Habari

Trafiki wawili wauawa Kibiti

Askari Polisi wawili wa Kikosi cha Usalama Barabarani wilayani Kibiti, mkoani Pwani wameuawa kwa kupigwa risasi na watu wasiojulikana katika Kijiji cha Msafiri, Kata ya Bungu wakiwa kazini.

Mbali na kupigwa risasi, pia watu hao wamechoma moto gari moja na pikipiki moja za askari hao kisha kutokomea kusikojulikana. Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Onesmo Lyanga alithibitisha mauaji hayo. Kwa mujibu wa taarifa kutoka Kibiti, trafiki hao waliouawa wametambuliwa kwa majina ya Sajini Salum na Konstebo Masola.

Inadaiwa askari mwingine alinusurika katika shambulio la jana mchana. Tukio hilo lilitokea kilometa chache kutoka walikouawa askari polisi wanane kwa kupigwa risasi. Askari hao wanane waliuawa katika eneo la Mkengeni walipokuwa wakitoka doria Kijiji cha Jaribu.

Ndani ya wiki tatu, watu sita wameuawa Kibiti na Rufiji huku mmoja akinusurika kifo kwa kupigwa risasi ya kichwa. Kumekuwapo na matukio ya mauaji katika wilaya za Kibiti na Rufiji katika siku za karibuni na hakuna sababu hasa za mauaji hayo ambayo yamelaaniwa kila pembe.

Akihutubia wananchi mjini Kibaha juzi katika siku ya kwanza ya ziara yake mkoani Pwani, Rais John Magufuli aliwataka wananchi wa wilaya hizo waache kuwaficha wahalifu kwa sababu wanawajua, ili wasiendelee kurudisha nyuma maendeleo yao.

Alisema ikiwa hawatatoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi ili kumaliza uhalifu na mauaji kwenye maeneo hayo, watakuwa wanarudisha nyuma maendeleo yao wao wenyewe.

Na Emmy Mwaipopo

Chanzo: Habarileo

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents