Burudani

Uchambuzi: Show ya Wizkid, Diamond, Christian Bella na Fid Q ilikuwa moto wa kuotea mbali, soma yaliyojiri

Wakati watanzania wakimaliza salama uchaguzi mkuu October 25 huku wakisubiria kuapishwa kwa rais mteule, Dr John Pombe Magufuli baada ya kuibuka kudedea, weekend iliyopita wapenzi wa muziki wa Dar es Salaam, walipata burudani ya kukata na shoka kutoka kwa msanii wa Nigeria, Wizkid aliyesindikizwa na Diamond, Christian Bella na Fid Q.

Wizkid akiwa karibu na mashabiki wake

Wizkid ambaye alitua kwa mara ya kwanza nchini Tanzania baada ya kuletwa na kampuni ya burudani, King Solamon alipata mapokezi yaliyomfanya ajisikie yupo nyumbani.

JINSI SHOW ILIVYOKUWA

Show ilichelewa kuanza kama ilivyodaiwa lakini nadhani ni kutokana na idadi chache ya watu waliojitokeza ukilinganisha na ukubwa wa wasanii hao.

Hata hivyo hali hiyo walijaribu kui-fix baada ya Dj Sinyorita na Ommy Crazy kutoa burudani kali, huku MC wa show hiyo T-Bway pamoja na Anna Peter wa East Africa TV/Radio wakijaribu kuwaongezea mzuka mashabiki wa muziki waliojitokeza.

Fid Q katika ubora wake

FID Q

Rapper Fareed Kubanda aka Fid Q ambaye alikuwa msanii wa kwanza kufungua show, bado anaendelea kuonyesha maboresho makubwa katika show zake hususan katika kutumbuiza live.

Ngosha alifanya vizuri sana hasa jinsi alivyojaribu kui-interact na mashabiki wake. Alishauri mara kadhaa bendi yake kupiga muziki taratibu kwa kuwa show hiyo ilikuwa ya wasanii wanne na kila mmoja alihitaji muda wa kutosha kwaajili ya mashabiki wake.

Kauli hiyo iliwafanya mashabiki wa muziki wake kuendelea kusikiliza muziki wake kwa makini bila shangwe kubwa huku wachache wakiimba naye. Kiukweli Fid alimaliza show ilihali mashabiki walikuwa wamuhitaji.

Malaika Band katika ubora wao

CHRISTIAN BELLA

Bella ambaye alikuwa ni msanii wa pili kupanda jukwaani, ameendelea kuonekana ni bora zaidi katika show zake za live hali ambayo inamfanya awe ni miongoni mwa wasanii wanaohitajika zaidi kwa sasa.
Shangwe za mashabiki awapo jukwaani pamoja na kuimba nao mwanzo mwisho kumemfanya aendelee kuteka hisia za mashabiki wengi hasa wanawake.

Kwenye show hiyo, Bella alipanda jukwaani akiwa na Malaika Band pamoja na bodyguard wake wawili walioshiba.

Baada ya kuanza kuimba mashabiki walionyesha kufurahishwa na nyimbo za Bella, lakini Nani Kama Mama, Subira aliyoshirikishwa na Cassim Mganga na Nashindwa ni miongoni mwa nyimbo zilizopata shangwe kubwa sana.

Pia kama kawaida ya show za Christain Bella, kutunzwa pesa nyingi ni kitu cha kutegemewa.

Katika show hiyo tulishuhudia wasanii wakongwe wa filamu, Vicent Kigosi aka Ray pamoja na Steve Nyerere wakishindana kumtunza pesa Bella. Hakuna shaka kuwa kampeni za CCM zimetunisha mifuko yao!!

Diamond katika ubora wake ndani ya stage

DIAMOND PLATNUMZ

Hitmaker huyu wa Nana mwenye tunzo nyingi za kimataifa kwa sasa, alikuwa ni msanii wa nyumbani wa mwisho kupanda kwenye jukwaa kabla ya Wizkid.

Katika show hii Diamond alifanya vitu vikubwa sana kwenye kucheza hata nahisi kuliko wasanii wote lakini kuimba alikuwa wa kawaida.
Siku hadi siku Diamond tumekuwa tukiona akiwekeza zaidi kwenye kucheza hasa hasa kubadili aina ya uchezaji lakini binafsi nimemuelewa zaidi kwenye kucheza.

Ndio, kuimba anaimba vizuri sana lakini binafsi kuna kitu cha ziada nahitaji kukiona kutoka kwake hasa kwenye kuimba live.

Pamoja na hivyo, show ilikuwa kali sana. Naamini kama Wizkid aliangalia show yake, nadhani alipata sababu ya kwanini anaendelea kuwapiga bao kwenye tuzo za kimataifa.

Pia wakati Diamond yupo jukwaani tulishuhudia muigizaji wa filamu, Aunty Ezekiel akipanda jukwaani kumtia moyo mpenzi wake Mose Iyobo pamoja na kumwanga minoti ya kutosha. Hakuna shaka na huyu kampeni za CCM zimemwacha vizuri!

Wizkid akiimba kwa hisia

WIZKID

Huyu ni hitmaker wa wimbo, Ojuelegba ambaye aliyetua kwa mara ya kwanza Tanzania na kufanya show.

Kabla ya show mchana wake wakati anazungumza na waandishi wa habari, aliulizwa anauonaje muziki wa Tanzania pamoja na wasanii wake. Alisema unakuwa kwa kasi huku akisema anakubali muziki wa Diamond, Alikiba na Vanessa Mdee.

SHOW YAKE

Wizkid alichelewa kupanda jukwanii kwa sababu ya setting ya bendi yake. Lakini mwisho wa siku alipanda na wimbo wa Ojuelegba kwa shangwe kubwa sana.

Wizkid alishangaa mno kuona mashabiki wa muziki wa Tanzania wakiimba nyimbo zake kwa shangwe hali iliyomfanya atoke kwenye stage kubwa na kupanda kwenye spika za mbele ili aimbe akiwa karibu na mashabiki wake.

Hali hiyo ilivuta hisia za mashabiki wake hali ambayo ilimfanya ajaribu kuinyamazisha bendio yake mara kwa mara ili aimbe na mashabiki wake.

Baada ya Wizkid kuwa karibu na mashabiki wake, ilibidi ulinzi wa msanii huyo uongezeke maradufu ili kuhakikisha anakuwa salama.
Wizkid alizidi kupandwa na mzuka kadri muda ulivyokuwa ukienda baada ya mashakiki kuimba naye mwanzo mwisho hali iliyomfanya kurudia mara kwa mara nyimbo zake.

Wiz ambaye aliimba zaidi ya saa moja na nusu kutokana na kurudiarudia nyimbo kulikosababishwa na mzuka wa mashabiki, alizungumza mara kadhaa na uongozi wake usimharakishe kumaliza show kwa kuwa yupo na watu wake muhimu kwenye muziki wake.

Kutokana na mahaba aliyooneshwa na Watanzania, Wiz aliamua kugawa album zaidi nakala 20 kwa baadhi ya mashabiki waliojitokeza, lakini baadaye aliona zawadi hiyo haitoshi na kuamua kuwaahidi kufanya show ya bure iliyokuwa ifanyike Jumapili.

Hata hivyo alidali alikosa kibali na kuahidi atarudi tena Tanzania December kwaajili ya Fiesta.

DOSARI ILIYOTOKEA

Pamoja na yote mazuri yaliyotokea, jambo moja baya lilitokea ambalo uongozi wa East Africa Radio unapaswa kulifanyia kazi.
DJ Ommy Crazy wa EATV na EA Radio alifanya kitu kilichowaacha mdomo wazi mashabiki waliokuwa wamefurika na kuwakera vibaya.

DJ huyo alisikika akitukana matusi makubwa hadharani hali ambayo ilifanya aondolewa jukwaani huku mashabiki wakilalamika kudhalilishwa. Ommy alipokea ‘buuuuuuuu’ za kutosha.

Pia kulikuwa kuna dosari ndogo kwenye stage kwakuwa ilikuwa fupi sana hali ambayo ilisababisha baadhi ya watu kutoona vizuri kutokana watu wa VIP kulizingira stage!

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents