Michezo

Ripoti: Kampuni za Ujerumani zahusishwa kutuma kemikali Syria

Ripoti imedhihirisha kuwa licha ya vikwazo vya Umoja wa Ulaya kampuni za Ujerumani zilituma kemikali Syria. Kemikali hizo zinaweza kutumika kutengeneza gesi ya sarin ambayo ilitumiwa dhidi ya raia katika vita vya Syria.

Chemiewaffen Inspektoren in Syrien (picture alliance/AP Photo)

Kwa mujibu wa shirika la habari la DW Kampuni za Ujerumani zinahusishwa katika kuiuzia Syria kemikali za kutengeneza silaha wakati taifa hilo likiwa katikati ya vita, licha ya vikwazo vilivyowekwa na Umoja wa Ulaya. Taarifa hizo ni kulingana na ripoti iliyotolewa Jumanne na kuchapishwa na gazeti la Ujerumani la Süddeutsche Zeitung, kituo cha utangazaji cha Bayerischer Rundfunk pamoja na kundi la vyombo vya habari la Uswisi Tamedia.

Ripoti hiyo imesema kampuni ya kemikali ya Ujerumani ya mauzo ya jumla Brenntag AG, iliiuzia Syria kemikali za isopropanol na diethylamine mnamo mwaka 2014 kupitia kampuni nyingine ndogo ya Uswisi. Kemikali hizo ziliuziwa kampuni ya Syria ya kutengeneza madawa ambayo ina uhusiano wa karibu na serikali ya Bashar al-Assad. Ingawa kemikali hizo zinatumika kutengeneza dawa za kawaida, zinaweza pia kutumika katika kutengeneza silaha za kemikali.

Maripota wamedhihirisha kwamba diethylamine ilitengenezwa na kampuni kubwa ya kemikali nchini Ujerumani BASF katika kiwanda chake cha mjini Antwerp, Ubelgiji. Na isopropanol ilitengenezwa katika kampuni ya mjini Hamburg Ujerumani ya Sasol Solvents.

Gazeti la Süddeutsche Zeitung limesema kampuni ya Brenntag AG imethibitisha kwamba usafirishaji wa kemikali hizo hadi Syria ulishughulikiwa na kampuni ndogo ya Uswisi, ambayo ilifuata sheria za wakati huo.

Belgien BASF Chemifabrik in Antwerpen (Imago Images/Alimdi/Arterra)Kiwanda cha BASF mjini Antwerp, Ubelgiji

Sheria za Umoja wa Ulaya zilikiukwa

Kufuatia ripoti kadhaa zinazohusu serikali ya Assad kutumia silaha za kemikali dhidi ya raia wake katika vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Syria, Umoja wa Ulaya uliweka vikwazo vya kusafirisha kemikali za kutengezea silaha.

Ruhusa rasmi imekuwa ikihitajika kusafirisha kemikali ya diethlamine kuanzia mwaka 2012, na kwa isopropanol tangu mwaka 2013. Sheria hizo hazilengi tu usafirishaji wa moja kwa moja hadi Syria lakini pia mauzo yasiyo ya moja kwa moja kupitia nchi kama Uswisi.

Ofisi ya Shirikisho ya Uchumi na Udhibiti wa Mauzo ya Nje, ambayo inawajibu wa kuidhinisha bidhaa hizo, imesema kuwa haikutoa vibali vyovyote kwa kemikali hizo hadi hii leo.

Kuhusika kwa makampuni ya Ujerumani katika mikataba ya kuuza nje ya nchi kemikali hizo mnamo mwaka 2014 kunaleta utata mkubwa hasa ikizingatiwa kwamba hazina za silaha za kemikali za Syria ziliharibiwa katika hatua iliyoratibiwa kimataifa mwaka huo huo.

Waendesha mashtaka katika mji wa Ujerumani wa Essen iliko kampuni ya Brenntag AG, wamesema wameanzisha mchakato wa kisheria na wanatafakari kufungua uchunguzi rasmi. Waendesha mashtaka wa nchini Ubelgiji pia wamesema wanachukua hatua sawa na hizo.

Chanzo: DW

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents