Siasa

Mgodi wa Mererani wafungwa

MereraniSerikali imesimamisha uchimbaji wa Tanzanite katika migodi ya Mererani iliyoko mkoani Manyara huku kukiwa na hofu kuwa idadi ya walikufa ndani ya mashimo migodini ni kubwa kuliko ile iliyotangazwa

Mererani

 

 

 

Na Adam Ihucha, Mererani na Charles Ngereza, PST Arusha

 

 

 
Serikali imesimamisha uchimbaji wa Tanzanite katika migodi ya Mererani iliyoko mkoani Manyara huku kukiwa na hofu kuwa idadi ya walikufa ndani ya mashimo migodini ni kubwa kuliko ile iliyotangazwa.

 

 

 

Migodi hiyo imefungwa kwa muda usiojulikana kufuatia mafuriko yaliyoua wachimbaji wadogo zaidi ya 70 mwishoni mwa wiki.

 

 

 

Kadhalika serikali, imeunda kamati ya kuokoa na kusaka miili ya wachimbaji wadogo itakayoongozwa na Mkuu wa Operesheni wa Jeshi la Polisi, Bw. Venance Tossi.

 

 

 

Waziri wa Nishati na Madini Bw. William Ngeleja, alisema jana na kuongeza kuwa amri hiyo inaihusu pia migodi ya kampuni ya wawekezaji kutoka Afrika Kusini ya Tanzanite One.

 

 

 

Akizungumza jana na wachimabaji wadogo katika kituo cha polisi Mererani Waziri alisema sababu za kusimamisha uchimbaji ni kutoa nafasi kwa wachimbaji wadogo kusaidia kutafuta miiili ya wenzao wanaohofiwa kufa.

 

 

 

“Kazi ya uchimbaji itasimama kwa muda usiojulikana kwa migodi yote katika vitalu B, C na D hadi hapo kazi ya kutafuta miili ya wenzetu itakapokamilika,“ alisema Waziri Ngeleja.

 

 

 

Wachimbaji hao zaidi ya 70 walikufa baada ya mashimo yao kujaa maji na pia juhudi za ukoaji kukwama kufuatia kukosekana vifaa vya kisasa na miundo mbinu ya uokoaji.

 

 

 

Waziri wa Madini alitangaza kusimamishwa shughuli hizo akiwa pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Bw. Henry Shekifu, pamoja na Mawaziri wa Mambo ya Ndani Bw. Lawrence Masha na Bw. Phillip Marmo wa Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Bunge, Sera na Uratibu.

 

Waziri wa Mambo ya Ndani Bw. Lawrence Masha
[Waziri wa Mambo ya Ndani Bw. Lawrence Masha]

 

 

 

Kamati hiyo maalumu ya kutafuta miili inaongozwa na Kamanda Venance Tossi na kwamba waopoaji kutoka Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) Brigedi ya Kaskazi na wa kampuni ya kuchimba dhahabu ya Barrick Gold kutoka mkoani Mara wamefika Mererani tayari kwa kazi.

 

 

 

Wajumbe wa kamati hiyo kwa mujibu wa Mkuu wa Mkoa ni 10 nao ni pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro Bw. Khalid Mandia , Mwenyekiti na Katibu wake ni Ofisa Madini Kanda ya Kaskazini Bw.John Nayopa.

 

 

 

Wajumbe wengine ni pamoja na Ofisa Usalama wa Mkoa wa Manyara, mbunge wa Siamaniiro Bw. Chiristopher ole Sendeka, mbunge wa viti maalumu Dora Mushi, Mwenyekiti wachimbaji kitalu B, Zephania Joseph, Mwenyekiti wa kitalu D, Philip Mkenga na wachimbaji wengine watatu.

 

 

 

Alisema kazi ya kamati hiyo ni kusimamia kazi ya utafutaji miili na uokoaji pamoja na kuhakikisha kuwa zana na nyenzo muhimu zinapatikana kufanikisha zoezi hilo.

 

 

 

Akizungumzia miili alisema mingine iliyoopolewa zaidi ya wachimbaji watano waliopatikana juzi kutokana na kazi hiyo kuwa ngumu.

 

 

 

Alisema uchunguzi uliofanywa na kamati ya ulinzi na usalama ya mkoani Manyara ulionyesha kuwa wachimbaji waliozama siku ya tukio walikuwa 166.

 

 

 

Alisema miongoni mwao 93 waliokolewa na 67 wanahofiwa kufa ndani ya mashimo hayo.

 

 

 

Wakati serikali ikijipanga kufanya kazi ya kuopoa miili ya wachimbaji hao, tayari kuna taarifa kuwa idadi kubwa ya wachimabji wadogo huenda wamekwama kutoka katika mpaka wa kitalu `B` na `C` ambapo mashimo yanaungana chini ya ardhi kwa lugha ya wachimba huitwa `mitobozano`.

 

 

 

Hata hivyo, baadhi ya ndugu na marafiki wa watu wanaohofiwa kufa katika tukio hilo waliofika kwenye machimbo hayo wameonyesha wasiwasi wa miili ya jamaa zao kama itapatikana kutokana na uopoaji kusuasua.

 

 

 

Mmoja wa watu hao aliyejitambulisha kwa jina la Rashid Iman alisema anashangazwa na namna taratibu za kusaka miili hiyo zilivyofanyika akidai kuwa serikali ina uwezo wa kutoa msaada kwa haraka hata kama ingeshindwa ingeomba kutoka nje ya nchi.

 

 

 

Hata hivyo, habari zaidi zilisema kuwa shughuli ya uokoaji inakwamishwa pia na kukatika kwa umeme baada ya mafuriko kuangusha nguzo za umeme.

 

 

 

Mvua hizo zilizonyesha sehemu nyingine za Afrika Mashariki zimeharibu maisha, makazi, mali na mazao mashambani.

 

 

 

Hii ni ajali ya pili kubwa kutokea katika migodi ya Tanzanite ambapo mwaka 1998 wachimbaji zaidi ya 100 waliangamia kutokana na mafuriko ya mvua za El-nino.

 

 

 

Mererani ni sehemu pekee duniani ambapo kito hiki chenye thamani, Tanzanite, hupatikana .

 

 

 

Wachimbaji wadogo wamekuwa wakifa kwenye milipuko ya baruti machimboni na kufukiwa na vifusi, wengine wanakosa hewa mashimoni ambaapo mwaka 2002 wachimbaji 48 walikufa baada ya mashine ya kusafisha hewa kuzimika.

 

 

 

Wakati huo huo, Rais Jakaya Kikwete, amemtumia salamu za pole Mkuu wa Mkoa wa Mkoa wa Manyara kutokana na maafa makubwa yaliyowapata wachimbaji madini katika machimbo ya Tanzanite ya Mererani, Wilayani Simanjiro, mkoani humo.

 

 

 

Taarifa iliyotolewa jana na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Ikulu, ilisema Rais amepokea kwa masikitiko, huzuni na mshtuko mkubwa taarifa ya janga hilo kubwa.

 

 

 
Ilisema Rais Kikwete amehuzunishwa na upotevu wa maisha ya watu ambao mpaka sasa imethibitika kuwa wamekufa, yaliyosababishwa na kujaa kwa maji katika mashimo ya machimbo hayo kutokana na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha.

 

 

 

Rais pia aliwaombea wachimbaji ambao taarifa zao hazijathibitika waweze kupatikana haraka wakiwa hai na salama.

 

 

 

Pia aliwaombea wote walioumia katika ajali hiyo kupona haraka.

 

 

 

Rais anatoa pole kwa familia ambazo zimeathirika na janga hilo na kuzihakikishia kuwa, yuko pamoja nao katika wakati huu wa majonzi na huzuni.

 

 

 

Wakati huo huo, Waziri Mkuu, Bw. Mizengo Pinda, amewaagiza Mawaziri watatu kwenda mara moja Mererani mkoani Manyara kutathimi maafa ya mafuriko yaliyosababisha vifo katika machimbo ya Tanzanite.

 

 

 

Walioagizwa kwenda Manyara ni Mawaziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Bw. Philip Marmo, Nishati na Madini Bw. William Ngeleja na Mambo ya Ndani, Bw. Lawrence Masha.

 

 

 

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu, jijini Dar es Salaam, Bw. Pinda ambaye yuko mkoani Mara kwa vikao vya CCM aliwataka mawaziri hao kutathimini hali ilivyo na kutoa taarifa kwa serikali ili ichukue hatua za haraka za kukabiliana na hali hiyo.

 

 

 

Waziri Mkuu alisema serikali inafuatilia kwa karibu tukio hilo na inawapa pole jamaa wa marehemu na wote walioathiriwa na maafa hayo.

 

 

 

Source: Nipashe

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents