Rais mpya Malawi, Lazarus Chakwera aapishwa
Rais mpya wa Malawi Mhe.Lazarus Chakwera ameapishwa hii leo huku hafla ya kuapishwa kwake ikifanyika katika mji mkuu wa Lilongwe baada ya kiongozi huyo kushinda katika uchaguzi wa marudio uliofanyika nchini humo.
Lazarus Chakwera ameshinda uchaguzi wa wiki hii wa rais ulioamriwa kufanyika tena kwa asilimia 58.57 ya kura, tume ya uchaguzi ya nchi hiyo imesema.
Ilikuwa ni mabadiliko makubwa ya majaaliwa kwa kiongozi aliyeko madarakani, Peter Mutharika, ambaye ushindi wake katika uchaguzi wa mwezi Mei 2019 ulibatilishwa na mahakama ya katiba, yakihusishwa na udanganyifu mkubwa.
Kiasi ya wapiga kura milioni 6.8 katika taifa hilo dogo la kusini mwa Afrika walijitokeza katika vituo vya kupigia kura siku ya Junanne. Na jana Jumamosi , tume ya mwenyekiti wa tume ya uchaguzi Chifundo Kachale aliwaambia waandishi habari; “Tume imemtangaza Lazarus Chakwera , kwa kupata asilimia 58.57 ya kura, kuwa amechaguliwa kuwa rais wa Malawi.
Mutharika alikuwa wa pili kwa kupata kura 1,751,377, wakati mgombea ambaye hajulikani sana Peter Dominico Kuwani amepata kuwa 32,456.
Watu waliojitokeza kupiga kura ni asilimia 64.81.
Tangazo hilo lilipokelewa kwa shangwe kubwa na vigelegele wakati waungaji mkono upinzani wakipepea bendera ya Malawi yenye rangi nyekundu , nyeusi na kijani na kuimba “serikali” katika lugha ya Kichechewa.
Mwezi Februari , mahakama ya juu ya Malawi iliona kuwa uchaguzi wa kwanza umegubikwa na mapungufu mengi , ikiwa ni pamoja na matumizi ya wino wa kufanyia marekebisho kubadilisha matokeo katika karatasi ya matokeo.