Siasa

Somalia: Rais wa zamani aliyeshindwa uchaguzi 2017, Hassan Sheikh Mohamud ashinda urais

Rais wa zamani wa Somalia aliyeshindwa katika uchaguzi wa 2017 amerejea madarakani baada ya kumpiku rais wa sasa, katika kinyang’anyiro cha muda mrefu kilichoamuliwa na wabunge katika duru ya tatu ya upigaji kura.

Hassan Sheikh Mohamud, aliyehudumu kama rais wa Somalia kati ya mwaka wa 2012 na 2017, alishinda uchaguzi huo katika mji mkuu Mogadishu, wakati kukiwa na ulinzi mkali uliowekwa na mamlaka ili kuzuia mashambulizi makali ya wanamgambo wa itikadi kali.

“Linapokuja suala la chuki za aina yoyote, niko tayari kuzitatua, kama tu nilivyosema wakati natangaza kugombea urais mwanzoni mwa wiki hii. Hakuna kisasi wala ufuatiliaji wa kisiasa unaomlenga mtu yeyote. Nchi hii ina kanuni na sheria za kutosha na kama tofauti zozote zikitokea, tutapitia sheria zilizotungwa na nchi hii.” Amesema Mohamud.

Ushindi ni wa watu wa Somalia

Amesema ushindi huo ni watu wa Somalia, na huo ni mwanzo wa enzi ya umoja, demokrasia ya Somalia na mwanuzo wa vita dhidi ya rushwa. Aliongeza kuwa anaona kazi ngumu mbele baada ya kushinda urais.

Duru ya kwanza ya upigaji kura ilikuwa na wagombea 36, ambapo wane walisonga hadi duru ya pili. Baada ya kukosekana mshindi aliyepata angalau theluthi mbili ya kura 328, upigaji kura kisha ukaingia katika duru ya tatu ambapo ushindi wa zaidi ya nusu ya kura ulitosha kumchagua mshindi.

Wajumbe wa mabaraza mawili ya bunge walimchagua rais katika kura ya siri iliyopigwa ndani ya katika uwanja wa ndege wa kambi ya jeshi ya Halane, ambayo inalindwa na walinda amani wa Umoja wa Afrika.

Kuchaguliwa kwa Mohamud kumekamilisha mchakato wa uchaguzi uliocheleweshwa kwa muda mrefu ambao uliibua mivutano ya kisiasa na ongezeko la wasiwasi wa ukosefu wa usalama, baada ya muhula wa Rais Mohamed Abdullahi Mohamed kumalizika Februari 2021 bila kuwepo na mrithi wake.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents