Habari

TCRA yaonya kuhusu maudhui yenye utata kuhusu dini

Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA)
imeonya kuchukua hatua kali za kisheria kwa chombo chochote cha utangazaji kitakachobainika kurusha taarifa zenye maudhui ya kufikirika ambayo yanaleta utata kuhusu imani za kidini.

Taarifa ya TCRA iliyotolewa na Mkurugenzi Mkuu wa TCRA Dkt. Jabiri Kuwe
imesema, masuala yanayohusu imani za dini ni binafsi, hivyo mahali sahihi pa kuyazungumzia ni kwenye nyumba za Ibada na sio kwenye vyombo vya habari na utangazaji.

Taarifa hiyo imesisitiza kuwa vyombo vya habari na utangazaji vina wajibu wa kufuata misingi na maadili ya taaluma zao kwa kutoa taarifa zilizofanyiwa uchambuzi, za kuaminika na za kweli.

Hii ni pamoja na kutoa taarifa kwa kufuata sheria, kanuni, miongozo na maadili katika kutoa huduma ya utangazaji.

TCRA imetoa taarifa hiyo
kufuatia hivi karibuni kuwepo kwa mfululizo wa taarifa fupi zilizo kwenye mfumo wa video zinazozungumzia masuala yanayohusu mawazo fikirika yanayogusa imani za kidini.

Kwa mujibu wa TCRA, mawazo hayo yamekuwa yakitolewa kwenye vyombo mbalimbali vya utangazaji ikiwa ni pamoja na redio na televisheni, vyombo vya utangazaji vya mitandaoni na kwenye makundi ya mitandao ya kijamii.

“Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania inakemea vikali hali hii ya taarifa za mawazo ya kufikirika, na yenye utata kuhusu imani za kidini ambazo zinaendelea kushamiri kwenye vyombo vya utangazaji vya mitandaoni na vile vya redio na runinga za kawaida (traditional media) na inaagiza kuacha mara moja kurusha maudhui yeyote ya kufikirika ambayo yanaleta utata kuhusu imani za kidini kwenye jamii.” Imeeleza taarifa hiyo ya Dkt. Kuwe

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents