mpenzi wake lakini hata hivyo ilikuja kubainika hawakuwa wapenzi na hata project waliyoeleza kuwa ingetoka hadi leo haijaonekana.

3. Kuikosoa WCB, Shobo kwa Alikiba

Kwa mujibu wa Producer Mr. T Touch wakati Harmorapa anaenda studio kwake kwa ajili ya kuingia rasmi katika muziki alikuwa akitumia jina la Jembe la Kusini. Baadaye kutokana na kufanana kwa mbali na msanii kutoka WCB, Harmonize ndipo likazaliwa jina la Harmorapa.

Hata hivyo Producer mkongwe, P Funk Majani alimuonya kuhusu kutumia jina hilo kwa kueleza kuwa kitendo hicho kingemnufaisha zaidi Harmonize.

“Nilimshawishi kabisa toa jina hilo tumia jina lako mwenyewe, hajanijibu vizuri. Sasa hivi utakuwa unampa yeye kiki,” P Funk aliiambia FNL ya EATV.

Kitendo cha kuanza kutumia jina Harmorapa kilimfanya baadhi ya mashabiki hasa wa Harmonize na WCB kutompenda. Siku zilivyozidi kwenda akajikuta katika vita ya maneno na Dansa wa Diamond Planumz, Mose Iyobo.

Katika ngoma yake inayokwenda kwa jina la Kiboko ya Mabishoo anaamua kumchana kabisa Mose Iyobo. Harmorapa anasema kuwa; Tulikuwa Wasafi kabla ya WCB, maneno yao machafu hayanivunji CV.

August 04, 2017 katika mahojianao na Tricod skills, Harmorapa alisema kati ya vitu asivyopenda katika maisha yake ni kuizungumzia label ya WCB kwani ana vitu vingi vya kuzungumza nje ya label hiyo.

“Hili swali linajirudia kama matangazo ya vifo lakini kiufupi nishawahi kusema siwezi kufanya na msanii yeyote kutoka WCB,” alisema

Akiendelea na mahojiano hayo alieleza kuwa kiu yake ni kufanya kazi na Alikiba kwani ndiye msanii anayemkubali zaidi kutoka Bongo na mikakati ya kufanya kolabo hiyo ipo tayari.

“Niseme msanii bora kwangu ni King Kiba, kiukweli sijui nisemaje katika kile kiwango chake cha uimbaji wake, umaridadi wake, performance ndio kitu kinachonivutia,” alieleza.

Wakati anatoa kauli hiyo ilikuwa ni miezi michache imepita tangu agonge vichwa vya habari mara baada ya kwenda kumpokea Alikiba Air Port akitokea Afrika Kusini alikokuwa ameshinda Tuzo ya MTV EMA, 2016.

Katika mapokezi hayo Harmorapa alitengeneza tukio la aina yake pale alipompigia Alikiba magoti na kumkabidhi zawadi ya tisheti. Hata hivyo Alikiba hakuwa na muda wa kuzungumza naye.

Anguko la Harmorapa

Ukiacha sababu mbili nilizozitaja hapo awali, sote tunafahamu kuwa Alikiba na Diamond/WCB ni kambi mbili zenye mashabiki wengi ambao ni washindani kimuziki. Hivyo Harmorapa alitaka kutumia uchochoro huo ili kufanikisha mipango yake kimuziki.

Harmorapa alikuwa akionyesha jitihada kubwa kwa kujipambanua kuwa yeye ni team Kiba lakini Alikiba mwenye hakuwa na muda naye. Katika moja ya interview Alikiba aliwahi kuulizwa kuhusu kolabo na Harmorapa hakujibu chochote zaidi ya kucheka na kuondoka.

Hivyo kwa upande wa team Kiba alipotegemea kuwa ni kambi yake hakupata chochote na upande wa pili tayari alishakuwa hana maelewano nao mazuri, hivyo akabakiwa na mashabiki wanaopenda kiki na vituko vyake na sio wale wa muziki ambao kwa asilimia kubwa wapo pande hizo mbili.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents