Habari

Serikali: Tunawashusha vyeo viongozi wazembe kwa kuzingatia kanuni

Serikali imesema masuala mazima ya nidhamu, ajira na upandishwaji vyeo yanaongozwa na kanuni, sheria na taratibu huku ikisema kuwa kama kuna mfanyakazi wa umma aliyewahi kuonewa awasilishe malalamiko yake.

Kauli hiyo imekuja baada Mbunge wa Ukonga, Mwita Waitara kuuliza Je, Nini kauli ya Waziri wa utumishi kwa wale watumishi ambao wanashushwa vyeo wanadhalilishwa na kutukanwa na viongozi hasa Wakuu wa Wilaya na Mikoa?

Swali hili lilijiwabiwa na Waziri Angella Kairuki na Waziri wa Tamisemi, George Simbachawene.

Mheshimiwa Kairiku alisema, “Masuala mazima ya nidhamu, masuala mazima ya ajira pamoja na upandishwaji wa vyeo na kushushwa vyeo yanaongozwa kwa kanuni sheria na taratibu, naomba niseme kwamba kama kuna ambaye anaona kanuni hazikufuatwa tuweze kupata taarifa ili tuweze kufuatilia. Lakini tumetoa miongozo mbalimbali pamoja na watendaji kuhakikisha kwamba wanazingazia sheria za umma, wanazingatia kanuni za kudumu za utumishi wa umma pamoja na kanuni za utumishi wa umma, kwahiyo naomba niseme kama kuna mtumishi ambaye hakutendewa haki basi awasilishe malalamiko yake”.

Kwa upande wake waziri Simbachawene aliweza kujibu swali hili akisema, “Ni kweli kumekuwa na hatua mbalimbali zilizochukuliwa na wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya kutokana na watumishi wazembe, namtambue kwanza katika ilani yetu ya chama cha mapinduzi tulisema kwamba kwa watumishi wazembe hatutakubali kuendelea nao, nataka nichukue nafasi hii kusema kwamba wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya wamegawiwa maeneo yao ya utawala na wanasimamia masuala yote, lakini wanasimamia yote kwa mujibu wa sheria. Hiwezekani unapewa pesa ya basket fund wewe ni DMO halafu huzitumii na watu wanakosa huduma, tumefanya utafiti katika mikoa minne ziko hela nyingi katika halmashauri hazitumiki wanataka kuzifanyia nini na mnasema tusichukue hatua haiwezekani!”

Aliongeza, “Haiwezekani unapewa shule una walimu zaidi ya 15 pamoja na changamoto zilizopo ambazo ni haki zao kuzidai lakini si sababu ya wao kutotimiza wajibu wao, nataka tu kusema wakuu wa mikoa wanayo haki ya kisheria kuchukua hatua kwa mtumishi yeyote awe mkuu wa shule, kwa mfano uteuzi wa mkuu wa shule unateuliwa na RAS ambaye ndiye katibu wa mkuu wa mkoa.”

Na Emmy Mwaipopo

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents