Habari

Mkulima aliyechomwa mkuki arejea nyumbani

Wiki iliyopita kulikuwa na habari iliyowashtua watu kwa namna moja au nyingine. Ni habari ya mkulima na mkazi wa kitongoji cha Upangwani, kijiji cha Dodoma Isanga, Kata ya Masanze, Kilosa mkoani Morogoro ,Augustino Mtitu(35), aliyechomwa mkuki mdomoni. Hatimaye kijana huyo ameruhusiwa kutoka hospitali alikokuwa amelazwa na kurejea nyumbani.

Madaktari wamesema kuruhusiwa kwa mgonjwa huyo kumetokana na yeye kupona kufuatia kufanyiwa upasuaji mkubwa mara baada ya kupata mkasa huo. Tukio hilo lililotokea majira ya saa tano asubuhi mwishoni mwa mwaka jana wakati alipokuwa shambani kuzuia vurugu zilizokuwa zimetokea baada ya wafugaji wa jamii ya kimasai kulisha mifugo yao kwenye shamba la maharage na mahindi yaliyopo katika kijiji hicho.

Akizungumza na mwandishi wa habari Jumatatu hii, Mganga mkuu wa mkoa wa Morogoro, Dk Frank Jacob, alisema kuwa Mtitu ambaye alilazwa wodi namba moja ya wagonjwa wa majeruhi wa ajali katika hospitali hiyo tangu Disemba 25 mwaka jana aliruhusiwa kutoka hospitalini hapo kwenda nyumbani baada ya kupona jeraha lilolotokana na mkuki na kufanyiwa upasuaji mkubwa.

Hata hivyo, Dk Jacob alimshukuru Mungu na madaktari, wauguzi kuwezesha kufanikisha upasuaji wa mgonjwa huyo uliofanikisha kuondolewa kwa mkuki aliochomwa mdomoni na kutokea upande wa shingoni .

Kwa upande wake Mtitu, alimshukuru Mungu, madaktari, uongozi wa halmashauri ya wilaya ya Kilosa na wananchi wa kijiji hicho kwa kuwezesha kunusuru maisha yake.

BY: EMMY MWAIPOPO

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents